loader
Picha

Jaji- Kuna rushwa ya ngono vyuoni, mahakamani

JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Agnes Bukuku, amesema ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono, uko maeneo mengi ikiwemo vyuoni, mahakamani na hospitalini, hivyo aliitaka jamii isifumbie macho vitendo vya aina hiyo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Jumuiya Wataalamu wa Sheria, Majaji, Mahakimu, Mawakili na wanazuoni wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu AugustinoTanzania (SAUT) kilichopo Nyegezi Jijini Mwanza.

Alikuwa akizungumza katika Mahakama ya mfano (Moot Court), zinazofanyika katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na kuratibiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Africa (WiLDAF) na Chama cha Majaji Wanawake (TAWJA), kama sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

“Masuala ya ukatili siyo ya kufumbia macho, upo katika sehemu zote hata vyuoni kuna rushwa ya ngono, kwenye ofisi za serikali, hospitalini na mahakamani, TAWJA na WiLDAF wameona waandae Moot Court chuoni hapa kuwaongezea uelewa wanafunzi wa sheria ikiwa ni kuwaonyesha jinsi ya kuendesha kesi mahakamani," amesema Bukuku.

Pia alisema unyanyasaji wa kiuchumi dhidi ya wanawake ndani ya jamii, unatajwa kusababishwa na uelewa mdogo wa jamii, hasa kuhusu makosa ya jinai.

Alisema hali hiyo imechangia wanawake wengi waishio vijijini, kuendelea kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono na kuporwa haki yao ya kumiliki ardhi kimila.

Fatuma Kimwaga ambaye ni Mwanasheria wa Chama cha Wanawake Wanasheria (TAWLA), alisema rushwa ya ngono hasa maeneo kazi na vyuoni, inatajwa kuwa ni miongoni mwa vitendo vya unyanyasaji, vilivyoshamiri vinavyoitesa jamii.

Alisema hali hiyo ndiyo imekilazimu chama cha TAWJA na WiLDAF, kuona umuhimu wa kuwaelimisha wanafunzi wa vyuo vikuu, wajue namna mahakama zinavyofanyakazi na na tafsiri za kisheria.

Mwanafunzi wa Kitivo cha Sheria katika chuo hicho, Brightness Shija alisema mjadala huo wa kisheria, utakuwa chachu kwao katika kupambana na changamoto za kisheria na siyo kufanya maamuzi kwa msukumo wa kihisia.

Emmanuel Mtawa ambaye ni mwafunzi wa Sheria mwaka wa nne, alisema licha ya kwamba walikuwa wakifanya mafunzo kwa njia ya vitendo, lakini Moot Court hiyo iliyofanywa na mahakimu na wanasheria wazoefu, imewaongezea uelewa jinsi ya uendeshaji wa kesi mahakamani.

Mkuu wa Kitivo cha Sheria chuoni hapo, Dk. Erasma Rutechura alisema," shughuli hiyo ya Mahakama ya Mfano imefanyika kwa mara ya kwanza chuoni hapa na ni sehemu ya mitihani kwa baadhi ya wanafunzi wetu wa sheria wa mwaka wa pili, wa tatu na wa nne chuoni hapa".

Mahakama hiyo ya kuigiza imefanyika wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine, kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Mahakama inashirikiana na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (Tawja) na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Wildaf).

MAMLAKA ya Usimamizi wa Shughuli za Bima nchini (TIRA) kwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Mwanza

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi