loader
Picha

TUCTA wavunja ukimya mafao ya pensheni

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limesema bado kuna fursa ya majadiliano na Serikali kuhusu vikokotoo vya mafao ya pensheni vinavyolalamikiwa.

TUCTA imekiri kuwa, mchakato wa kutunga sheria ya kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kutunga kanuni ulifuata sheria na walishiriki hatua zote.

Hayo yamebainishwa na Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya wakati akitoa tamko la Kamati ya Utendaji ya Tucta iliyokutana hapa kwa siku mbili kuanzia juzi.

Pamoja na mambo mengine, Nyamhokya alisema kamati hiyo ilijadili kwa undani suala la kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na mkanganyiko uliojitokeza baada ya serikali kuanza kutangaza kuanza kutumika kwa vikokotoo vya mafao ya pensheni kwa wastaafu wa mifuko ya PSSSF na NSSF kuanzia Agosti 1, 2018.

Rais huyo wa Tucta alisema kwa kuzingatia hekima na busara, na kwa kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi nchini, ni vyema serikali ikaliona jambo hili kwa mtazamo chanya na kwamba kilio cha wafanyakazi sio jambo la kupuuzwa.

"Serikali ichukue hatua za haraka na za makusudi za kurudi kwenye meza ya mazungumzo na vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kuhakikisha suala hili linapatiwa ufumbuzi utakaoleta tija kwa wafanyakazi na Taifa kwa ujumla, " amesema Nyamhokya.

Alisema baada ya kikao chao hicho wamekubaliana kukutana haraka na waziri mwenye dhamana ya masuala ya Kazi wakiamini bado kuna fursa ya majadiliano na kuleta unafuu katika kikokotoo hicho.

Akifafanua alisema Tucta hawakubaliani na uamuzi wa kumlipa mstaafu mafao ya pensheni ya mkupuo ya asilimia 25 na asilimia 75 alipwe katika pensheni ya mwezi.

Aliongeza kuwa Tucta walipendekeza kwa serikali angalau itoe malipo ya mkupuo asilimia 40 na asilimia 60 ilipwe katika pensheni ya mwezi.

"Tucta tulienda mbali zaidi na kutoa pendekezo la kikokotoo cha 1/580, asilimia 40 malipo ya mkupuo, asilimia 60 malipo ya kila mwezi na miaka 15.0 iwapo serikali ingeona ugumu wa kupokea pendekezo letu la awali, " amesema Nyamhokya.

Amesema pendekezo lao la awali ni kuitaka serikali iendelee na Kanuni za Mafao za mwaka 2017 ambazo zinatoa malipo ya mkupuo wa asilimia 50, kikokotoo cha 1/540 na umri wa kuishi baada ya kustaafu miaka 15.5 kwa wafanyakazi walioko kwenye mifuko.

Alikiri hoja ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ilianzishwa na wafanyakazi tangu mwaka 2004 kwa lengo la kuboresha mafao ya wafanyakazi na wastaafu.

Alisema waliamini mifuko hiyo ikiunganishwa gharama za uendeshaji na ushindani usiokuwa na tija kwa mfanyakazi ingepungua, hivyo mifuko kuokoa fedha nyingi ambazo zingeelekezwa katika kuboresha mafao ya wafanyakazi.

Amesema Tucta ilishiriki kwa niaba ya wafanyakazi katika majadiliano ya utatu kupitia vikao vya kisheria ambavyo pia vilitoa fursa ya wawakilishi wa wafanyakazi kukutana na kujadiliana na wadau wote wakiwamo waajiri, serikali, Kamati za Bunge, mashirika yasiyo ya kiserikali, watumishi wa mifuko iliyokuwepo kabla ya kuunganishwa na wafanyakazi wenyewe.

Aidha, alisema Tucta kama mwakilishi wa wafanyakazi nchini ilishiriki katika mchakato mzima wa kutungwa sheria ya PSSF Namba 2 ya mwaka 2018 kwa kutoa maoni na msimamo wao kwenye vikao mbalimbali vya wadau.

"Ni wajibu na haki yetu kusema kwamba mapendekezo yetu kwenye sheria hiyo yalizingatiwa kwa kiwango kikubwa sana zaidi ya asilimia 80. Tatizo kubwa limekuja kujitokeza kwenye utungwaji wa kanuni," amesema Rais wa Tucta.

Amebainisha kuwa utungaji wa kanuni hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu waliwashirikisha wadau wote wakiwamo Tucta, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), wataalamu kutoka katika mifuko ya hufadhi ya jamii na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Alisema katika vikao hivyo serikali ilieleza kuwa ujio wa kikokotoo cha asilimia 25 badala ya asilimia 50 na miaka 12.5 badala ya 15.5 ya awali ilitokana na hatari ya kufilisika kwa mifuko ya PSPF na LAPF.

Aliongeza kuwa baada ya wasilisho la Tucta la hoja za wafanyakazi walishindwa kukubaliana hivyo serikali iliamua hoja za pande zote ziwasilishwe katika Baraza la Utatu la Ushauri (LESCO) ambako pia waligonga mwamba.

"Kupitia tamko hili, Tucta tunawaomba wafanyakazi wote nchini kuwa watulivu na kupuuza uvumi kwamba wafanyakazi kupitia shirikisho lao tulikubali vikokotoo vipya. Ukweli ni kwamba tangu hatua za awali hadi kutangazwa kwa kanuni hizi Tucta tumepinga ujio wa kanuni hizi na hata sasa na hata sasa hatukubaliani nazo, " ameeleza Nyamhokya.

Alisema ana imani waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi na viongozi wengine nchini akiwamo Rais John Magufuli watasikia kilio cha wafanyakazi.

Hivi karibuni, SSRA ilitoa ufafanuzi wa kikokotoo kipya na kueleza kuwa kilizingatia hali halisi ya mifuko na kimekuja kuleta uwiano wa viwango vya mafao kwa wanachama wote. Pia ilisema vikokotoo hivyo vimekuwa vikitumiwa na mifuko hiyo tangu mwaka 2014.

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga ameonesha kukerwa na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi