loader
Picha

Mahakama inavyonufaika na matumizi ya Tehama

KATIKA toleo la jana, LYDIA CHURI aliandika makala yenye kichwa cha habari kisemacho Miaka Mitatu ya JPM; Mahakama ya Tanzania na maboresho utoaji huduma alipozungumzia maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwamo ya majengo ya mahakama nchini, kwa kipindi cha miaka mitatu ambayo Rais John Magufuli (JPM) amewatumikia Watanzania katika wadhifa huo.

Leo, anazungumzia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika mhimili huo. Fuatilia. Kutokana na Mahakama ya Tanzania kuamua kujikita katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama) katika uendeshaji shughuli zake, majengo yote yanayojengwa hivi sasa yanajengwa kwa kuzingatia matumizi ya tehama ili kurahisisha shughuli zote za utoaji wa haki kwa wananchi.

Hivyo, Mahakama ya Tanzania imejikita katika matumizi hayo hasa katika kuhifadhi taarifa za mashauri yote yanayosajiliwa kuanzia yanapofunguliwa mpaka yanapoisha. Hadi sasa jumla ya mashauri 55,677 yamesajiliwa yakiwemo mashauri 24,317 ya madai na 31,360 ya jinai.

Mwaka 2014 Mahakama ya Tanzania ilianzisha mfumo wa kuhifadhi taarifa za mashauri ujulikanao kama ‘Judicial Statistical Dashboard System (JSDS)’ ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za takwimu, ili zisaidie katika kupanga mipango ya maendeleo ya mahakama kulingana na rasilimali zilizopo. Hii inalenga kuzifanya takwimu hizo pia zisaidie katika utekelezaji wa kila siku wa kazi za mahakama.

Lengo la awali ya kuanzishwa kwa mfumo huu lilikuwa ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa za takwimu kwa ajili ya kusaidia kupanga shughuli za maendeleo ya taasisi, lakini baadaye ikaonekana kuna umuhimu mfumo huu kufanya kazi nyingine za kurahisisha upatikanaji wa haki. Kutokana na hali hiyo, mwaka 2017, Mahakama ya Tanzania iliamua kuuboresha mfumo huo na kuuita JSDS II.

Baada ya kuboreshwa kwa mfumo huu, wananchi wanaweza kusajili mashauri yao kwa njia ya mtandao na pia kuweza kutuma taarifa mbalimbali kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno wa simu ya mkononi kuwataarifu wadaawa na wahusika wote wa haki, juu ya hatua mbalimbali za mashauri yao zilipofikiwa zikiwemo taarifa za ratiba za mashauri mahakamani.

Aidha, mfumo huu wa mashauri pia umeunganishwa na mfumo wa malipo wa Serikali (Government e-payment gateway-GePG) hivyo utawawezesha wananchi kulipa ada mbalimbali kama vile za kusajili mashauri kwa njia ya mtandao kupitia Mpesa, Tigopesa, Airtel Money n.k. Faida za matumizi ya Tehama mahakamani Mahakama ya Tanzania inatumia tehama ili kurahisisha utoaji wa haki kwa wakati.

Matumizi ya tehama kwa Mahakama ya Tanzania yanasaidia kuokoa muda na kupunguza gharama kwa wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki zao. Kupitia mifumo ya tehama iliyoanzishwa na mahakama, wananchi sasa watakuwa na muda mrefu wa kufanya shughuli zao za kiuchumi zinazowaingizia kipato badala ya kutumia muda mwingi mahakamani.

Aidha, taarifa mbalimbali muhimu za kimahakama sasa zitakuwa zikipatikana kwa wakati zikiwemo nakala za hukumu, mienendo ya kesi n.k. Kadhalika, katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli (JPM) matumizi ya tehama yanaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na kuongeza uwazi katika masuala mbalimbali.

Kuwepo kwa uwazi (transparency) pia kunasaidia kuondoa ama kupunguza vitendo vya rushwa. Mfumo wa takwimu za mashauri Hadi hivi sasa, mfumo huu wa takwimu za mashauri unafanya kazi katika mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi, mahakama kuu pamoja na mahakama ya rufani. Hata hivyo, mfumo huu haujawekwa kwenye mahakama za mwanzo kutokana na idadi kubwa ya mahakama hizo kutokuwa na miundombinu rafiki inayowezesha kutumika kwa mfumo huu.

Lengo la Mahakama ya Tanzania ni kuwa na mfumo huu katika ngazi zote za mahakama zikiwemo mahakama za mwanzo nchini. Mahakama inafanya jitihada kuwezesha mfumo huu uanze kutumika kwenye mahakama za mwanzo zilizo na miundombinu itakayowezesha matumizi ya mfumo huu wa JSDS, zikiwemo Mahakama za Hakimu Mkazi katika Mkoa wa Pwani.

Nyingine ni Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo ya Kigamboni, Mahakama ya Mwanzo ya Kawe, na Mahakama za Wilaya za Mkuranga na Bagamoyo. Mifumo mingine iliyoanzishwa na Mahakama Sambamba na kuanzishwa kwa mfumo wa takwimu za mashauri (JSDS), mahakama inayo mifumo mingine inayorahisisha suala zima la utoaji wa haki kwa wananchi.

Mifumo hiyo ni pamoja na ule wa taarifa za mawakili yaani ‘Tanzania Advocates Management System’ (TAMS). Mfumo huu unawasaidia wananchi kuwafahamu mawakili halali. Kwa msingi huo, wananchi wanashauriwa kutembelea mfumo huu ili kuthibitisha kama wakili atakayemwakilisha kwenye kesi yake ni halali. Mfumo mwingine ulioanzishwa na mahakama ili kurahisisha suala la utoaji wa haki ni huu wa kuhifadhi nakala za hukumu unaoitwa ‘Judgement Management System’ (JMS).

Mfumo huu hutumika kuhifadhi hukumu zote zilizotolewa na majaji pamoja na mahakimu. Kupitia mfumo huu, hukumu zote hupatikana bure kwa wananchi. Kadhalika, mfumo huu unawasaidia wanafunzi pamoja na watafiti katika kazi zao za utafiti na masomo ambao hupata nafasi ya kuzipitia kesi zote zilizotolewa maamuzi au zilizomalizika na kufahamu kwa undani maamuzi hayo.

Aidha, mfumo mwingine unaotumiwa na Mahakama ya Tanzania ni mfumo wa teknolojia ya mawasiliano kwa njia ya picha za video (video conferencing). Mfumo huu hutumiwa na mahakama kuendesha kazi zake kama vile kusikiliza mashauri pamoja na kufanya mikutano ya kazi. Hadi hivi sasa, mfumo huu tayari umefungwa katika Kituo cha Mafunzo cha Mahakama kilichopo Kisutu, Dar es Salaam na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya. Mpango uliopo ni kufunga mfumo huu kwenye Mahakama Kuu zote nchini pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kilichopo Lushoto mkoani Tanga.

Tovuti ya Mahakama ya Tanzania ni miongoni mwa mifumo unaotumiwa kutoa taarifa mbalimbali za kazi zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania. Tovuti ya mahakama humwezesha pia mwananchi kuingia kwenye mifumo mingine ya mahakama.

Aidha; Blogu huwezesha utoaji wa taarifa mbalimbali za kazi zinazofanywa. Pamoja na juhudi zote za Mahakama ya Tanzania kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati kwa kubuni mikakati mbalimbali ya kurahisisha utoaji na upatikanaji wa haki, bado wadau pamoja na wananchi wanao wajibu wa kuhakikisha wanashirikiana na mahakama ili itekeleze jukumu lake la msingi na la kikatiba la utoaji wa haki.

Rais John Magufuli amewapa wiki moja ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi