loader
Picha

Utakula bata hivi hivi? Thubutu!

KUNA mwanasiasa mmoja amekuja na kauli yake ya ‘kazi na bata’ akiamini kwamba ndio itakayomwingiza ikulu.

Anasema anataka falsafa hiyo ichukuliwe na wagombea wengine wa urais mwaka 2020 na kwamba siku wakishinda basi falasfa itakayotawala Tanzania iwe ni hiyo, kazi na bata. Huyu jamaa, kwa lugha nyingine, kama ilivyo kawaida ya wapinzani wetu, anachofanya ni kutafuta ‘kukandia’ kila kinachofanywa na serikali ya awamu ya tano au kukitafutia kasoro.

Anataka kutuaminisha kwamba dhana ya ‘Hapa kazi tu’ inayohimiza uwajibikaji ili kila mtu ale jasho lake na siyo kuishi kwa kupiga madili na njia za mkato inasababisha Watanzania tusile bata! Kula bata hapa bila shaka anamaanisha kuwa na maisha bora na mazuri zaidi.

Anataka pia kutuaminisha kwamba sisi watanzania starehe kwetu ni muhimu pengine kuliko hata maendeleo yetu! Kwamba hakuna sababu ya kujenga misingi itakayotuhakikishia maendeleo endelevu mbele ya safari bali kila tunachovuna sasa ni kutumbua tu! Kanuni zote za maendeleo zinaonesha kwamba msingi wa mtu kula bata ni kuchapa kazi kwa bidii.

Ndio maana tunakutana na misemo ya wahenga kama ‘mchumia juani, hulia kivulini’ kwa maana ya kwamba kama hujatoka jasho sahau kula bata. Methali nyingine zinazotupeleka huko huko ni kama ile ya ‘usione vinaelea, vimeundwa’ kwa maana ya kwamba utajidanganya bure kutaka kuona na wewe una chombo kinachoelea baharini bila kukiunda.

Wahenga wanaposema ‘Roma haikujengwa siku moja’ wanamaanisha kwamba kazi ilifanyika ndipo leo tunaiona Roma ikimeremeta. Msemo wa kazi ni bata ni kama unapingana na dhana hiyo na kutaka kutuaminisha kwamba Roma ingeweza kujengwa ghafla (overnight)! Serikali ya awamu ya tano inapambana vilivyo kuhakikisha kwamba kama sasa Watanzania wanakula bata, basi siku si nyingi watakula mabata makubwa yaliyonona zaidi.

Hii ni sawa kabisa na msemo maarufu kwamba huwezi kwenda peponi bila kufa kwanza. Kazi kubwa imefanyika kuhakikisha matobo yaliyokuwa yanatorosha pesa zetu yanazibwa, mapato yakapanda kwa mwezi kutoka kubilioni hadi kwenye trilioni. Ndio sasa unaweza kuona tumeanza kununua ndege na kuboreha usafiri wa anga kwa pesa zetu.

Ndio unaona tumeanza pia kujenga reli ya kisasa kwa fedha zetu. Hivi ni ‘mabata’ mangapi Watanzania watakula baada ya reli hii kukamilika? Tunapoelekea Tanzania ya viwanda serikali ya awamu ya tano inachapa kazi kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika kupitia maporomoko ya Stiegler’s Gorge.

Hivi ni mabata mangapi Watanzania watakula baada ya kuwa na umeme wa uhakika zaidi na wa bei nafuu kuliko ilivyo sasa? Mbali na madaraja ya juu yanayoendelea kujengwa hususani katika jiji la Dar es Salaam, karibu kila mkoa barabara zinajengwa ili kuhakikisha mazao ya wakulima yanafika sokoni.

Haya yanawahakikishia wakulima kula mabata mangapi kuliko hali ilivyokuwa miaka ya nyuma? Niseme tu kwamba utakuwa mtu usioona mbele kuwaza kula bata bila kuchapa kazi kwa bidii kwanza.

Vinginevyo utataka kutafuta njia za mkato au kuiba, na zama hizo zimepitwa na wakati. Isitoshe, wachapa kazi wote kwa maana ya wanaofanya kazi za halali kila siku wanakula bata. Wanaoshindwa labda ni wale waliozoea kuishi kwa njia za mkato na ufisadi. Hawa bata sasa wanazisikia tu redio labda kama watakubali ukweli na kubadilika.

Kimsingi, hakuna aliyewazuia Watanzania kula bata. Kama ni kumbi za starehe zinaendelea kama kawaida na ndio maana tunasikia matamasha kama Wasafi au Fiesta yakiendelea kutangazwa ili wachapa kazi wakapate maeneo ya kuburudika na kujilia makuku yao na mabata. Tukubaliane kutokubaliana kwamba mtu mzima kukaa na kuibuka na kijimsemo hicho cha ‘kazi na bata’ akadhani amekuja na kitu cha maana kuipiku ‘hapa kazi tu’ kunaonesha uchanga katika kuyatazama mambo muhimu kwa mustakabali wa taifa letu.

LEO Watanzania wanakumbuka miaka 23 iliyopita, baada ya meli ya ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi