loader
Picha

Sheria mpya ya mafao kunufaisha wengi

MAMLAKA ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imefafanua kuhusu vikokotoo vya pensheni ikisema vimeanza kutumika tangu 2014, kuwa kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii hakujapunguza vikokotoo hivyo.

Imesema kilichobadilika ni kiwango cha mkupuo kwa kundi dogo la wanachama takribani asilimia 20 ya wanachama wote wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini waliokuwa wakipokea mkupuo wa asilimia 50, kwamba sasa ili wawe sawa na wanachama wenzao wa mifuko mingine wanaopokea asilimia 25.

Aidha, imesema si wakati mwafaka kuilaumu serikali hasa inaposimamia misingi ya hifadhi ya jamii.

Ufafanuzi huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka jana, baada ya kuwapo kwa taarifa mbali mbali kuhusu kupungua kwa vikokotoo vya pensheni baada ya kuunganishwa mifuko.

Agosti mosi, mwaka huu, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ulianza rasmi ukiwa ni utekelezaji wa Sheria Namba 2 ya 2018, ambayo pamoja na mambo mengine, iliunganisha mifuko ya pensheni minne ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda mfuko mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma yaani PSSSF.

Sambamba na kuanzishwa kwa PSSSF, sheria hii ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Sura ya 50 ili kuufanya mfuko wa NSSF kuwa utakaohudumia wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.

Isaka alieleza jana kuwa hivi karibuni kumetokea upotoshaji kwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwamba kwa kuunganisha mifuko, serikali imepunguza vikokotoo vya pensheni.

Alisema jambo hilo si kweli, kwani vikokotoo vinavyotumika vilianza kutumika tangu Julai Mosi, 2014; na tayari wastaafu wa mifuko ya pensheni ya NSSF na PPF ambao ni wengi walishakuwa wakipokea pensheni kwa kikokotoo hiki.

“Mwaka 2014 ilikubalika kwamba wanachama wa PSPF na LAPF ambao walikuwa kwenye mifuko hiyo kabla ya Julai Mosi, 2014 waendelee na kikokotoo cha 1/540: 15.5 na mkupuo wa asilimia 50. “Hivyo ukisoma kwa makini Sheria Namba 2 ya Mwaka 2018 iliyounda mfuko wa PSSSF Kanuni za Mafao: Public Service Social Security (Benefits Regulations) zilizotolewa imezingatia kwa kina jambo hilo.

Nafikiri si wakati muafaka kuilaumu serikali,” alieleza bosi huyo wa SSRA. Aliwaondoa hofu wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwamba kikokotoo hicho sio kipya kwani kimetumika kwa muda wa miaka minne tangu 2014.

Aliwashauri kutembelea tovuti ya SSRA walinganishe Amri ya 2014 na Kanuni za 2018. “Kilichobadilika ni kiwango cha mkupuo kwa kundi hili dogo la wanachama takriban asilimia 20 ya wanachama wote wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini waliokuwa wakipokea mkupuo wa asilimia 50 kwamba sasa ili wawe sawa na wanachama wenzao wa mifuko mingine wanaopokea asilimia 25,” alisema Isaka.

Alieleza kuwa haikuwa sahihi kundi dogo la wanachama kulipwa mkupuo mkubwa. “Taarifa halisi za malipo zinaonesha kwamba mwanachama wa PSPF/ LAPF anapokea mkupuo ambao ni zaidi ya mara tatu ya michango aliyochanga kwa kipindi chote cha ajira yake tofauti na wanachama wenzake waliopo mifuko mingine kama vile NSSF na PPF.

“Tungependa kusisitiza kwamba hii asilimia 25 iliyopunguzwa kwenye mkupuo imewekwa kwenye pensheni ya mwezi ambapo pensheni ya mwezi imeongezeka kwa asilimia 50. Kwa hiyo si sahihi kusema wanachama wamepunjwa mafao yao,” alifafanua zaidi Isaka.

Alisema lengo la kuinganisha mifuko ni pamoja na kuweka usawa kwa wanachama kwa kuwa wote wanachangia asilimia 20.

“Tena kwa watumishi wa umma, serikali ambaye ni mwajiri anawachangia asilimia 15, mtumishi anachangia asiliami tano. “Je, ni sawa mwanachama wa NSSF anayechangia asilimia 10 apate mkupuo asilimia 25 wakati mwenzake wa PSPF anayechangia asilimia tano apate asilimia 50, kwa nchi inayofuata misingi ya Hifadhi ya Jamii (Solidarity Principle),” alihoji. Aidha, Isaka alisema malalamiko ambayo SSRA imepokea na kuanza kuyafanyia kazi ni kwamba wanachama wa PSPF walikopa mikopo ya nyumba kwa kutegemea watalipwa mkupuo wa asilimia 50.

“Hivyo kwa kuwa sasa wanapokea asilimia 25 wanaona kwamba mkupuo hautoshi kulipa deni la nyumba. Hili si jambo gumu kwani kunaweza kufanyika makubaliano na mfuko kuona namna ya kuondokana na changamoto hiyo,” alieleza.

Alisisitiza kwa kuwahakikishia wanachama kwamba pensheni hailipwi kwa miaka 12.5 tu, bali kwa muda wote wa uhai wa wastaafu. Pia kwa wastaafu wa PSPF na LAPF bado wanapokea kikokotoo cha 15.5 na si kikokotoo cha 12.5 kama inavyopotoshwa.

Ili kuhakikisha wastaafu hawapunjwi na mfuko mpya wa PSSSF, alisema SSRA imetuma wakaguzi maalumu kujiridhisha kwamba ukokotoaji umefanyika kwa mujibu wa kanuni na taratibu. Hivi karibuni, baada ya kutolewa kwa taarifa kuhusu kuanza kwa mfuko wa PSSSF, baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa walikuja juu na kudai kuna mabadiliko ya vikokotoo yenye nia ya kuwapunja mafao wastaafu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, alidai sheria hiyo mpya inamuumiza mtumishi mwenye kipato cha chini katika mafao yake pindi anapostaafu.

Wadau wataka elimu zaidi itolewe Katika hatua nyingine, wadau mbalimbali wamesema elimu kwa umma inahitajika zaidi kwani inaonekana wadau hawajaelewa namna ambavyo ukokotoaji unafanyika na nini manufaa kwa wastaafu. Ofisa Mwandamizi wa Serikali mstaafu, Isaac Mruma alisema elimu ya kutosha haijatolewa kwa wadau wa sheria hiyo pamoja na kanuni zake, jambo ambalo linawafanya watu kupotosha.

“Nadhani elimu haijatolewa ya kutosha kwa wadau ndio maana tunaona watu wanatoa maoni mbalimbali yasiyo na ukweli lakini mimi mpaka sasa sijaona athari yoyote kwa mstaafu, hiyo miaka 12.5 haijatajwa kokote kwenye sheria, bali imetajwa kwenye kanuni ya kukokotoa,” alisema Mruma. Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya alisema tatizo linalojitokeza sasa ni elimu ndogo kwa umma juu ya ukokotoaji wa mafao ambapo ameshauri kuendesha kampeni kubwa ya kutoa elimu.

Alisema hata hivyo TUCTA inaendelea kufanya majadiliano na serikali kuona namna bora ya kuboresha mafao ya mstaafu lakini pia kuhakikisha mifuko ya hifadhi za jamii haifi. Makamu Mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwete aliishauri serikali kuongeza fao la kuanzia, yaani isiwe mstaafu anapata asilimia 25 mwanzo na asilimia 75 aipate kwa miaka 12.5 badala yake fedha ya mwanzo apewe angalau asilimia 40.

Alisema pia kuwa malalamiko juu ya ukokotoaji huo umekuja kwa sababu watumishi wengi walikuwa wakikopa asilimia 25 ya mafao yao lakini kwa ukokotoaji wa sasa watakapokwenda kuchukua mafao watajikuta hawana kitu kwani walishazichukua kama mkopo.

“Mtu mwenye mipango hata kidogo fedha hiyo ya mwanzo yaani asilimia 25 haitamfaa atashindwa kujipanga na kuanzisha miradi ya kumsaidia kuishi, kabla mradi haujakaa vizuri fedha imeshaisha kwa hiyo kwa ushauri wangu ingeongezwa angalau ya mwanzo iwe asilimia 40,” alisema Profesa Mbwete. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema sheria na kanuni zake zimetungwa na serikali na serikali ya awamu ya tano ni sikivu itapokea maoni ya watu na kufanya mabadiliko yanayofaa.

Imeandikwa na Mgaya Kingoba na Regina Mpogolo.

SERIKALI mkoani Songwe imewataka wakulima wa zao la alizeti kubadilika ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu, Dar es Salaam

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi