loader
Picha

Mkojo wa sungura Tabora unavyonufaisha wakulima

JE, umewahi kusikia kwamba mkojo wa sungura unatumika kama dawa ya kuulia wadudu shambani, lakini pia kurutubisha udongo? Ukweli ndio huo kwamba mnyama huyo anazidi kupanda chati kutokana na ukweli kwamba ufugwaji wake siyo kwa ajili ya nyama pekee kama ilivyokuwa awali, lakini mkojo wake ni mkombozi kwa wakulima hasa katika kupambana na wadudu waharibifu wa mazao.

Kwa kawaida sungura ni wanyama wa jenasi mbalimbali katika familia Leporidae ambao wanaweza kukimbia kwa kasi sana. Baadhi ya wanyama hao hasa wanaoishi Ulaya huweza kukimbia hadi kufikia umbali wa mpaka kilometa 72 kwa saa. Kipindi cha zamani, sungura alizoeleka sana kuwindwa hasa kwa ajili ya kula nyama, lakini siku za hivi karibuni, mnyama huyo amekuwa kati ya wanyama wanaofugwa kwa kasi kama vile ng’ombe, mbuzi, nguruwe na kondoo.

Kama ilivyo kwa wanyama wengine wafugwao, sungura naye kinyesi chake si jambo la ajabu kutumika kama mbolea shambani au kwenye bustani, lakini tofauti na wanyama hao wengine wafugwao, sungura sasa ana thamani zaidi baada ya kugundulika kwamba mkojo wake ni dawa ya kuulia wadudu shambani. Wajasiriamali wa mkoa wa Tabora baada ya kung’amua siri hiyo, imewaletea manufaa katika mashamba yao na kuvuna kwa wingi lakini pia kwa wafugaji wa sungura imewaongezea kipato kutokana na kuuza mkojo huo kwa wakulima.

Mmoja wa wajasiriamali aliyeshiriki kwenye maonesho ya Jukwaa la Fursa za Biashara Tabora, Rahel Mghenyi, anasema mkojo wa sungura tangu wajulishwe kwamba ni dawa ya wadudu shambani na walipoutumia wakaona mafanikio, umekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima hasa wa mahindi, mtama na mboga. Anasema mkoani humo wajasiriamali wameunda umoja wao ambao yeye ndio Katibu wao ambapo hualika wataalamu mbalimbali ili kupatiwa mafunzo na moja ya mafunzo waliyoyapata ni pamoja na namna ya kufuga sungura.

“Tumebaini kuwa ufugaji wa sungura una faida kubwa sana pamoja na kumuuza kwa ajili ya nyama, lakini pia kinyesi na mkojo wake vina faida kwa kuwa hutumika kama dawa ya kuulia wadudu shambani,” anaeleza.

Anasema walianza kufuga kwa wingi sungura baada ya kuwanunua wakiwa na umri mdogo kwa Sh 60,000 mpaka 80,000 ambapo hukua na kuzaliana kwa haraka. “Jambo la msingi ni kujua faida za kufuga mnyama huyu, sisi baada ya kugundua thamani ya mkojo wake, tulipatiwa mafunzo ya kujenga banda la kuwafuga ambalo hutengenezwa maalumu na kuwekewa ‘gata’ kwa ajili ya kuvuna mkojo na kinyesi chake,” anaeleza Mghenyi.

Anafafanua kuwa kwa wastani, sungura mmoja mkubwa huzalisha si chini ya robo lita ya mkojo kwa siku. Idadi ya sungura ndiyo inayochangia mfugaji kuvuna mkojo na kinyesi kingi kwa siku. Anasema kwa kutumia ‘gata’ na chombo maalumu kama ndoo au galoni, hukusanya mkojo huo na kisha kuutenganisha na uchafu na kuuhifadhi katika galoni tayari kwa matumizi shambani.

Hata hivyo, anabainisha kuwa mkojo mwingi wa sungura hutokana na chakula anachopatiwa ambacho mara nyingi huwa ni nyasi, mboga kama vile kabichi, karoti, spinachi na mchunga, lakini pia huwa na chakula maalumu kinachouzwa kwenye maduka ya vyakula vya mifugo. Anasema baada ya kupata mkojo mwingi wa sungura, wajasiriamali hao huuza mkojo huo na mwingine kuutumia kwenye mashamba yao ambapo pamoja na kurutubisha udongo na kuua wadudu, pia husaidia uzalishaji kwa wingi wa zao husika.

Mghenyi anaelezea namna ya kutumia mkojo huo kwa ajili ya kurutubisha na kuulia wadudu shambani kuwa ni kuuchanganya na udongo na kisha kuuacha kwa muda wa siku 21 na baada ya hapo unakuwa tayari kwa matumizi shambani. Anasema mara nyingi katika kikundi chao kupitia mashamba yao ya mahindi na bustani za mboga, wanatumia mkojo huo uliochanganywa kama mbolea na kuutupia kwenye mashimo ya mimea ambapo huua mara moja vimelea vya wadudu lakini pia kurutubisha udongo.

“Sikufichi tangu tumeanza biashara hii, mkojo huu wa sungura umekuwa na soko kubwa sana hapa Tabora, wakulima wengi wanatukimbilia. Pamoja na kwamba tunauza kwa maelewano lakini lita moja huuzwa kuanzia Sh 15,000 hadi Sh 20,000,” anafafanua.

Mjasiriamali huyo anasema katika ekari moja zinahitajika jumla ya lita mpaka 200 hadi 300 za mkojo wa sungura na hivyo kuufanya mkojo huo kuwa na thamani kwa mfugaji kutokana na kumuingizia kipato kikubwa kwa mara moja.

Anasema wakulima pia hunufaika na matumizi ya mkojo huo na ndio maana huwa tayari kuununua kwa gharama hiyo kwa lita. Kwa mujibu wa mwanadada huyo, ufugaji wa sungura umewezesha kikundi chake cha wajasiriamali kupata fedha za kutosha kujikopesha na kujiendeleza na miradi mingine ikiwemo kilimo cha mpunga, tumbaku na ufugaji wa nyuki kwa ajili ya asali.

Anasema hali hiyo imetokana na urahisi wa ufugaji wa sungura kwani pamoja na faida ya kuuza na kutumia mkojo wake kama mbolea na dawa ya kuulia wadudu shambani, pia sungura huwapatia faida ya kuwauza kama kitoweo. “Kati ya ufugaji rahisi zaidi kuutekeleza ni ufugaji wa sungura, hauna hasara kama ilivyo kwa kuku, bata, ng’ombe au mifugo mingine ambayo ikishambuliwa na maradhi tu mfugaji anapata hasara kubwa,” anaeleza.

Anasema hakuna hasara katika ufugaji wa sungura zaidi ni changamoto tu unazokutana nazo katika kuwatunza kama mfugaji asipokuwa makini. Anataja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuzidiwa ujanja na sungura ambao huchimba mashimo kwenye banda na kutoroka, ukosefu wa chakula hasa kipindi cha kiangazi na vifo vya wanyama hao endapo mfugaji asipokuwa msafi kwenye banda lao.

“Katika ufugaji wa sungura, usafi wa banda lazima ufanyike kila siku ili kuondoa uchafu kama vyakula vilivyo mwagika na kinyesi kilichoganda,” anaeleza. Kundi hilo la wajasiriamali mkoani Tabora lina jumla ya wanachama 300 kutoka maeneo yote mkoani humo na wanaendesha miradi zaidi ya 18, ukiwemo mradi wa ufugaji sungura.

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi