loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Chumba cha Daktari: Tambua sabau za tumbo kujaa gesi

Tumbo kujaa gesi ni tatizo linalowapata watu wengi na wakati mwingine linasababisha usumbufu katika kazi za kila siku au kwenye shughuli za starehe. Gesi inapojaa tumboni tumbo linaweza kuvimba, kuwa gumu na wakati mwingine kuuma kama vichomi.

Hewa inayoingia tumboni ni mchanganyiko wa gesi ya oksijeni na naitrojeni, aina hizi mbili za gesi zinachanganyika na gesi ya kaboni dayoksaidi inayotengenezwa kwenye njia ya mfumo wa chakula. Asilimia kubwa ya gesi za oksijeni na kaboni dayoksaidi zinaingia kwenye mishipa ya damu kwa ajili kufanya kazi ndani ya mwili na kiasi kikubwa cha naitrojeni hutolewa nje ya mwili kupitia njia ya haja kubwa.

Njia kuu za kutoa hewa iliyoingia mwilini ni kwa kubeua au kupitisha hewa kwenye njia ya haja kubwa. Mara nyingi gesi tumboni inaletwa na chakula ambacho hakijameng’enywa vizuri au kumeza kiasi kikubwa cha hewa. Mtu anapokula au kunywa, anameza kiasi fulani cha hewa, hata hivyo zipo baadhi ya sababu zinazofanya mtu ameze kiwango kikubwa zaidi cha hewa na kusababisha tumbo kujaa gesi. Sababu hizi ni pamoja na kula au kunywa kwa haraka, kutafuna pipi aina ya chewing gum (Big G), na kuvuta sigara. Vilevile endapo kuna hitilafu katika mfumo wa kupitisha chakula ambayo inapunguza kasi ya kutoa gesi mwilini, gesi hii hubaki tumboni na kusababisha karaha kwa aliyeathirika.

Dalili kuu ya tatizo la tumbo kujaa gesi ni kutoa hewa mara kwa mara kupitia mdomoni (kubeua) au kwenye njia ya haja kubwa, kuwa na milio kama muziki ndani ya tumbo, tumbo kuwa kama limebanwa kiasi cha kusababisha kufungua mkanda au kulegeza nguo iliyovaliwa. Mtu mwenye tatizo la kujaa gesi mara kwa mara anashauriwa kupunguza matumizi ya vinywaji vyenye carbon (mfano Coca Cola au Pepsi Cola) au baadhi ya vyakula vinavyoleta gesi kama kabichi (cabbage) au maharagwe makavu; kupunguza utafunaji wa bigi G na kula chakula kwa taratibu. Kufanya masaji kwenye tumbo kunaweza kupunguza hisia ya maumivu ya tumbo lililojaa gesi.

Zipo dawa za kutumia endapo tumbo limejaa gesi, hata hivyo ni vizuri kupata ushauri wa mtaalamu kuliko kutumia dawa hasa kama tatizo hili linajirudia rudia. Ni muhimu kumuona mtaalamu wa afya kwa kuwa yapo baadhi ya magonjwa ya njia ya mfumo wa chakula ambayo yanasababisha tumbo kujaa gesi; hasa magonjwa kwenye utumbo mkubwa.

Dalili ambazo zinaweza kuashiria kuwepo tatizo la kujaa gesi tumboni ni pamoja na hali ya kujaa gesi kujirudia-rudia, kuharisha hasa kuharisha damu, kuambatana na kutapika au homa, kukosa hamu ya kula au damu kupungua mwilini.

Vilevile tumbo linaweza kujaa kwa sababu ya magonjwa megine kama ya figo, moyo au ini.

Endapo una dalili kama hizi ni vizuri kuhudhuria hospitali ili kupata ushauri zaidi na mtaalamu wa afya anaweza kufanya vipimo ili kuweza kubaini endapo una tatizo kubwa na kukupa tiba sahihi. Faraja Chiwanga ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba na Mbobezi wa magonjwa ya Homoni.

Faraja Chiwanga ni Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Tiba
na Mbobezi wa magonjwa ya
Homoni. Simu: 0786587900.

Naamka asubuhi,  sioni kilongalonga, 
Napapasa kitandani,  hamadi hiki hapa,  

foto
Mwandishi: Faraja Chiwanga

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi