loader
Picha

Uzalishaji asali unavyotumika kubadilisha maisha ya Wahadzabe

WAHADZABE ambao wengi wanaishi katika Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi porini na kuendelea na mila zao za tangu na tangu.

Kutokana na kutojishughulisha na shughuli zingine za uzalishaji mali kama vile kulima au kufuga, chakula kikuu cha Wahadzabe kimeendelea kuwa mizizi na nyama, hususani nyama ya nyani.

Utamaduni wao huo sambamba na uongeaji pamoja na uchezaji wa ngoma zao vimekuwa pia ni sehemu ya kivutio kwa watalii. Mazingira hayo yamewafanya Wahadzabe kwa muda mrefu kuishi kwa kuhamahama ili kujitafutia mahitaji yao ya chakula na maji. Mbali na kukosa ustawi kama jamii, hamahama hiyo imekuwa ikihatarisha maisha yao kwa kuwa kuna wakati wanahama kwenda kutafuta chakula na kukumbana na upinzani kutoka kwa jamii za wakulima na wafugaji. Hamahama hiyo pia imekuwa ikisababisha hali ya watoto wao kushindwa kusoma.

NCA YAJITOSA KUWASAIDIA Pamoja na serikali kujaribu kufanya mambo kadhaa ili kuileta jamii hiyo pamoja, bado Wahadzabe wengi wamebaki porini, hali ambayo imevutia wadau wengine kuangalia namna ya kushirikiana na serikali katika kuisaidia hii jamii.

Wadau wanaojitokeza wanalenga kusaidia jamii hii ya Wahadzabe katika kubadilisha mfumo wao wa maisha yao ili wasiendelee kutegemea kinachopatikana kwenye mazingira (mizizi na wanyama) bali kujihusisha na uzalishaji mali utakaosaidia kuwapa ustawi mzuri zaidi. Shirika la Misaada la Makanisa ya Norway (NCA) ni moja ya wadau waliojitosa katika kusaidia kuboresha maisha ya Wahadzabe.

Shirika hilo limewaanzishia Wahadzabe mradi wa kufuga nyuki kisasa ili waweze kuvuna asali, hatua ambayo itawasaidia kupata kipato katika jitihada za kubadilisha maisha yao. Akiwa ameandamana na maofisa wa NCA, mwandishi wa makala haya alishuhudia mizinga zaidi ya 100 ya kisasa ambayo ilitolewa na shirika hilo ikiendelea kuwanufaisha wananchi hao.

Mizinga hiyo, ikiwa imefungwa juu ya miti ilielezwa kwamba tayari ilikuwa na makundi ya nyuki yakiendelea kuzalisha asali na sasa ina miaka zaidi ya mitano tangu ifungwe na kuanza kuzalisha asali. KUBADILISHA MAISHA Akizungumzia namna nyuki walivyobadilishia maisha yao, mwezeshaji anayesimamia shughuli za kabila hilo ambaye pia ni mwakilishi wa Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) kinachofadhiliwa na NCA, Jacob Lubumba anasema kwa sasa asali ni moja kati ya shughuli kuu zinazowapatia kipato wananchi hao.

Lubumba ambaye pia ni Mhadzabe anasema kwamba, tangu mwaka 1995 walipofika kwenye eneo hilo akiwa mdogo, wamekuwa wakijihusisha na uwindaji ambao ndio ilikuwa njia kuu ya kujipatia chakula. “Wanyama ambao tumekuwa tukiwawinda zaidi na kuwala ni nyani,” anasema na kuongeza kwamba hali hiyo imekuwa pia ikisababisha idadi kubwa ya watoto wa Kihadzabe washindwe kusomeshwa na wazazi wao.

Anabainisha kwamba mwaka 2012 NCA iliwafikia na kuanza kuwapatia njia nyingine mbadala za maisha, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kuanzisha mradi huo wa nyuki ambao umesaidia kuwaondoa kwenye utegemezi wa uwindaji na sasa asali inawaingizia kipato.

Anaweka wazi kuwa, kulikuwa na changamoto za kuyakubali mabadiliko hayo, lakini kwa sasa wanavutiwa na maisha mapya, kwani ufugaji nyuki si shughuli inayowafanya muda mwingi wawe wanahudumia mizinga lakini kile wanachovuna kimechangia katika kubadilisha maisha yao. Akizungumzia namna walivyopokea mafunzo ya kufuga nyuki na kuvuna asali, anasema walikusanywa vijana zaidi ya 10 na kupewa mafunzo kwa siku kadhaa kuhusu ufugaji wa kisasa wa nyuki.

Anasema mafunzo hayo yaliambatana pia na namna ya kurina asali, ikiwa ni pamoja na mbinu mbadala za kutumia wakati wa kupakua asali hiyo. Anasema mbali na NCA kuwapa mizinga na ujuzi, lakini pia iliwawezesha kwa kuwapatia vifaa maalumu kwa ajili ya kupakua asali. “Lakini sio kwamba shughuli nyingine za uwindaji zimesimama moja kwa moja, hapana ila tumetakiwa kubadili maisha na kujikita katika uzalishaji zaidi,” anasema.

Anasema wanapovuna hutengeneza zaidi ya Sh milioni nane. Anafafanua kwamba wanauza ndoo kuanzia 80 hadi 100 zenye ujazo wa lita 20. Anasema inapokuwa ni asali nzito, ndoo moja wanaiuza kwa Sh 60,000 huku ile nyepesi wakiiuzwa hadi Sh 80,000.

Anasema, tangu mwaka 2012, wamekuwa pia wakifanya shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule ya awali na nyumba za mtoa huduma za afya. Anasema, uwepo wa shule hiyo ya awali umesaidia kusomesha watoto wa jamii hiyo ya wawindaji na wengi wanapata msingi wa kujiunga na elimu za msingi na hatimaye elimu ya sekondari.

“Tunashukuru kwamba tumejenga shule ya awali na kumwajiri mwalimu na pia tumejenga nyumba ya mtoa huduma za afya kwenye zahanati yetu ya kijiji,” anasema. Anasema wamefungua pia benki za vijijini (vicoba) na hivyo wanatumia pesa wanazopata kwenye asali kwa kukopeshana pia. Akizungumza huku akionesha nyumba aliyojengewa na wanakijiji, Farida Suleiman ambaye ni tabibu katika zahanati ya kijiji anasema mwaka huu amezalisha watoto nane wa Kihadzabe.

Anasema kwa muda aliokaa kwenye jamii hiyo amekuwa akijitahidi kutoa huduma bora ya afya huku akiainisha changamoto kadhaa zinazomkabili kuwa ni pamoja na ukosefu wa msaidizi wa kutoa huduma. Anasema changamoto nyingine anasema ni upungufu wa dawa na kukosekana kwa baadhi ya miundombinu wezeshi kama vile umeme.

Mratibu wa Mafunzo wa 4CCP, Juma Godliving anasema, amekuwa karibu zaidi na kabila hilo katika kusimamia mafunzo mbalimbali yakiwemo ya ujasiriamali. Anafafanua kwamba wanatoa mafunzo katika mfumo shirikishi zaidi na sio kwa mfumo wa kuwaelekeza tu na kuwaacha. “Tunatumia wataalamu waliopo kwenye kabila hili ili kuwafundisha wenzao mbinu mbalimbali za kujiendeleza katika ujasiriamali ikiwemo biashara ya asali,” anasema na kuongeza kwamba wanawasaidia pia kupata masoko.

Anasema wamewawezesha pia wananchi hao kutumia fedha wanazopata kwa kuuza asali viziri ikiwa ni pamoja na kuzitunza kwenye vikoba. Mkuu wa Mkoa wa Singida wa zamani, Parseko Kone, anakumbukwa pia kwa jinsi alivyohamasisha wadau wa maendeleo kusaidia kwa hali na mali maendeleo ya kabila hilo.

Katika kijiji cha Munguli wilaya ya Mkalama mkoani humo, kuna mabweni ambayo yalijengwa kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi wanaotokea kwenye vijiji linapoishi kabila hilo. Pia katika shule hiyo kuna darasa moja na ofisi ya walimu iliyojengwa na NCA.

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi