loader
Picha

Nafasi ya Tabora historia ya Tanzania

UNAPOZUNGUMZIA historia ya Tanzania tangu ilipokuwa Tanganyika, harakati za ukombozi, masuala ya utawala wa kikoloni pamoja na biashara ya watumwa, kamwe huwezi kuuruka mkoa wa Tabora.

Mkoa huo unabeba sehemu kubwa ya historia ya Tanzania kutokana na kuwa eneo muhimu la harakati za ukombozi, lakini pia ni eneo ambalo mwasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisomea na kufanyia kazi.

Tabora ni mkoa uliopo upande wa magharibi mwa Tanzania, ukielezwa kuwa ndio mkoa mkubwa kuliko mwingine wowote nchini.

Ni mkoa unaoungwa na wilaya zenye historia na vivutio vya utalii kama Sikonge, Uyui, Urambo, Nzega, Kaliua, Igunga na Manispaa ya Tabora.

Wanyamwezi ndio wenyeji wa asili wa mkoa wa Tabora pamoja na Wasukuma, Waha na makabila mengine yanayopakana au kuhamia katika mkoa huo.

Kwa mujibu wa Mtemi wa Wanyanyembe, Msagata Fundikira, historia ya Tabora inaanzia miaka ya 1800, enzi za utawala wa kichifu na biashara ya watumwa.

Anasema wakati Waarabu wanafika katika mji wa Tabora miaka ya 1830 walikuta mji huo umeendelea hasa katika maeneo ya Kwihala na Itetemya. Na hii ni kwa sababu maeneo hayo yalikuwa yana idadi kubwa ya watu.

Anasema mji wa kwanza kabisa kuanzishwa katika mkoa huo na kukua kwa kasi hadi kuizaa Tabora ni mji wa Itetemya ambao ulikuwa chini ya utawala wa Watemi wa Kinyanyembe, miaka 1800.

“Hadi Waarabu wanakuja kwa ajili ya biashara yao ya utumwa, walikuta Itetemya ikiongozwa na mtemi wa Wanyanyembe na ikabidi waunge urafiki ili kuweza kufanya biashara yao hiyo,” anaeleza Msagata.

Anasema eneo maarufu la sasa ambalo ni kituo cha Malikale la Livingstone, lilitolewa na Mtemi wa Wanyanyembe kwa mwarabu aliyekuwa akifanya biashara ya utumwa, Said Mohammed.

Anasema tangu eneo hilo litolewe kwa Mwarabu huyo pamoja na kwamba shughuli za kitemi zilikuwa zikiendelea, lakini pia biashara ya utumwa ilishamiri kiasi cha kuifanya Tabora kuwa kituo kikuu cha njia ya watumwa.

Hilo linathibitishwa zaidi na Mhifadhi katika kituo cha Malikale cha Livingstone Tabora, Mbaruku Salehe ambaye anaeleza kuwa eneo hilo alilopewa mwarabu huyo, Mohammed, kwa ajili ya watumwa lilijengwa nyumba ya tembe kwa ajili ya watumwa hao.

Anasema jengo hilo lililojengwa kwa mtindo wa nyumba za kale kama zilivyo Bagamoyo na Zanzibar, liliwekewa nakshi (hadi leo zipo), zikiwa na maana mbalimbali mojawapo ikiwa mmiliki wake (mwarabu) ameoa lakini hakuwa akiishi na mke wake kwenye jengo hilo.

Jengo hilo lina vyumba kadhaa, kikiwemo chumba cha watumwa waliokuwa wakisafirishwa kutoka nchi mbalimbali za Uganda, Rwanda na kupitia Tabora, Bagamoyo na baadaye Zanzibar ambako waliuzwa na husafirishwa na majahazi hadi Ulaya.

Hata hivyo, anasema biashara hiyo ya watumwa ilipata upinzani baada ya ujio wa wamishenari miaka ya 1870, Dk David Livingstone, aliyekuja kwa shughuli za kidini lakini pia utafiti.

“Livingstone alipofika alifikia kwenye jengo la huyu Mwarabu, Mohammed, la tembe na kwa kweli hakupendezwa na biashara ya utumwa na aliipinga waziwazi. Aliishi kwenye jengo hilo kwa muda,” anasema.

Anasema katika miaka ya 1890 Wajerumani walianza kufika na baada ya kushinda Wanyamwezi walifanya Tabora kuwa kitovu chao katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ya kati; mji ukawa kituo cha kikosi cha jeshi na pia kikosi cha polisi.

“Hadi leo hii jengo la ngome ya Wajerumani ambako ndiko ilikuwa makao makuu ya kwanza ya nchi lipo mjini Tabora, jirani na ofisi za mkuu wa mkoa na Halmashauri ya manispaa ya Tabora,” anaeleza.

Anasema kitendo cha Wajuremani kuingia nchini hakikuishia kupambana na serikali za kichifu zilizokuwepo pekee, bali walipambana na biashara ya watumwa ambao kwa kipindi hicho, ilikuwa ikimaliza nguvukazi ambayo Wajerumani waliihitaji kwa ajili ya uzalishaji kupitia mashamba.

Akielezea historia ya Tabora na mchango wake katika taifa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri anasema Tabora ni moja ya mikoa iliyobarikiwa kuwa na historia isiyofutika nchini.

“Hapa ndipo Mwalimu Nyerere alikosomea katika shule ya wamisionari Wakatoliki na baada ya kumaliza masomo yake ya ualimu aliyosomea Makerere, Kampala, Uganda, alirejea hapa Tabora na kufundisha shule ya St Mary's ambayo sasa inajulikana kama Milambo Sekondari,” anasema Mwanri.

Anasema pamoja na hayo, Tabora pia inabeba historia ya harakati za ukombozi ambapo historia ya Chama cha TANU haiwezi kuzungumziwa bila kuutaja mkoa huo.

“Hata zile nyimbo zilizokuwa maarufu za ‘Ooh TANU yajenga nchi’, zilitungwa hapa hapa Tabora na warugaruga na kutafsiriwa,” anasisitiza mkuu huyo wa mkoa na kwamba maeneo ya awali yalikuwa kwa lugha ya Kinyamwezi ‘Ooh Sasi jabela mitwe’ maana yake ikiwa ‘Risasi zimevunja vichwa’.

Kihistoria mkutano mkuu wa TANU ulifanyika Tabora mwaka wa 1958 kuanzia Januari 21 na miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na chama hicho ama kishiriki katika uchaguzi chini ya masharti ya kibaguzi yaliyowekwa au isusie uchaguzi.

Mkutano huo wa Tabora ulitishia kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa.

Katika mkutano huo, chama hicho cha TANU kilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama hicho kama isingekuwa busara za Mwalimu Nyerere na viongozi wanzake wa kipindi hicho.

Baada ya kupatikana kwa ufumbuzi wa mgogoro huo kwa TANU kukubali kushiriki uchaguzi kupita kura tatu zilizopigwa, siku iliyofuata wakati wa mkutano bado ukiendelea Mtemvu alituma simu ya maandishi kwa rais wa TANU, Mwalimu Nyerere kupitia ofisi ya TANU Tabora, akitangaza kujiuzulu kwake kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama chake cha upinzani - African National Congress (ANC).

Hata hivyo kwa mujibu wa historia, inayoizungumzia Tabora, kabla ya kuondoka Tabora Mwalimu Nyerere alifanya mkutano wa hadhara soko kuu la Tabora na kuelezea maamuzi ya mkutano mkuu.

Katika hotuba hiyo ya Mwalimu Nyerere ilijaa hisia kali. Aliwaambia wasikilizaji wake kuwa endapo Waingereza watakaidi kutoa uhuru basi wananchi wataelekeza kilio chao kwa Mwenyezi Mungu.

Mwalimu Nyerere alipotamka maneno haya hakuweza kujizuia, akaangua kilio na vilio vya wananchi waliouelewa uchungu wa dhuluma vikatanda uwanja mzima.

Baada ya hotuba hiyo iliyowaliza watu, wananchi wengi ambao walisita kujiunga na TANU sasa waliingia kwa wingi.

Na hadi leo pale Tabora Mjini eneo la sokoni umejengwa mnara unaomwonyesha Mwalimu Nyerere akizungumza na wananchi huku akiwa na huzuni kubwa.

Mnara huo ni kumbukumbu tosha juu ya harakati za ukombozi zilizofanyika Tabora chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Pamoja na hayo, Mwanri anabainisha kuwa historia ya Tabora kuibeba Tanzania haikuishia hapo kwani hadi leo, wilayani Sikonge kuna kaburi la mchungaji wa kwanza wa Kinyamwezi wa Kanisa la Moravian.

“Na pia utapata kuona Kanisa la pili la Moravian lililojengwa miaka ya 1897 na linatumika mpaka leo,” anasisitiza.

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi