loader
Picha

Mahakama ya Tanzania na maboresho utoaji huduma

KATIKA kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa kuboresha utoaji haki nchini.

Kipindi hiki kimeshuhudia maboresho makubwa yakifanyika kwenye maeneo mbalimbali yanayolenga kuboresha utoaji huduma. Ujenzi wa majengo ya mahakama Katika kuhakikisha inatekeleza azma yake ya kuboresha na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, Mahakama ya Tanzania katika kipindi hicho imeendelea na ujenzi wa majengo mapya na hadi kufikia Juni mwaka 2019 jumla ya majengo 52 ya mahakama yatakuwa yamekamilika kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo yale ya mahakama za mwanzo, wilaya, mahakama za hakimu mkazi na mahakama kuu.

Majengo yanayoendelea kujengwa ni pamoja na Mahakama za Mwanzo 22, Mahakama za Wilaya 20, Mahakama za Mikoa (Hakimu Mkazi) 8 na Mahakama kuu 2, zinazojengwa katika mikoa ya Mara na Kigoma. Baadhi ya majengo yamekamilika na mengine yako katika hatua za mwisho za ukamilishwaji huku mengine yakiwa katika hatua za awali kabisa za ujenzi.

Majengo yaliyokamilika ni yale yaliyokuwa kwenye mpango wa ujenzi katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017. Majengo hayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkuranga, Kigamboni, Mahakama ya Mwanzo Kawe pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Ilala lililopo eneo la Kinyerezi ambapo ujenzi wake uko hatua za mwisho.

 

Mahakama ya Tanzania katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 ilikamilisha mradi wa ujenzi wa majengo 12 ambayo ujenzi wake ulisimama katika miaka ya nyuma. Miradi hiyo ni ile inayojumuisha mahakama za hakimu mkazi, mahakama za wilaya na mahakama za mwanzo zilizopo katika maeneo ya Manyara (Mahakama ya Hakimu Mkazi), pamoja na Mahakama za Mwanzo za Iguguno (Singida), Wasso (Loliondo), Old Korogwe na Magoma (Korogwe).

Miradi mingine iliyokamilishwa ni ile ya Mahakama za Mwanzo za Karatu, Robanda (Serengeti), Itinje (Meatu) na Totoe (Songwe). Aidha, Mahakama ya Tanzania pia ilikamilisha miradi ya ukarabati mkubwa wa majengo yake ya Mahakama Kuu ya Tanzania yaliyopo Mbeya, Mwanza na Dodoma.

Katika kutekeleza Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020) wenye nguzo tatu muhimu ambazo ni Utawala Bora na Matumizi ya Rasilimali, Upatikanaji wa Haki kwa wakati na Kuimarisha Imani ya wananchi kwa Mahakama, na Ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama, Mahakama imeendelea kusogeza huduma kwa wananchi na kuhakikisha wanapata haki kwa wakati.

Katika mwaka 2016/2017, iliandaa mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo yake ambapo kupitia mpango huo ilikamilisha miradi yote iliyokwama kuanzia miaka ya nyuma hadi mwaka 2013. Mahakama ya Tanzania katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 ilipanga kujenga majengo ya mahakama za mikoa (hakimu mkazi) katika mikoa yote mipya yaani Geita, Njombe, Simiyu, Katavi na Mkoa wa Lindi.

Ujenzi wa majengo hayo ulianza na hivi upo katika hatua za mwisho na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Mwaka 2017/2018, Mahakama ya Tanzania ilianza kutekeleza ujenzi wa miradi 16 ya mahakama za wilaya nchini zikiwemo wilaya za Geita, Njombe, Bariadi, Lindi, Mpanda, Rungwe na Ruangwa. Mahakama nyingine za wilaya zinazojengwa ni Chato, Bukombe, Bunda, Kasulu, Sikonge, Kilwa Masoko, Kondoa, Longido na Kilindi.

Ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mahakama kwa wakati na kwa ukaribu zaidi, Mahakama ya Tanzania imeanza kutekeleza azima yake ya kuwa na Mahakama Kuu katika kila Mkoa. Tayari imeanza ujenzi wa majengo ya mahakama kuu katika mikoa ya Mara na Kigoma. Ujenzi huo umefikia hatua za ukamilishaji ambapo majengo hayo yanatarajiwa kuwa yamekamilika ifikapo Aprili, 2019.

Mwaka 2018/2019, Mahakama ya Tanzania imepanga kutekeleza miradi ya ujenzi wa mahakama za wilaya na za mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini. Mahakama za mwanzo zitakazojengwa ni katika maeneo ya Mtae (Lushoto), Mdandu (Wanging’ombe), na Mkunya (Newala). Mahakama nyingine za mwanzo zitajengwa maeneo ya Msanzi, Laela na Mtowisa (Sumbawanga), Uyole (Mbeya), Mlimba, Mang’ula na Ngerengere (Morogoro).

Katika mwaka huu wa fedha chini ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyokaa madarakani kwa miaka mitatu sasa, Mahakama ya Tanzania imepanga kujenga mahakama za wilaya katika Wilaya za Chunya (Mbeya), Ludewa na Makete (Njombe). Mahakama hizi za wilaya na za mwanzo zimeanza kujengwa tangu Oktoba mwaka huu baada ya taratibu za zabuni kutangazwa na kukamilika.

Kwa upande mwingine, Benki ya Dunia imekuwa bega kwa bega na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya mahakama yakiwemo majengo kwa kutoa ufadhili kupitia Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama. Kupitia ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Mahakama ya Tanzania, tayari mahakama kadhaa zimeshajengwa na kuanza kufanya kazi zikiwemo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkuranga, Ilala (Kinyerezi), Mahakama ya Wilaya na Mwanzo ya Kigamboni na ya Mwanzo ya Kawe.

Katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inakusudia kuendelea kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi kwa kujenga majengo sita ya Mahakama Kuu maarufu kama vituo vya utoaji wa Haki (Integrated Justice Centre) katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Mwanza na Arusha.

Aidha, katika Jiji la Dar es Salaam, Mahakama itajenga majengo hayo katika Wilaya ya Temeke na katika Viwanja vya Mahakama ya Tanzania vya Chimala vilivyopo jirani na Hospitali ya Ocean Road. Aidha, katika mwaka huu wa fedha, mahakama inakusudia pia kujenga majengo mengine 23 ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini. Yote haya ni matunda ya juhudi za Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli katika kipindi alichokwishawatumikia Watanzania cha miaka mitatu iliyotimia Novemba 5, 2018.

WABEBA nyama kwenye machinjio na mabucha watachukuliwa hatua za kisheria ...

foto
Mwandishi: Lydia Churi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi