loader
Picha

Mataifa mengine yaige China

JUZI Rais John Magufuli alifungua maktaba kubwa na ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliyojengwa katika Kampasi ya Mlimani.

Katika uzinduzi huo, Rais aliishukuru China kwa kuipatia Tanzania misaada ambayo haiambatani na masharti.

Alieleza kuwa jambo la kufurahisha ni kwamba misaada ya China, haiambatani na masharti. Wenyewe wakiamua kukupa wanakupa.

Walitujengea Reli ya Tazara na Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kilichopo Dar es Salaam na pia wametusaidia katika maeneo mengine mengi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa maktaba hiyo na chuo cha VETA kitakachojengwa mkoani Kagera.

Anamshukuru Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke na kumuomba apeleke shukrani za Tanzania kwa Rais wa China, Xi Jinping kwa misaada ambayo China imekuwa ikiitoa kwa Tanzania.

Anamhakikishia Balozi Wang kuwa serikali itahakikisha kila msaada unaotolewa, unatumiwa vizuri.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, urafiki wa China na Tanzania ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti, Mao Zedong umeendelea kuleta manufaa makubwa.

Anasisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, itaendeleza na kukuza uhusiano na ushirikiano huo mzuri.

Tunamuunga mkono Rais kwa kuishukuru Serikali ya China kwa misaada mingi na mikubwa ya hali na mali, ambayo imekuwa ikiipatia Tanzania kwa miaka mingi, tangu tulipopata Uhuru hadi sasa.

Ni wazi kuwa misaada hiyo, imewezesha Tanzania kutekeleza miradi mingi ya kiuchumi na kibiashara na kuinua maisha ya wananchi. Pia, misaada hiyo imekuza elimu, sayansi na teknolojia.

Kwa upande wa maktaba hiyo ya kisasa, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, anasema majengo ya maktaba hiyo yenye ghorofa mbili, yamechukua eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 20,000 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, kukalisha watumiaji 2,100 kwa wakati mmoja.

Pia, majengo hayo yana kompyuta 160 zilizounganishwa na mtandao kwa ajili ya kusoma vitabu kwa njia ya kielektroniki, ofisi za wafanyakazi, eneo la wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukumbi wa kisasa wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua watu 600. Tunaungana na Prof.

Anangisye kuishukuru Serikali ya China kwa kutoa msaada wa fedha za ujenzi wa maktaba hiyo kubwa na ya kisasa na kampuni ya ujenzi ya Jiangsu Jiangdu ya China, kwa kujenga majengo hayo yenye ubora na hadhi ya hali ya juu. Tunahimiza mataifa mengine duniani kuiga mfano wa China.

Aidha, tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli kwa mchango mkubwa, uliosaidia kufanikisha ujenzi wa maktaba hiyo.

Tunaitaka jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kutunza vizuri majengo ya maktaba hiyo na kuitumia kwa manufaa ya wanafunzi wa chuo hicho, wanafunzi wa taasisi zingine na wananchi wa kawaida.

HAKUNA ubishi kwamba ili kuimarisha biashara yoyote ile duniani, zikiwemo ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi