loader
Picha

RC ashauri mbinu wasomi kuupanda mlima Kilimanjaro

SERIKALI imetaka wakuu wa shule za sekondari na vyuo vikuu mkoani Kilimanjaro, kuandaa utaratibu maalumu ambapo wahitimu wa taaluma mbalimbali, hawatatunukiwa vyeti vyao bila kwanza kupanda Mlima Kilimanjaro.

Mpango huo umelenga kuhamasisha utalii wa ndani lakini pia kuongeza mapato, jambo ambalo litasaidia uimarishwaji wa miradi ya kijamii hususan vijiji vinavyozunguka mlima huo.

Mkuu wa Mkoa huo, Anna Mghwira alisema hayo jana wakati akizindua kampeni ya kupanda mlima huo kama sherehe za miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania zenye kaulimbiu, ‘Ujasiri na uzalendo, dira ya kuimarisha utalii Tanzania’.

Akizungumza kwa niaba ya Mghwira, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu alisema serikali itaandaa mazingira rafiki kusaidia kutekelezwa kwa mpango huo kwa mafanikio.

“Leo tunashuhudia timu ya watu 40, wakiwemo wanajeshi kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), wanahabari na watendaji wa Taasisi ya Benjamin Mkapa na Umoja wa Ushirikiano baina ya Tanzania na China, wanapanda mlima huu,” alisema.

Alisema endapo mpango huo wa shule za sekondari na vyuo hivyo wa kupanda Mlima Kilimanjaro utaanzishwa utasaidia kujenga uzalendo na ujasiri kulinda rasilimali za Taifa.

Katika safari hiyo iliyoratibiwa na Tanapa kwa kushirikiana na Kampuni ya kupandisha Watalii Mlima Kilimanjaro ya Zara, na kupanda mlima kupitia njia ya Marangu, Mghwira alitaka wadau zaidi kuunga mkono juhudi za serikali. Alitaka viongozi waliopewa dhamana ya kulinda rasilimali za Taifa kufanya kazi hiyo kwa uzalendo na kuwa na mikakati ya kuzilinda.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Tanapa, Jenerali mstaafu, George Waitara alisema mpango kupanda mlima huo ulianza mwaka 2008 na lengo ni kuhamasisha utalii wa ndani na utunzwaji wa mazingira na maliasili za Taifa. “Awali wakati naongoza kampeni ya kupanda mlima huu sikuwa nafahamu kama nitakuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanapa. Nimebaini tunahitaji uzalendo na ujasiri katika kulinda rasilimali za Taifa, kinyume na hapo rasilimali hizi zitapotea na dunia itatushangaa,” alisema.

SERIKALI mkoani Songwe imewataka wakulima wa zao la alizeti kubadilika ...

foto
Mwandishi: Nakajumo James, Moshi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi