loader
Picha

Bei ya saruji ‘yanukia’ kuwa chini ya 10,000/-

MATUNDA ya uwekezaji mkubwa katika kiwanda cha saruji uliofanywa mkoani Mtwara na bilionea namba moja Afrika, Aliko Dangote huenda yakaanza kuonekana kuanzia katikati ya mwaka ujao na hivyo kuleta unafuu na mapinduzi makubwa katika sekta ya ujenzi nchini na pengine Afrika Mashariki kwa ujumla.

Inaelezwa kuwa kufikia mwakani huenda saruji ya kiwanda hicho ikashuka na kuwa chini ya Sh 10,000 kwa kila mfuko mmoja wa kilo 50 kama ilivyokuwa dhamira ya mwekezaji.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Blasius Byakanwa alipokuwa anazungumzia maendeleo ya viwanda na biashara katika mkoa wake, hasa katika kipindi hiki ambacho Watanzania wanaiangalia miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli inayohimiza ujenzi wa viwanda ili kuisaidia nchi kupiga hatua za kimaendeleo kwa kasi na pia kusaidia kukuza ajira.

Alisema kutokana na kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa umeme kiwandani hapo baada ya kuunganishwa na nishati ya gesi, hali ya uzalishaji inatarajiwa kuimarika. “Hivyo muda si mrefu faida ya uwekezaji huu unaotokana na juhudi za serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji itaanza kuonekana kwa kuona saruji ikipatikana kwa wingi, lakini pia bei ikishuka pengine hata kufikia Sh 8,000,” alisema.

Kwa sasa bei ya saruji sokoni ni kati ya Sh 13,500 na Sh 15,000. Nyakati za uhaba, bei ya saruji hufikia hadi Sh 19,500. Moja ya malengo ya Dangote yalikuwa kuzalisha saruji itakayotosheleza soko la ndani na nchi jirani, huku kivutio kikubwa kikiwa katika being nafuu, lakini kwa bidhaa yenye kiwango cha kimataifa.

Hata hivyo, katika miaka mitatu ya awali, uzalishaji wake haukuwa mzuri sababu ikielezwa kuwa ni gharama kubwa za uzalishaji, hasa nishati ya umeme kwani kiwanda kilitegemea zaidi dizeli kuendeshea mitambo yake.

Hali hiyo ilimlazimu Rais John Magufuli kuingilia kati na kuagiza uwekezaji wa kiwanda hicho apewe gesi kwa ajili ya matumizi ya kiwanda chake, agizo ambalo limetekelezwa na kukamilika kwa awamu ya kwanza ambapo jumla ya megawati 45 zinazalishwa.

Uzinduzi wa umeme unaotokana na nishati ya gesi, ulizinduliwa Septemba mwaka huu na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani ambaye alieleza kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria mazingira rafiki kwa uwekezaji nchini.

Uongozi wa kiwanda cha Dangote ulielezea kufurahishwa na uamuzi wa kukipatia umeme wa gesi kiwanda hicho, huku wakisema gharama za uzalishaji zitapungua. Kwa upande wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), likieleza kuwa manufaa ya gesi yanazidi kuongezeka hasa katika matumizi ya viwandani, ambapo tayari viwanda vingi vikubwa sasa vinatumia gesi kama chanzo cha nishati.

Viwanda Mtwara Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, mkoa una jumla ya viwanda vya kati 17, kati ya hivyo 18 ni vya kubangua korosho, vinne vya maji ya chupa, viwili cha kuchakata gesi, Madimba na Msimbati, kimoja cha mazao yatokanayo na gesi na vingine viwili vya saruji.

Kwa ujumla, viwanda hivyo vimetoa ajira za kudumu 4,442. Aidha, mkoa una viwanda vidogo 2,582 ambavyo vimetoa ajira za muda 19,190. Tayari kampuni nne zimeonesha nia ya kujenga viwanda, viwili vikiwa vya kubangua korosho, cha mbolea na kingine cha kusindika mazao.

Byakanwa amesema, mkoa katika kuitikia mwito wa Rais Magufuli wa ujenzi wa viwanda, mkoa umebainisha maeneo yenye ukubwa wa hekta 5,821.19 kwa ajili ya kujenga viwanda, hatua inayotajwa kuwa ni fursa kwa wawekezaji wakubwa na wadogo kuwekeza kwenye viwanda.

Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikihitimiza mikoa kutenga maeneo ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda ili kuifanya nchi ijengwe na uchumi wa viwanda, hatua itakayosaidia kuipeleka nchi katika uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga ameonesha kukerwa na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Mtwara

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi