loader
Picha

SMZ- Fedha Mfuko wa Jimbo ni za wananchi

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema fedha za mfuko wa jimbo ni za wananchi wa jimbo la uchaguzi na sio za mwakilishi hivyo zinatakiwa kutumika ili kuleta maendeleo yao.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed ametoa msimamo huo wakati anajibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliotaka wajumbe wa Viti Maalumu kupewa fedha za mfuko wa jimbo.

Mwakilishi wa Viti maalumu, Mwantatu Mbaraka aliwasilisha hoja binafsi inayoitaka serikali kutoa fedha hizo kwa Wawakilishi wa Viti maalumu ambao hufanya kazi za kuwahudumia wananchi.

Alisema katika muundo wa mfuko wa jimbo, Mwakilishi wa jimbo ni Mwenyekiti tu na si mtu wa mwisho wa maamuzi ya matumizi ya fedha.

Amesema anachojua katika hoja binafsi ni uwepo wa mabadiliko katika muundo wa mfuko huo ikiwemo kuingizwa Wajumbe wa baraza hilo wa Viti Maalumu kama sehemu ya mfuko huo.

''Tunaweza kuwaingiza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Viti maalumu kama sehemu ya mfuko wa jimbo na sio kuanzisha mwingine,'' amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud akijibu hoja alisema Zanzibar inayo bahati kuwa na mifuko miwili katika jimbo moja ikiwemo Mfuko wa Mbunge na Mwakilishi.

Alisema kinachotakiwa ni viongozi hao wawili kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzipatia ufumbuzi kero zilizopo katika jimbo la uchaguzi.

''Wenzetu Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waliwahi kulalamika kwanini Zanzibar wana mifuko miwili ya jimbo, wa Mwakilishi na Mbunge huku majimbo yao yakiwa na idadi ndogo ya watu na eneo,'' amesema.

Aboud aliwakumbusha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kusema kwamba kazi za kisiasa ni za kujitolea zenye uzito mkubwa ikiwemo kuwa tayari kuwahudumia wananchi wakati wowote.

''Hizo ndiyo kazi za kisiasa zinahitaji kujitolea na kuwa tayari kuwatumikia wananchi wakati wowote huku kiongozi ukitumia fedha binafsi, '' amesema.

WABEBA nyama kwenye machinjio na mabucha watachukuliwa hatua za kisheria ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi