loader
Picha

Wapishi waalikwa maonesho ya utalii

WAPISHI wabobezi kutoka Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar wamealikwa kushiriki maonesho ya utalii ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Karibu Kusini) yatakayofanyika kati ya Desemba 12 na 16, mwaka huu, mjini Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema mpango huo utawawezesha wapishi wa hoteli  za mkoani Iringa kujifunza na kubadilisha uzoefu na wapishi hao ili kuboresha zaidi shughuli zao.

“Kutakuwa na upishi mbashara kutoka kwa wapishi wa hoteli mbalimbali za mikoa hii ya kusini, lakini tutaalika wapishi kutoka Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha. Ukienda Dar es Salaam pale kuna wapishi kama Sele Bonge, Mark Juice, Uiso na kule forodhani Zanzibar kuna wapishi wazuri sana wa vyakula vya pwani-tutawaleta,” amesema.

Amesema mikoa ya kusini haiwezi kuzungumza habari ya kukuza utalii kama baadhi ya hoteli zake zitaendelea kutengeneza vyakula visivyo na viwango na ubora unaokidhi mahitaji ya watalii wa ndani na nje ya nchi.

Mbali na maonesho hayo kunogeshwa na wapishi hao, amesema kutakuwa pia na mabanda yanayotangaza shughuli mbalimbali za utalii zinazofanywa na taasisi mbalimbali katika mikoa hiyo.

“Lakini pia kutakuwepo na fursa ya kuwapeleka wananchi katika vivutio mbalimbali ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni kubwa kuliko zote nchini,” amesema na kuongeza kwamba watakaokosa fursa hiyo kutakuwa na mabanda yatakayokuwa na baadhi ya wanyama kama simba, chui, fisi na wengineo.

Ametoa mwito kwa halmashauri zote za mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Rukwa na Katavi kushiriki maonesho haya na kuvitangaza vivutio vyake vyote.

Amesema lengo kuu la maonesho hayo ni kutangaza fursa na vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa hiyo ili wananchi na wageni kutoka ndani na nje wavifahamu na kuvitembelea ikiwa ni sehemu ya mikakati yao ya kukuza utalii katika kanda hiyo.

Amesema vivutio hivyo vikitembelewa vitaongeza ajira kwa wananchi, mapato, fursa za uwekezaji zitabainishwa ipasavyo pamoja na wananchi kujua umuhimu wa utunzaji mzuri wa maliasili na mzingira.

Mratibu wa Utalii wa Mkoa wa Iringa, Hawa Mwachaga alisema mkoa wa Iringa umepewa dhamana ya kuwa mwenyeji wa maonesho hayo baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuuteua na kuutangaza kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa hiyo.

Alisema mikoa hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na kampuni ya Capital Plus International pamoja na wadau mbalimbali imekuwa ikiandaa maonesho hayo tangu yaasisiwe mwaka 2016.

Katika vivutio vya kihistoria na kiutamaduni alisema, mikoa hiyo ina vivutio ambavyo sehemu kubwa vimehusishwa na historia ya mfumo mzima wa utawala na kupigania uhuru tangu enzi za vita dhidi ya uvamizi wa wakoloni.

Na kwa upande wa vivutio vya kiikolojia alisema mikoa hiyo inatambulika kwa kuwa na hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni kubwa kuliko zote nchini na Afrika Mashariki, Kitulo, Udzungwa, Katavi, Kipengere, Mapango, michoro na mito mikubwa.

TANZANIA na Uganda zimeanzisha rasmi Jukwaa la Biashara baina ya ...

foto
Mwandishi: Frank Leonard, Iringa

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi