loader
Picha

Ahsanteni Benki ya Dunia, wengine waige

BENKI ya Dunia (WB) imeridhia kutoa dola za Marekani milioni 300, sawa na Sh bilioni 680 kwa Tanzania, kutekeleza mradi wa uongezaji ubora wa elimu ya sekondari kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununulia vifaa vya kufundishia.

Makamu wa Rais wa Benki hiyo Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem alimweleza Rais John Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam juzi kuwa mbali ya kutoa fedha hizo, itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.2, sawa na zaidi ya Sh trilioni 13, inayotekelezwa kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

Tunaungana na Rais Magufuli kuwashukuru WB kwa msaada wao huo mkubwa kwa wananchi wa Tanzania kuinua elimu, ambayo ni moja ya malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN).

Msaada wao umethibitisha maneno ya Rais Magufuli kuwa Benki ya Dunia hawatatuacha, na hivyo kuondoa sintofahamu iliyowakumba wananchi, kufuatia habari za kwenye mitandao ya jamii, zilizodai kuwa wanafikiria vinginevyo.

Ni jambo la kujivunia kwamba Tanzania inapata msaada huo mkubwa, wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa imeelekeza nguvu katika kutoa elimu bila malipo kwa watoto wote maskini, kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.

Ni matumaini yetu kuwa fedha hizo zitatumiwa vyema kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa na WB na kwa mujibu wa mipango ya Serikali ili kujenga miundombinu muhimu kwa elimu. Ni kupitia elimu, Tanzania inaweza kupiga hatua haraka zaidi katika harakati zake za kuleta maendeleo ya jamii kwa kuongeza wataalam wa fani mbalimbali za uzalishaji na huduma, kuinua uchumi wake kufikia wa kati ifikapo mwaka 2025, ukichagizwa zaidi na uchumi wa viwanda.

Tunaomba msaada wa WB, uendelezwe katika maeneo mengine ya huduma za jamii, kama afya, usafirishaji na kuzidi kuwasuta watu wote wakiwemo wanaharakati wasioitakia mema Tanzania iliyopania kuleta maendeleo makubwa.

Kwa mara nyingine, tunawashukuru WB na pia kuwapongeza kwa misaada yao ya hali na mali. Tunaomba wahisani zaidi, wanaoguswa na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuleta maendeleo kwa wananchi, nao kuiunga mkono.

Ni kwa msaada kama huu wa WB na wahisani wengine kama Umoja wa Ulaya (EU), Marekani na mashirika mengine makubwa ya maendeleo ya kimataifa, nchi kama Tanzania zitapiga hatua. Juhudi za Rais Magufuli kudhibiti rushwa,wizi, ubadhirifu serikalini na kukuza sekta za umma na binafsi katika uchumi, zinapaswa kuungwa mkono, kwa wahisani kutoa misaada zaidi ili wananchi wengi zaidi waboreshe maisha yao.

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, umekuwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi