loader
Picha

Mbowe, Matiko kuendelea kusota rumande

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kusikiliza kesi ya msingi ya uchochezi inayowakabili na wenzao saba.

Mahakama hiyo imetoa ruhusa kwa mmoja wa washitakiwa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ahudhurie michezo ya mabunge Afrika Mashariki nchini Burundi.

Hakimu Wilbard Mashauri pia ameruhusu Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, aendelee kumuuguza mkewe ambaye amejifungua kwa upasuaji hivi karibuni.

Mbowe na Matiko watakuwa mahabusu pengine hadi mwakani kwa kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesitisha usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na washitakiwa hao kupinga uamuzi ya Mahakama ya Kisutu ya kuwafutia dhamana.

Mahakama Kuu imesitisha usikilizwaji wa rufaa hiyo baada ya upande wa Serikali kudai kuwa wanakusudia kukata rufaa kupinga uamuzi wa Jaji Sam Rumanyika aliyesema rufaa ya akina Mbowe ipo mahakamani hapo kisheria na kwa maana hiyo, haina mamlaka ya kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Jaji Rumanyika alisema, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) anapewa mamlaka ya kukata rufaa kwa uamuzi mdogo chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa na kwamba kunapokuwa na taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri.

Leo Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai mbele ya Hakimu Mashauri kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba washitakiwa Mdee na Heche hawapo mahakamani.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa, Heche alitolewa taarifa kuhusu kufanyiwa upasuaji mdogo kwa mke wake lakini afya ya mtoto si nzuri.

Amesema, mshitakiwa mwingine, Mdee yupo nchini Burundi kushiriki mashindano ya mabunge ya Afrika Mashariki. Mdhamini wa Mdee, Fares Robinson ameieleza mahakama hiyo kuwa Mbunge huyo yupo Burundi kwa safari za kibunge.

Kwa mujibu wa mdhamini huyo, Katibu wa Bunge aliandika barua kwa Hakimu Mfawidhi wa mahakama kumtaarifu kuwa mshitakiwa huyo atakuwa nje kwa shughuli za kibunge na kwamba atarudi Desemba 20, mwaka huu.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Nchimbi amedai kwa, walipokea hati ya wito ikiambatanishwa na maombi ya ruhusa ya kupitia Mdee kupitia kwa Katibu wa Bunge.

Amedai kuwa, kwa mantiki hiyo wanaona washitakiwa wanafuata taratibu na hawana pingamizi na hilo.

Upande wa mashitaka pia umesema, hawana pingamizi kwa Heche kumuuguza mkewe ikizingatiwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa tu.

Hakimu Mashauri amesema, walipokea barua kutoka kwa Katibu wa Bunge kuomba ruhusa ya Mdee kwenda Burundi kuhudhuria michezo ya EAC na kwamba pande zote za utetezi na mashitaka walikuwa Mahakama Kuu kwa kesi nyingine.

"Mahakama inamruhusu mshitakiwa kuhudhuria michezo na ruhusa ya Heche ya kumuuguza mkewe imekubaliwa lakini wazingatie kuwepo mahakamani siku ya kutajwa kesi hiyo Desemba 21, mwaka huu, "amesema Hakimu Mashauri.

Mahakamani hapo kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi waliozuia baadhi ya wafuasi wa Chadema kuingia mahakamani na badala yake waliwaruhusu viongozi wa chama hicho pekee.

Washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kutowachagua wagombea uongozi katika Uchaguzi ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi