loader
Picha

Sababu za mwanaume kuwa na matiti

Wataalamu wanasema, kwa kawaida matiti ya mwanamke huwa makubwa kuliko yale ya mwanaume kwa sababu za kibaiolojia.

Ukuaji wa matiti kwa mwanamke unaletwa na homoni za kike ambazo ni nyingi kuliko kwa mwanaume.

Ukuaji wa matiti ni dalili ya mwanzo ya kubalehe mtoto wa kike.

Kawaida kukua kwa matiti husababishwa na homoni za kike wakati za kiume huzuia ukuaji wa matiti hivyo ni lazima kuwe na uwiano sahihi kwa upande wa mwanamke (kuwa na homoni za kike nyingi na za kiume kidogo) na kwa mwanaume (kuwa na homoni za kiume nyingi na za kike chache) ili matiti yakue zaidi kwa mwanamke na yasikue kwa mwanaume.

Uwiano huu unapopata hitilafu upande wa mwanaume, matiti yanaweza kukua. Kwa mtu wa jinsia ya kiume matiti kuwa makubwa yanaleta mfadhaiko na athari kisaikolojia hivyo ni vizuri kuonana na wataalamu wa afya ili kupata maelezo sahihi na kutafuta chanzo na tiba yake.

Matiti yanaweza kuwa makubwa kidogo kuzunguka chuchu au kuwa makubwa kiasi cha kuchukua sura ya matiti ya mwanamke; inaweza kutokea kwenye titi moja au yote mawili; na yanaweza kuambatana na maumivu au bila maumivu.

Kukua kwa matiti kwa mwanaume kunaweza kukawa kwa sababu ya mabadiliko ya homoni ya mwilini au inaweza kuletwa na magonjwa husika.

Kuna vipindi vitatu vya ukuaji ambavyo hutokea mabadiliko ya homoni kwa mtu yanayosababisha ukuaji wa matiti kwa watu wa jinsia ya kiume.

Cha kwanza ni wakati mtoto akiwa mchanga, cha pili ni wakati ya kubalehe na cha tatu ni uzeeni.

Mtoto anapozaliwa anakuwa na homoni za mama nyingi na kuna wakati husababisha matiti ya mtoto kuwa makubwa kiasi.

Hali hii huwa inapotea baada ya wiki chache. Kipindi cha kubalehe matiti yanaweza kukua kutokana na kuchelewa kuongezeka kwa homoni za kiume hali ambayo inatakiwa kutokea katika kipindi hicho.

Hii ni sababu mojawapo kubwa ya tatizo la matiti kukua kwa mwanaume na hali hii hupotea katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili. Wakati wa uzeeni homoni za kiume hupungua kiwango na hivyo inaweza kusababisha matiti kukua.

Sababu nyingine za kukua kwa matiti kwa mwanaume ni dawa za kutibu baadhi ya magonjwa ikiwemo baadhi ya dawa za kulevya, kunywa pombe kupita kiasi, magonjwa kama figo na ini, magonjwa ya kurithi yanayoathiri korodani, na uvimbe unaotoa homoni za kike kwa wingi.

Pia unene kupita kiasi unasababisha kukua kwa matiti kwa sababu ya kupungua kwa homoni za kiume.

Sababu nyingine ni saratani ya matiti, ambayo ingawa haitokei kwa wingi kwa wanaume, mara nyingi hugundulika kwa kuchelewa na hivyo kuwa na matokeo mabaya kwa mgonjwa.

Athari kubwa ya tatizo la kukua kwa matiti kwa mwanaume ni la jamii na kisaikolojia, lakini hakuna madhara makubwa kiafya, isipokuwa kwa wachache wenye saratani.

Hivyo, matibabu ya tatizo yatategemeana na kipindi cha ukuaji wa mtu ambapo tatizo limetokea na kama kuna sababu maalumu kwa (mfano uvimbe) ambao umesababisha mabadiliko ya homoni.

Wataalamu wa afya watashauri njia inayofaa, kwa mfano kusubiri kwa mwaka mmoja au miwili kwa wale ambao wako kwenye umri wa kubalehe au kupunguza uzito kwa wale wenye uzito mkubwa.

Baadhi ya dawa zinatumika kupunguza maumivu yanayoambatana na ukuaji wa matiti kwa ghafla hasa kwa wanaotumia dawa zinazofanya matiti ya mtu yakue.

Endapo matiti yamekuwa makubwa kiasi cha kubadilisha mwonekano, wataalamu wa upasuaji maalumu watafanya upasuaji kwa ajili ya kupunguza ukubwa wa matiti.

Faraja Chiwanga ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba na Mbobezi wa magonjwa ya Homoni. Simu: 0786587900.

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Dk Faraja Chiwanga

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi