loader
Picha

TRA , TLS wajadili ulipaji kodi

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na mawakili kwa lengo la kusikiliza hoja na changamoto za kiutendaji za kikodi wanazokutana nazo katika majukumu ya kila siku ili kwa pamoja watambue njia ya kuzitatua.

Kamishna wa kodi za ndani wa TRA, Abdul Mapembe amesema hayo kwenye mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema jukumu lao ni kukusanya mapato ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu hivyo TRA imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali na kujadiliana mambo ya kikodi.

Awali, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema mamlaka hiyo inatambua umuhimu wa kuwa na mahusiano kati yake, walipa kodi na wadau wengine ndio maana imetengeneza mkataba wa huduma na mlipakodi kuonyesha dhamira yake ya kutoa huduma bora kwa walipakodi na wadau wengine.

Alitaja mambo manne muhimu ambayo ni wajibu na haki ya mlipakodi ambapo mamlaka inategemea kutoka kwa walipa kodi na mawakili kuwa ni kusajiliwa, uwasilishaji wa ritani za kodi, usahihi wa ritani au madai ya marejesho pamoja na malipo ya kodi kwa wakati.

Alisema Rais John Magufuli kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza wananchi kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

“Lengo hili litatimia endapo sisi sote tutashirikiana na kutimiza wajibu wetu ikiwemo kulipa kodi stahiki kwa wakati, kuboresha ushirikiano baina ya serikali na wafanyabiashara, kutofumbia macho vitendo vya rushwa, magendo, uhalifu na uhujumu uchumi na vitendo vingine ambavyo vinasababisha nchi kupoteza mapato,” amesema.

Wakichangia hoja katika mkutano huo mawakili wamesema wamekuwa wakipata changamoto katika maeneo ya kazi yao hivyo wakati mwingine wanatoa msaada wa kisheria kwa mteja lakini hawalipwi pesa kwa wakati ilhali TRA inawahitaji walipe kodi.

Pia walisema mashine ya kielektroniki ya EFDs huuzwa kwa bei kubwa hivyo inawavunja moyo mawakili vijana wanaotaka kujiajiri.

“Hela ya EFDs mashine ni kubwa sana inavunja tama vijana kuanza biashara, mngetafuta utaratibu wa kupunguza gharama,” amesema wakili mojawapo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS), Kaleb Gamaya amesema inapofika wakati wa kuhuisha leseni mawakili wanakuwa na hofu katika hilo.

Pia aliomba TRA kuwepo na dawati maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala ya mawakili badala ya kusumbuka muda mrefu kuyafuatilia.

ILI Tanzania ijenge Uchumi wa Viwanda, hadi kufikia mwaka 2025 ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi