loader
Picha

Hadithi: Pumzika Kwa Amani Inspekta-18

RPC Martine alipiga hatua moja ndefu ya kustukiza, akamkwapua yale makorokoro. Kemirembe akashindwa kumdhibiti, akajikuta kaisha yaachia mikononi mwa baba yake, huku akizidi kutetemeka kwa hofu na aibu. Kutokana na wingi wake, mengine yalianguka chini. Mwili mzima wa Kamanda uliishiwa nguvu. Ghafla akahisi kizunguzungu, akawa akitetemeka kwa hasira. Kila alipokuwa akivitazama vile vitu, alihisi Kemirembe anamfedhehesha kwa maksudi, ghafla akahisi kumchukia sana! Picha za Evodius Muganyizi Mutashobya, kadi, maua na barua za mahaba ndizo alizokuwazo mikononi mwake.

La Haula! Ndipo akaibaini siri nzito sana iliyojificha kiasi cha kumstaajabisha sana! Kwani pamoja na ujanja wake wote, na ufaulu wa mitihani yote aliyokabiliana nayo kama askari polisi mpaka kuwa Kamanda wa polisi wa mkoa, wanawe waliweza kumchezea faulo mbaya kiasi kile! Na wakati huo ndio alipofahamu kwamba, watoto wake wapendwa, wanamahusiano ya kimapenzi! ‘Mtu na dada yake!’ RPC Martine ilimbidi ajikaze kiume, vinginevyo angeanguka na kuzirai pale pale. Kila aliyeyashuhudia yale mabadiliko yake, alijisogeza kuvitazama vile vitu. Hakuna aliyeamini. Jipu lilitumbuka na kutoa usaa ulionuka jinamizi la mapenzi. Mwalimu mkuu hakuongea chochote, zaidi ya kuwataka wote, akiwemo Kemirembe, warudi ofisini. Na huko ndiko walipomuweka mtu kati, binti Kemirembe. Mwalimu Ndalawa alikuwa ni mtu mwenye upendo na uvumilivu mkubwa mno.

Mara zote huwa sio mtu wa kukurupuka, hususani linapokuja suala la maamuzi, hususani maamuzi magumu. Hutafakari kabla ya kuamua au kuzungumza na hutafakari mara mbili mbili juu ya kauli anayotaka kuzungumza na kuipima juu ya madhara na faida yake. Pia huzingatia sana kuisoma saikolojia ya mtu anayemkabili kimaamuzi, bila kujali alikereka au kukwazika kiasi gani. Ndivyo alivyojitahidi ku enenda hata katika kipindi hiki alichokuwa akimkabili Kemirembe, kwa mienendo yake .

Angeweza kufanya chochote, au kuamua kumpa adhabu ya moja kwa moja kwa mtazamo wa kumfunza adabu au kumkomoa, kwa sababu tabia alizozionesha ndani ya miezi miwili mfululizo, zilikera kwa kweli. Lakini haikuwa hivyo. Alimvutia subira, ndio maana aliamua kumuita mzazi wake. Walifika ofisini kwa mwalimu mkuu kwa mara nyingine na kuketi vile vile kama walivyokuwa wameketi awali. Kasoro tu Kemirembe, yeye alisimama katikati yao. Macho ya RPC Martine yalitengeneza vijifereji vya machozi ya uchungu na hasira yalimchuruzika taratibu. Mwalimu mkuu akamsihi awe mstahimilivu akiamini hayo mambo yangeisha tu. Ndiposa alipomtaka Kemirembe aieleze hadhira iliyomzunguka, nini kilikuwa kikiendelea. Kemirembe aliumia sana moyoni kwa hali ilipokuwa imefika. Alijiona mkosaji sana na hakumtendea haki kabisa baba yake kwa kumfanya adondoshe machozi mbele ya watu wazima namna ile kwa utovu wake wa nidhamu.

Akaadhimia kutokuendelea kumuumiza mzazi wake na jopo lote la walimu, akiwemo mwalimu mkuu aliyempenda, kumthamini na kumtegemea sana pale shuleni. Na sasa aligeuka kituko na kuwaangusha sana. Akaamua kuweka wazi kila kitu. Akasimulia kila hatua jinsi mambo yalivyokwenda mpaka alipojikuta akitumbukia kwenye penzi zito la kijana Evodius Muganyizi Mutashobya... kaka yake! Watu wote waliokuwemo mule ofisini walistaajabishwa na ile simulizi ya mapenzi yenye kusisimua sana. Iliyowahusu vijana wawili wa nyumba moja, waliopendana na kuhusiana ki mapenzi japo kuwa hawakuwahi kuonana.

Duh! Kukaibuka mjadala mrefu kidogo, huku Kemirembe akizidi kusisitiza kuwa hamjui Evodius. Upande mmoja wakisadiki usemi ule huku wengine wakipinga, wakidai kuwa Kemirembe alikuwa anawalaghai ili kumlinda Evodius. Waliopingana na Kemirembe walidai kwamba; Kemirembe anampenda sana huyo mvulana anayeelezewa, ambaye wao hawamjui.

Eti Kemirembe ndiye aliyemtongoza Evodius..! Wapi na wapi? Kama sio mpango wa Kemmy kumuepusha mpenzi wake na adhabu atakayopewa na baba yake... kamanda. Inawezekanaje msichana mdogo namna ile akapata ujasiri wa kumtongoza mvulana asiyemjua, wala hajawahi kumuona. Wakati huo huo akisistiza kuwa hajawahi kujihusisha na mwanaume yeyote yule ki mapenzi, hapo kabla.

‘Ndio kuanza mapenzi… ndio na kutongoza na wanaume!’ Watu wote hoi! “Msichana kumtongoza mwanaume huo ni zaidi ya umalaya! Hii inamaanisha Kemirembe na udogo wako wote huo, umeshakuwa malaya, malaya aliye kubuhu. Very shameful... shame to you... shame to your school and shame to your family!” Mwalimu mkuu alimshutumu kwa sauti ya chini yenye uchungu

. “Mi siku zote huwa nakuuliza, “What’s wrong with you?” you just hide to the bush. “Oh nothing teacher, oh nothing teacher...” THIS IS IT!” Mwalimu Ndalawa alizidi kulalamika kwa kiingereza akimaanisha kuwa Kemirembe amejitia aibu yeye, shule na familia yake yote. Pia alimshutumu kuwa alikuwa akimuuliza mara kwa mara ana tatizo gani lakini Kemirembe alikuwa akimkwepa kwepa tu na kumbe mambo yenyewe ndio hayo. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, kuhojiana na kukemeana, mwalimu mkuu aliamuru Kemirembe awapishe.

Kemirembe akatii kwa kuelekea nje kidogo ya eneo hilo. Kisha mazungumzo ya kiutu uzima yakafanyika. Kila mmoja akatoa dukuduku lake na mtazamo wake kuhusu hatima ya Kemirembe. Kwani kulikuwa na dalili kwamba hali haikuwa nzuri. RPC Martine akachekecha akili yake, hatimaye akapata jawabu. Akauomba uongozi wa shule umsamehe Kemirembe.

Pia wamruhusu aendelea na masomo, kisha nini atakifanya, akaomba wamuachie yeye. Mwalimu mkuu akajaribu kumbana RPC Martine ili kujua iwapo alifikiria kumpa adhabu kubwa, pindi binti yake atakapo kuwa likizo. Kamanda Martine akakanusha kabisa wazo lile. Akasisitiza kwamba hawezi kumwachisha shule binti yake wa pekee, hatakuwa akimkomoa bali kujikomoa mwenyewe. Majibu ya baba Kemirembe yalimfurahisha sana mwalimu mkuu pamoja na wenzake. Wote hawakutaka kabisa Kemirembe asitishwe masomo.

Kwani yule ni mtoto wa kike, na adhabu kama ile, ingemgharimu sana kwenye dunia inayokua kwa kasi kwenye eneo la utandawazi. Bali njia za busara zitumike ili kumrekebisha. Baadae Kemirembe aliruhusiwa kuingia ofisini. Akastaajabu sana, tofauti na matarajio yake, aliziona sura zote zikikuwa zimepoa kwa utulivu mkumbwa. Tofauti sana na hapo awali ambapo sura zote zilitawaliwa na hasira.

Ghadhabu. “Kemerembe.” Mwalimu mkuu akaanza. “A...aaa...bee...eee...mwa... aalimuuuu.” Kemiremba aliitikia sanjari na kilio cha kwikwi. Nafsi ilimsuta na hakuamini jinsi sauti ya mwalimu mkuu ilivyopoa. “Hautaki kusoma?!” Kwa upole zaidi uliombatana na lafudhi ya kinyamwezi, mwalimu Ndalawa alimsaili.

“Natak...nataa aaa kaaa aaahahaha... agriiii mama yangu weee. Baba na walimu jamani naomba nisamehewe mimi jamani iiii...iiii” Kemirembe alimjibu huku akilia na kutetemeka kwa hofu. “Una uhakika?” “Ndiyo mwalimu.” “Kweli?” “Ndiyo.” “Kivipi..! Utawezaje kusoma kama kweli unapenda kusoma, wakati unampenda Evodius kiasi cha kushindwa kuhudhuria vipindi darasani!?” Mwalimu mkuu akawa makini kuisoma saikolojia ya Kemirembe. “Nisamehe mwalimu, nimekosa sana...aah aaah...nimekoma mimi ooohooo...uuuuh...uuuh...” Toba ya Kemirembe ilimfariji kila mtu. Kitendo cha kukiri kosa na kutubu, kilimaanisha kujirudi kwenye mstari mnyoofu.

“Sijakuambia ulie, jibu swali langu. Utawezaje kuendelea na masomo wakati mapenzi yana kupeleka puta! Na hauwezi tena kuhudhuria vipindi darasani. Na sijui kama unajua kwamba uko kidato cha pili, si unakabiliwa na mtihani wa kitaifa wewe…au?!” “Ndiyo” “Your not serious my daughter.” Kwa mara nyingine Kemirembe aliangua kilio, huku akizidi kuomba radhi. “Look at me Kemirembe... niatazame usoni Kemirembe.” Mwalimu mkuu alimuamuru. Akamtazama.

“Tumekusamehe. Sisi kama shule tumekusamehe. Baba yako mzazi pia amekusamehe… sio kwa sababu madudu unayoyafanya ni mazuri mno la hasha....” Akaendelea “...ni kwa sababu tunakupenda sana. Tazama ulivyomtesa mzazi wako, umemuumiza sana baba wa watu asiyekuwa na hatia. Umemvua nguo baba yako. Lakini wahenga walisema uchungu wa mtoto aujuaye mzazi. Baba amekusamehe pia.” Akameza mate. “Hatutakupa adhabu yoyote, tunachotaka ubadilike kuanzia sasa… ubadilike kuanzia...?

” Mwalimu Ndalawa hakumalizia sentesi yake, badala yake alibaki akimtumbulia macho Kemirembe yenye ishara ya kumtaka kuimalizia ile sentensi. “Sasa.” Kemirembe aliimalizia. Kamanda Martine naye alipewa nafasi aongee, kama mzazi akamuhusia mwanae kubadilika. Akamuhadharisha kuwa huko aendako, akiendelea na michezo ya kijingajinga, atakuja kujutia sana.

Walimu wengine pia waliokuwepo pale walitoa yao ya moyoni, na kumsihi ajirudi na kuwa Kemirembe yule wanaemfahamu. Hakupewa adhabu yoyote, lengo likiwa kutozidi kumvuruga kisakolojia na kiakili. Akahusiwa sana juu ya hatari na athari ya kuchanganya masomo na mapenzi. Akaruhusiwa kurudi bwenini kujiandaa ili aingie darasani. Inaendelea…..

Facebook; Egidius Jack Matungwa

Instagram; egidiusjack5

Email:egidiusjack@gmail.com

0715499002

HIVI karibuni Wizara ya Nchi Ofi ...

foto
Mwandishi: Egidius Jack Matungwa

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi