loader
Picha

Vijana nao wamsaidie JPM kujenga Tanzania ya viwanda

TANGU alipoingia madarakani, Rais John Magufuli ameonesha nia ya dhati ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati kupitia viwanda na suala hili limepokewa kwa mikono miwili na Watanzania.

Hii ndiyo sababu hivi sasa maneno Tanzania ya viwanda yanatamkwa kijasiri na Watanzania karibu wote ukiachilia mbali vibaraka wa mabepari wa nje. Katika ufafanuzi wake kwa nyakati mbalimbali, Rais Magufuli amekuwa akielezea faida za nchi kuwa katika uchumi wa viwanda akisisitiza kuwa, hali hiyo itaongeza ajira kwa vijana na itapunguza mzigo kwa taifa kununua nje bidhaa kwa bei kubwa.

Badala yake, Rais anaelimisha kuwa, kuuza malighafi nje kwa bei ndogo na kisha malighafi hiyo ikaongezwa thamani na kurudishwa nchini na kuuzwa kwa waliozalisha kwa bei kubwa, ni sawa na kujikaanga kwa mafuta yetu wenyewe.

Kwa msingi huo, anataka Watanzania wazalishe kwa juhudi na maarifa mazao na rasilimali mbalimbali kisha kabla ya kuuza, wasindike na kuongeza thamani bidhaa zao ili waziuze katika ubora wa juu unaowaongezea tija katika bei huku wakiwa wamewafaidisha Watanzania wenzao hata kwa ajira.

Mchakato huo wa kuongeza thamani badala ya kuuza malighafi, utawagusa na kuwanufaisha hata wazalishaji wa shambani kwa kuwa viwanda vingi hutegemea mazao ya shambani, hivyo Tanzania ikiwa ya viwanda, hata wakulima watanufaika kwa kuuza mazao yao kwa bei yenye tija na isiyowapa hasara.

Rais amekuwa muwazi katika hili na suala la utetezi wa maslahi ya wakulima na ndiyo maana hata hivi karibuni, aliagiza korosho zinazouzwa kwa wafanyabiashara, zisiuzwe chini ya Sh 3,300 kwa kilo, na kama wafanyabiashara wanasita kufanya hivyo, serikali iko tayari kuzinunua na kutumia hata magari ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuzisomba.

Wengi walifikiri ‘anapiga mkwara’, lakini Rais wetu anatembea juu ya maneno yake kwa kutekeleza anayoyaamini na kuyasema akimini yanaletya tija kwa taifa. Hivi sasa serikali inanunua korosho na kazi hiyo imekabidhiwa kwa JWTZ baada ya Mkuu wa Majeshi, Venance Mabeyo kumhakikishia Rais Magufuli kuwa JWTZ ipo tayari kwa kazi hiyo.

Kimsingi, hadi mkuu wa nchi kuamua hivyo, ni wazi ndani ya ‘wanaomchekea’ au basi niseme aliotarajia wawajibike ipasavyo kuwezesha matamanio yake, wapo wasaliti wanaomchekea huku ‘wanakula mbao za nyumba yake’ kimyakimya kama mchwa mharibifu.

Hao pia wamo baadhi ya wasaidizi wake na watendaji wa serikali wasio waadilifu maana penye msafara wa mamba kenge hawakosekani; ndio hao ambao mbele yake na mbele ya kadamnasi, wanajidai wanamuunga mkono, lakini wanamsaliti bila kujua kuwa, kumsaliti au jaribio lolote la kumsaliti au kumhujumu Rais wa Nchi aliyechaguliwa na watu ili kuongoza watu, ni kuwahujumu wananchi kwa jumla na ndiyo maana hawafanikiwi.

Kibaya kwa hao ni kwamba, wanapokuwa wenyewe gizani ‘wanachumia tumbo na kuganga njaa zao’ huku wakijua kuwa Mkuu hataki hilo na kwamba hii ni Tanzania mpya ya Watanzania wote wakiwamo wakulima na wanyonge wengine. Hao ndio ninaomwomba Rais azidi kuwa makini dhidi yao kwani wengine ‘wamelalia’ katika nafasi zao; wapo usingizini.

Wanataka kila kitu, lazima Rais aje ndipo kipate ufumbuzi kwa manufaa ya taifa jambo ambalo sio jema na hao, wanapaswa ‘kufyekelewa mbali’ mapema. Hao viongozi, watendaji na watu wengine wa namna hiyo, wanadhani kila jambo ‘linapigwa kisiasa’ na ndio wanaojaribu kuliyumbisha taifa kwa kutaka kila jambo liingizwe siasa na tunamshukuru Mungu kwa Rais wa Nchi hii kuwa makini dhidi ya mambo kama haya na pia, ‘kutoyachekea’.

Hapa niseme tu nikimuomba rais akaze uzi dhidi ya watu wa namna hiyo kwani hatuwezi kuwa na amani kama tutafanya kosa la kuilazimisha siasa kuwa mbele ya watalaamu. Nijuavyo mimi, wataalamu hawafuati siasa, bali siasa ndiyo huwafuata wataalamu.

Amani haitakuwapo kama taifa tuitaruhusu wanasiasa watafute umaarufu wa kisiasa kwa gharama na sheria za kanuni za kuendesha nchi na ndiyo maana ninasema, ninafurahi na kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano kwa kutojaribu kuwachekea wanaotaka kuzoea mchezo huo maana ukimchekea nyani, utavuna mabua na furaha ya wanasiasa wachache isiwe gharama ya wananchi.

Ninaposema yote haya, niwahimize na vijana pia kutambua kuwa hatuwezi kujenga uchumi wa viwanda, kama wote tutakimbilia mijini na kuwaachia wazee kazi ya kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi popote duniani.

Tutambue bila kusubiri kuambiwa na mtu ukweli kuwa, tukirogwa kukubali ugonjwa huo, tutajenga viwanda ambavyo kesho na kesho kutwa, vitakufa kwa njaa ya kukosa malighafi kutoka shambani. Ni kwa msingi huo ninasema, tumuunge mkono Rais Magufuli kwa maono yake kwa vijana wote kukubali kubaki vijijini na kuzalisha shambani ili viwanda tunavyojenga nchini, vipate malighafi.

Tangu vijijini, ndugu, jamaa na marafiki waione kuwa ni aibu na usaliti kwa taifa, kuwaacha vijana wao au wenzao kukimbia kilimo kitakacholipatia taifa tija, eti wakakimbilia mjini kuuza karanga, chips na Big G. Hii ni aibu, ni kumsaliti kiongozi wetu wa nchi anayetuonesha njia kuelekea nchi ya ahadi; nchi ya maziwa na asali; anayetutoa katika jehanamu ya mateso ya uchumi.

Kufanya hivyo ni kulisaliti taifa na kunajisi uzalendo unapotakiwa. Watanzania wote tutambue na kumsaidia Rais Magufuli kuonesha ukweli kuwa, Tanzania haitajengwa na vijana wanaokimbia kilimo, eti wakakimbilia kucheza ‘pool’ kwenye baa, kubeti na kutumia walicho nacho kwa michezo ya kubahatisha. Taifa likiwa na utitiri wa mambo hayo, linaelekea shimoni.

Tuungane kumsaidia Rais wetu anayekesha usiku na mchana kutafuta na kutuonesha ‘njia iendayo uzimani’ michezo hii ya kubeti na bahati nasibu, inatupeleka shimoni japo wananchi tunakosea kushangilia.

Watanzania tumebahatika kupewa na Mungu zawadi ya Rais John Magufuli anayetaka tufanye kazi kwa juhudi na maarifa kupitia kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, hivyo mambo mengine yakiwamo ya kutaka utajiri kupitia michezo ya bahati nasibu na kubeti, ni kumsaliti au kumhujumu Rais wetu jambo ambalo hakuna mwenye akili timamu atakayelibariki.

Ninaamini kwa dhati kuwa, kila kijana kijijini akilima japo eka moja na kuihudumia vizuri katika zama hizi ambazo Rais anaonesha waziwazi kujali, kupenda na kusimamia maslahi ya wakulima, hakuna kijana au mvivu yeyote ambaye atakaimbilia mjini maana faida ya kilimo vijijini sasa inaonekana.

Hii ni kwa kuwa, mbolea na pembejeo zitapatikana kwa ukaribu, unafuu na ubora, na pia soko litapatikana. Hilo litawezesha tija kwa wakulima huku viwanda vyetu vikipata malighafi, bila kulazimika kuzitafuta nje ya nchi. Ndiyo maana ninasema, vijana nao wamsaidie JPM kujenga Tanzania ya viwanda.

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi