loader
Picha

Tuchukue tahadhari joto kali

MAMLAKA ya Hali ya HewaTanzania (TMA) imeonya kuhusu joto kuongezeka juu ya wastani hadi kufikia nyuzi joto 34 hadi Januari, 2019 kutokana na jua la utosi na mvua hafifu za vuli.

TMA imesema wastani wa joto kwa Novemba na Desemba ni nyuzi joto 31.5 mikoa ya Dar es Salaam,Tanga na visiwa ya Unguja na Pemba huku kukiwepo uwezekano wa kufikia nyuzi 35.

Tunaipongeza TMA kwa tahadhari hiyo kwa wananchi na hasa wa mikoa inayoathirika na hali hiyo na kuwataka wachukue tahadhari ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea kwao.

Imekuwa ni kawaida kwa TMA kutahadharisha jamii kuhusu kuwepo kwa mvua kubwa na au maafa yake na yatokanayo na upepo, kimbunga na hivyo kwa wengine hii inaweza isiwe tishio.

Ni kwa kutambua ukweli huu tunaungana na TMA kuwatahadharisha raia wote, wananchi na wageni kutoka nje ya nchi, kuchukua tahadhari ya kutembea maeneo yenye kivuli chochote na kunywa maji mengi ya kutosha kuhimili joto.

Kwa wanaofuatilia matangazo ya runinga na vyombo vingine vya habari kama magazeti na redio watakumbuka yaliyowakuta wananchi nje. Wengine hasa nchi zenye joto, baridi kali, mvua kubwa au kimbunga wamekuwa wakipewa onyo la kuchukua tahadhari kulingana na janga lijalo.

Ni matarajio yetu kuwa, onyo la TMA nchini kwetu litapewa uzito na wananchi kuepusha maafa makubwa yanayoweza kuikuta jamii.

Ongezeko lolote la joto bila kujali kiasi chake ni tishio kwa maisha ya binadamu, wanyama na pia mimea hivyo kutakiwa kuchukua tahadhari. Tunaomba kila mmoja achukulie onyo la TMA kwa tahadhari akijua mchelea mwana kulia, hulia yeye. Ni vyema kila mmoja akajihadhari.

Kwamba safari hii joto litasumbua si jambo geni. Mara nyingi TMA inatoa tu tahadhari ya majanga yanayohusu mvua kubwa au upepo mkali unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Tahadhari kama hii imesaidia kupunguza maafa kama si kuyamaliza katika maeneo mengine na hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kujihami. Tujihami kwa kutembea na miavuli, sehemu zenye vivuli vya miti au majengo marefu ili kupunguza adha ya kuchomwa na miali ya jua.

Pia tunywe maji mengi kudhibiti upoteaji wa maji mwilini kulingana na kazi na maeneo ya kufanyia kazi, viwandani, shamba au michezoni. Lakini zaidi, tuwe wasamaria wema kwa ndugu zetu wenye ualbino kwa kuwasaidia ili joto hilo lisiwaathiri zaidi.

Mbali ya tahadhari hiyo, joto hili linapaswa liwe fundisho la wananchi kuchukua hatua za dhati za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi sasa. Na njia nzuri ya kufanya hivyo ni kupanda miti na kutunza na kuhifadhi mazingira ili yatutunze.

Shime tukabili mabadiliko hayo kwa kupunguza athari zitokanazo na joto hili.

TANZANIA imekabidhiwa rasmi uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi