loader
Picha

Matumizi sahihi ya ndiyo/ ndiye na yoyote/yeyote

MAKALA haya yataangalia matumizi ya maneno ndiyo/ndiye na yoyote/yeyote, jinsi yanavyotumiwa na watumiaji wa Lugha ya Kiswahili.

Usahihi wa matumizi ya maneno haya, umekuwa ukielezwa na kufafanuliwa mara kwa mara na wataalamu wa Kiswahili lakini inaonekana watumiaji wa lugha hiyo bado wanaendelea kufanya makosa wanapotumia maneno haya.

Haya ni maneno ambayo kimaumbo yanafanana na hata kimatamshi pia yanakaribiana sana. Hivyo, watumiaji wengi hudhani yanaweza kutumiwa kwa vyovyote vile.

Ama unaweza kutumia neno moja katika nafasi ya neno lingine.

La hasha! Maneno haya yana matumizi tofauti kabisa ingawa kidogo yanafanana kimaumbo na kimatamshi na yana sifa moja kisarufi yote ni viwakilishi. Ndiyo/ ndiye viwakilishi na yeyote/ yoyote navyo ni viwakilishi.

Wazungumzaji wengi wa Kiswahili huchanganya matumizi ya maneno haya.

Wapo wanaotumia neno ndiyo mahali pa ndiye na ndiye mahali pa ndiyo.

Mahali pa yoyote wanatumia yeyote. Uchanganyaji huu huenda unatokana na watu kuchanganya hivyo kwa mazoea tu au pengine kwa kutokujua matumizi ya maneno haya kisarufi.

Wakati mwingine unaweza kusikia mtu anasema “huyu kijana ndiyo alimpiga huyu mtoto” Au utasikia mtu akisema, niitie mtu yoyote aje hapa au niitie pikipiki yeyote.

Sentensi zote hizi zina makosa kama ambavyo tumekwisha eleza hapo juu.

Maneno haya yametumika kimakosa. Msingi wa makosa haya ni wakutokujua vizuri sarufi ya Kiswahili na hasa upatanisho wa kisarufi na mkanganyiko unaowapata wazungumzaji katika kupambanua ni wakati gani neno fulani litumike mahali fulani.

Ndiyo, hutumika unapozungumuzia vitu visivyo na uhai kama vile nyumba, silaha, zana, ngalawa, taa, chupa, n.k.

Kwa mfano, mtu anaposema fulani ndiyo aliyepanga nyumba hii, ni kwamba ukisema hivyo, umemuondoa mtu huyo kwenye kundi la vitu vyenye uhai na kumweka kwenye kundi la vitu visivyo na uhai. Kwa hiyo, ndiyo hutumika katika vitu visivyo na uhai na ndiye hutumika katika vitu vyenye uhai.

Halikadhalika yoyote hutumika katika vitu visivyo na uhai na yeyote hutumika katika vitu vyenye uhai. Kwa mfano, katika sentensi tulizotaja hapo juu.

Sentensi ya kwanza inasema, - “Huyu kijana ndiyo, aliyempiga yule mtoto” Usahihi wa sentensi hii ni kwamba mtu huyu alitakiwa kusema:

“Huyu kijana ndiye aliyempiga yule mtoto” “Niitie pikipiki yoyote niondoke” Sentensi hii ni sahihi lakini kama mtu atasema, “mvua kubwa ndiye iliyosababisha mafuriko”.

Hapa atakuwa amefanya makosa kwa kuwa amechanganya kiwakilishi hiki pamoja na jina la kitu kisichokuwa na uhai. Hivyo, alitakiwa kusema, “mvua kubwa ndiyo iliyosababisha mafuriko”.

Huyu ndiye Mbunge wetu. Mwalimu Nyerere ndiye aliyetuletea uhuru. Jamal ndiye alikuwa mwanafunzi bora katika somo la Kiswahili.

Sentensi zote hizo ni sahihi: Huu ndiyo muhuri uliotumika kama uthibitisho.

Mlango huu ndiyo uliotumiwa na wezi kuingia ndani. Ukuta huu ndiyo kinga pekee ya maji kutoka mtoni. Hizi nazo ni sentensi sahihi kwa kuzingatia matumizi ya neno ndiyo. Sentensi hizi haziwezi kutumika katika kinyume chake.

Yaani huwezi kutumia ndiyo mahali pa ndiye na ndiye mahali pa ndiyo.

Kama tulivyokwisha eleza hapo mwanzo, utaona ndiye imetumika sambamba na vitu vyenye uhai na ndiyo imetumika sambamba na vitu visivyo na uhai katika mifano hii. Sasa tuangalie matumizi ya maneno yoyote na yeyote.

Watumiaji wengi wa maneno haya wamekuwa na mazoea ya kuchanganya na kusema mtu yoyote badala ya yeyote.

Matumizi ya neno yoyote yamechukua nafasi kubwa zaidi kuliko matumizi ya neno yeyote.

Ongezeko hili linakatisha tamaa hasa kwa wale ambao kila uchao hutoa au hufanya usahihi wa matumizi haya mabovu ya maneno haya lakini bado makosa hayo yanaonekana yakirudiwa na watumiaji wa lugha ya Kiswahili.

Msingi wa matumizi sahihi ya maneno hayo ni kama tulivyofafanua hapo juu. Neno yoyote hutumika kwa vitu visivyo na uhai wakati yeyote hutumika kwa viumbe vyenye uhai tu na hasa kwa binadamu,wanyama na wadudu.

Matumizi sahihi ya maneno haya hujipambanua zaidi katika upatanisho wa kisarufi yaani ni nomino au jina gani limeambatana na maneno haya.

Hivyo, unapotaka kutumia mojawapo ya maneno haya, angalia kwanza kitu unachozungumzia, Je, kina uhai au hakina uhai? Kipo katika kundi gani la wanyama au mimea.

Ukishajua hilo, ndipo unaweza sasa kubaini utumie neno gani kati ya hayo mawili. Kwa mfano.

Neno yeyote ambalo hutumika sambamba na majina ya viumbe hai linaweza kutumika hivi: Chagua kuku yeyote hapo bandani, tumchinje.

Mtu yeyote anaweza kuja kutusaidia. Kiongozi yeyote atatufaa ili mradi awe Mtanzania. Kondoo yeyote huwa na mafuta. Samaki yeyote huishi kwenye maji. Anatafuta mdudu yeyote ili aweze kufundishia darasani .

Sentensi zote hizi ni sahihi. Neno yeyote limetumika vizuri na kwa usahihi. Hivyo si sahihi kusema kuku yoyote, mtu yoyote, kiongozi yoyote, kondoo yoyote nk. Ni makosa.

Kama tulivyoeleza hapo juu, neno yoyote hutumika sambamba na majina ya vitu visivyo na uhai. Kwa mfano: Nitafutie kalamu yoyote niweze kuandika.

Nitafutie shule yoyote nikamwandikishe mwanangu. Amesema ataishi nchi yoyote atakayopelekwa. Mbuzi wangu anaweza kula majani yoyote.

Mimi nitakula mboga yoyote ile. Kwa matumizi haya, sentensi zote hizi ni sahihi, zimetumia neno yoyote katika mahali sahihi na upatanisho wa kisarufi umezingatiwa.

Nafasi ya yoyote katika sentensi hizi haiwezi kuchukuliwa na yeyote. Ikiwa hivyo basi sentensi hiyo itakuwa si sahihi.

Ingawa katika makala hii tumesema matumizi ya maneno haya yanategemeana na uhai au kukosekana kwa uhai wa kitu na tukabaini zaidi katika uhai wa wanyama na wadudu, hasa kwa matumizi ya maneno yeyote na yoyote ambayo ndio yamekuwa yakisumbua zaidi wazungumzaji wa Kiswahili.

Mimea pia ni viumbe hai lakini katika matumizi sambamba na majina yake si lazima yaambatane na kiwakilishi yeyote.

Kiupatanisho wa kisarufi majina ya viumbe hivi havitegemei matumizi ya yeyote, nayo huweza kubeba kiwakilishi kingine kulingana na upatanisho wake wa kisarufi. Kwa mfano.

Nipatie tunda lolote nile. Kata mti wowote tujengee. Changua chungwa lolote nipatie. Chuma jani lolote, umpe atafune.

Pasua nazi yoyote nione kama imekomaa. Haya ni majina ya viumbe hai, mimea ambayo haitumii yeyote au yoyote, hasa kutokana na kauli yetu kuwa yeyote hutumika sambamba na majina ya viumbe hai hasa wanyama na wadudu na si mimea.

Vipo pia, viumbe visivyo hai mbavyo navyo hughairi matumizi ya yoyote katika kundi la vitu visivyo na uhai. Gari lolote litanisaidia. Kisu chochote kitanifaa Kitabu chochote cha Shaaban Robert ni hazina ya maarifa.

Pamoja na ziada hiyo ya maarifa ambayo nadhani si mbovu, lengo la makala haya ilikuwa ni kuweka bayana matumizi ya maneno ndiyo/ndiye na yoyote/yeyote.

Maneno haya yamekuwa yakitumiwa vibaya kuliko aina nyingine ya viwakilishi hivi katika jamii hii ya maneno.

Maneno haya yamekuwa yakichanganywa na kuendelea kuharibu ufasaha wa lugha kwa wasikilizaji na wazungumzaji. Makala haya yanaweza kuwa msaada wa kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la matumizi mabovu ya maneno haya.

Bila shaka wale wote watakaosoma makala haya, watanufaika na kuendelea kutumia vizuri maneno haya na hivyo kuboresha na kuendeleza Kiswahili.

0713340959

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Ambrose Mghanga

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi