loader
Picha

Azaki waomba maboresho sheria ya takwimu

ASASI za Kiraia (AZAKI) zimeiangukia serikali na kuiomba kuboresha sheria mpya ya takwimu, ili kuzipa uhuru wa kukusanya takwimu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Policy Forum, Japhet Makongo ambaye aliomba serikali iyazingatie maoni yao na kurekebisha sheria hiyo ili kuhakikisha misingi ya utawala bora inazingatiwa kama ilivyoanishwa kwenye Katiba ya mwaka 1977 ambayo ni sheria mama.

“Sisi tunaamini kuwa uhuru wa kupata na kusambaza taarifa ni nguzo muhimu katika kuchochea ushiriki wa wananchi na wadau katika maendeleo ya nchi,”alisema Makongo.

Kauli hiyo ya Makongo imekuja baada ya hivi karibuni serikali kutaka mchakataji wa taarifa za takwimu lazima aombe kibali kabla ya kusambaza kwa umma.

Mapendekezo ya sheria hiyo yapo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 3 ya mwaka 2018, uliosomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano uliopita wa Bunge.

Kwa mujibu wa marekebisho hayo, The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.3) Act, 2018 mtu yeyote aliyechakata taarifa za takwimu atalazimika kuomba idhini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kabla ya kusambaza kwa umma takwimu hizo.

Makongo alisema kuwa sheria ni nzuri, ila wanaomba baadhi ya vipengele viongezwe, makosa na adhabu chini ya sheria hii yajikite katika kusimamia mchakato mzima wa upatikanaji na usambazaji wa takwimu rasmi na sio takwimu zote.

Alieleza kuwa makosa na adhabu zinazohusiana na upotoshaji wa taarifa nyingine tayari yanashughulikiwa na sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 na sheria nyingine.

Alisema mapendekezo mengine ambayo wanaiomba serikali ni itambue uwepo wa taasisi na wadau wanaoandaa takwimu huru ambazo ni mbadala wa takwimu rasmi ili kuwezesha kuwepo kwa mijadala hai na chanya kwa maendeleo ya taifa letu.

“Kwa kuwa sheria imetoa tafsiri ya ‘takwimu rasmi’ ni vema pia itoe tafsiri ya neno ‘takwimu zisizo rasmi’ na kuweka mipaka iliyo wazi baina ya maneno hayo,” alisema Makongo na kuongeza.

Sheria iondoe sharti la kuomba vibali zaidi ya mara moja kwenye kuandaa, kukusanya na kusambaza takwimu rasmi.

Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Florence Majani alisema, “Sheria ni nzuri na ina umuhimu wake, lakini inabidi iboreshwe kidogo, kwa sababu tunafahamu Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ya kimataifa kama ule ya Afrika wa Bangui, na lile tamko la kidunia wa Universal Declaration of Human Right, hii yote inataka haki za watu kupata taarifa.

Amesema taasisi ya Tamwa inashughulika na masuala ya ukatili wa kijinsia, hivyo inapata ugumu katika ukusanyaji wa takwimu kwani bila takwimu hizo, watu hawatajua ukubwa wa tatizo.

SERIKALI mkoani Songwe imewataka wakulima wa zao la alizeti kubadilika ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi