loader
Picha

UDZUNGWA: Hifadhi iliyo hatarini kutoweka

TANZANIA ni nchi yenye idadi kubwa ya vivutio vya utalii na vya kipekee. Hivi ni pmaoja na kuwa na eneo lilipogunduliwa fuvu la binadamu wa kale zaidi duniani, huko Oldvai Gorge na hifadhi zenye idadi kubwa ya sokwe za Gombe na Mahale mkoani Kigoma.

Kati ya vivutio vilivyopo Tanzania, baadhi vimetajwa katika yale maajabu saba ya dunia. Vingine ni vya kipekee licha ya kwamba havijulikani sana, ndiyo maana watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani huvutiwa kuzuru Tanzania na kushuhudia utajiri huu wa maliasili ambao Tanzania imetunukiwa.

Katika vivutio hivi, yapo pia maeneo muhimu zaidi ya kihistoria yanayofaa kwa uwekezaji katika sekta ya utalii, maeneo haya siyo tu kwamba hayajulikani vizuri duniani kote, bali ni maeneo yasiyojulikana pia kwa Watanzania wengi.

Hii inatokana na kasumba ya baadhi ya Watanzania kutokuwa na utamaduni mzuri wa kutembelea maeneo haya ya kihistoria na kiutalii ambayo ni mengi tangu makumbusho hadi kwenye miji mikogwe ya Zanzibar na Kilwa Kisiwani. Hata hivyo, maeneo mengine yametambuliwa na kuwekwa kwenye hadhi za kuwa moja ya maeneo muhimu ya urithi wa dunia.

Maeneo haya maarufu kama Oldupai Gorge, Bagamoyo, Kilwa, Zanzibar ni muhimu kwa ukuaji wa utalii nchini Tanzania. Hapa ni muhimu kukumbuka kuwa, kinachoweza kuwa cha kawaida kwako, kinaweza kuwa cha ajabu kwa mwingine, au kinaweza kuwa kitu cha kushangaza na kusisimua kwa mtu mwingine.

Hali hii ndiyo inatufanya wengi wetu kuchukulia vitu na rasilimali tulizo nazo kikawaida, wakati kuna watu (wakiwemo nchi jirani zetu) wanatamani vitu hivi vingekuwa katika ardhi zao. Mfano, Tanzania imebarikiwa kuwa na milima mirefu kuliko yote barani Afrik ukiwamo Mlima Kilimanjaro unafahamika sana duniani.

Watu wengi wanapenda sana kuona mlima huu na kuupanda. Hii ni sehemu yenye mvuto wa kipekee hapa Tanzania. Kuna milima mingine kama Milima ya Usambara, Mlima Meru, Milima ya Rungwe, Milima ya Livingstone, Milima ya Udzungwa n.k. Mandhari nzuri ya milima hii ya kupendeza iliyojipanga na kuinuka juu sana na misitu minene inaifanya nchi yetu kuwa kivutio kikubwa cha mandhari ya kiasili na kivutio kikubwa cha utalii.

Katika makala haya nitajaribu kuangazia moja ya kivutio cha utalii chenye mandhari nzuri ya milima ya kupendeza iliyojipanga na kuinuka juu sana. Hiki ni kivutio kikubwa chenye sifa za kipekee na zisizopotikana sehemu nyingine duniani. Kivutio hiki cha utalii ni Hifadhi ya Milima ya Udzungwa. Milima ya Udzungwa ni hifadhi inayopatikana katika Wilaya ya Kilombero.

Iko umbali wa kilometa 350 Kusini mwa Dar es Salaam, na kilometa 65 kutoka katika Hifadhi ya Mikumi. Sehemu kubwa ipo Iringa Vijijini mkoani Iringa. Hifadhi hii ina ukubwa wa mita za mraba 1,990 ikihusisha Mkoa wa Iringa kwa asilimia 80 na 20 ipo katika Mkoa wa Morogoro.

Mto Sanje ni kivutio kikubwa. Una maporomoko ya maji yenye urefu wa mita zipatazo 170 kwenda juu yakianguka kupitia msituni na kututa mithili ya mianzo ya ukungu bondeni. Hali hii huifanya hifadhi hii kuwa eneo linalofurahisha wakati unapopanda Milima ya Udzungwa.

Ukiwa unaelekea katika mlima huo, utashuhudia mandhari nzuri ya miti mirefu kwa mifupi na uoto wa asili wenye rangi ya kijani kibichi muda wote, ama uwe msimu wa kiangazi, au masika. Jina la hifadhi hii limetokana na milima hiyo ya Udzungwa (yaani nchi ya Wadzungwa, tawi la Wahehe).

Kilele cha juu ni Mlima Luhombero (chenye urefu wa mita 2,579). Hifadhi hii ina hazina ya aina nyingi za mimea, ndege na wanyama ambao hawapatikani katika sehemu nyingine yoyote duniani.

Ni hifadhi pekee iliyo na jumla ya viumbe hai (wasio mimea) aina 70 ikijumuisha vipepeo, mijusi, nyani, mbega, ndege na wengine wengi. Kuna jumla ya aina 400 za vipepeo wakubwa na wadogo na kati yao, aina tatu zinapatikana katika Hifadhi ya Udzungwa tu na hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani. Katikati ya Hifadhi ya Udzungwa, kuna miti mirefu inayofikia mita 30 na huko, utaona ua linalojulikana kama ‘African Violet.’

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa, kati ya aina 11 za jamii ya nyani wanaopatikana katika Hifadhi ya Udzungwa, aina mbili hupatikana katika hifadhi hii pekee ambao ni: mbega mwekundu wa Iringa (Iringa red colobus monkey) na ngolaga (sanje crested mangabey) ambaye alikuwa hajulikani mpaka mwaka 1979.

Uwepo wa ngolaga ni moja ya mambo yanayoifanya Hifadhi ya Udzungwa kuwa ya kipekee duniani na kuwa katika kundi la vivutio muhimu zaidi vya utalii nchini. Kadhalika, kuna aina nyingine nne za ndege ambao hawakufanyiwa uchunguzi, hawa ni: chozi bawa jekundu na jamii mpya iliyogunduliwa ya aina ya kwale wa Udzungwa zinazofanya hifadhi hii kuwa ni moja ya makazi makuu na muhimu ya ndege pori barani Afrika.

Wanyama wengine wanaopatikana ndani ya hifadhi hii ni pamoja na simba, chui, nyati na tembo. Hata hivyo, pamoja na sifa lukuki za hifadhi hii ya Milima ya Udzungwa, bado hifadhi hii haifahamiki vizuri kwa watalii weng.

Hao si tu watalii wa nje, bali pia watalii wa ndani wasio na ufahamu mkubwa wa kivutio hiki chenye upekee duniani. Utafiti mwaka 2010 uliopewa jina la: “Udzungwa Scarp Forest Reserve in Crisis; An Urgent call to protect one of Tanzania’s most important forests” unaonesha kuwa, msitu wa Hifadhi ya Udzungwa unapaswa kuokolewa kwa kuwa uko hatarini kutoweka kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

Kiongozi wa maandalizi ya ripoti ya utafiti huo na mbobezi wa masuala ya ikolojia na wanyama, Dk Francesco Rovero kutoka Makumbusho ya Trento ya Sayansi Asilia nchini Italia, anabainisha kuwa, mwelekeo wa kupungua kwa bioanwai ni mkubwa.

Rovero anasema kuwa mwelekeo wa kufanana wa kupungua kwa bioanwai pia ulibainika kwa swala wadogo wa porini kama funo na idadi ya wanyamapori umekuwa mdogo ukilinganisha na idadi ya wanyama katika misitu, iliyohifadhiwa vizuri.

Naye mbobezi wa masuala ya ikolojia, misitu na wanyama pori na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Amani Kitegile aliyekuwa mmoja wa waandaaji wa ripoti hiyo, amebainisha uwindaji wa nyama pori na uharibifu wa misitu ni tatizo kubwa, na ndiyo moja ya mambo yanayosababisha kupungua kwa bioanwai.

Rovero na Kitegile pia walishiriki katika utafiti mwingine kuhusu Hifadhi ya Udzungwa za: “The newly- established Udzungwa Ecological Monitoring Centre in The Udzungwa Mountains” wa mwaka 2007, na “Hunting or habitat degradation? Decline of primate populations in southern Udzungwa Mountains, Tanzania: an analysis of threats. Biological Conservation” ya Mwaka 2012.

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi