loader
Picha

Athari kisima cha gesi zifanyiwe kazi haraka

SERIKALI imeahidi kuchukua hatua za haraka kudhibiti athari za mmomonyoko wa ardhi katika kisima cha gesi asilia kilichoko kijiji cha Msimbati, Kisiwa cha Mnazi Bay, Mtwara.

Imesema inajipanga kujenga ukuta kuzuia athari hizo kutokana na kuongezeka kwa kina cha Bahari ya Hindi na maji kutishia kumeza eneo hilo lote.

Tumeshtushwa na habari hizo na tunaungana na wananchi kuzitaka mamlaka husika, Wizara ya Nishati na inayohusika na uhifadhi mazingira, kuchukua hatua za haraka za dhati kukabili hali.

Habari za kisima hicho kinachotoa gesi asilia inayotumika kama nishati ya umeme na uzalishaji viwandani kuwa hatarini kumezwa siyo nzuri kwa Taifa na hata jumuiya ya kimataifa.

Si nzuri kwa sababu inatishia kurudisha nyuma maendeleo makubwa ambayo nchi inaelekea kupata kwa kuvuna gesi asilia na kuitumia.

Ni kutokana na hali hiyo, tunaungana na jamii yote inayopenda maendeleo ya nchi na jumuiya ya kimataifa, kuiomba serikali, ichukue hatua za dharura zinazolenga kuwezesha mamlaka husika, kudhibiti hali hiyo kabla haijaleta athari.

Na wakati ikichukua hatua hizo za kujenga ukuta na kutafakari njia nyingine bora za uvunaji gesi hiyo kwa kuboresha mfumo wake wa uvunaji au kuhamisha kisima, itoshe kusema hili liwe fundisho katika upembuzi yakinifu.

Yamkini kuwa wataalamu waliohusika kwa kutumia teknolojia ya vipimo au hata hesabu walipaswa kuona hilo mapema katika upembuzi na kupendekeza njia kulikabili kabla ya kukua kufikia hatua ya kuleta madhara.

Kwa kuwa tayari ni tatizo, huu si muda tena wa kutafuta mchawi bali kuunganisha nguvu zetu pamoja kutafuta muafaka wa uvunaji gesi hiyo.

Sisi tunaamini kuwa tunao wataalamu wazuri tu wenye uwezo mkubwa wa kutabiri majanga kwa kutumia vipimo vya hali ya hewa au teknolojia na mahesabu ya kawaida ya ukadiriaji viwango.

Ni muhimu basi utaalamu huo ukatumika kila mara tunapokuwa na miradi siyo ya nishati tu baharini au nchi kavu, bali hata miradi mingine.

Ndio maana tunasema ni vyema tatizo hili likawa fundisho kwetu na kutusaidia kujipanga katika kupambana na majanga au matatizo yetu.

Sisi tunaamini kama Taifa tunao uwezo mkubwa wa kukabili matatizo yetu na hata hili tutaweza kuweka gesi katika hali ya usalama.

Kama serikali imetumia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kununua korosho na kuwahakikishia wakulima wake wa mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Lindi na Pwani uhakika wa soko na mafao, vipi ishindwe hili.

Ni suala la kujipanga tu haraka kwa JWTZ na taasisi nyingine zinazohusika na ujenzi kama SUMA JKT, wizara husika, wananchi na pia wahisani wanaohusika na masuala ya tabia nchi kushirikiana kwa hali na mali kupambana nalo.

HAKUNA ubishi kwamba ili kuimarisha biashara yoyote ile duniani, zikiwemo ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi