loader
Picha

Ukuta waua wanafunzi Dar es Salaam

WANAFUNZI wawili wa shule za msingi Kijichi na Bwawani zilizopo Mtoni Kijichi wilayani Temeke, Dar es Salaam wamekufa baada ya kuangukiwa na ukuta leo asubuhi. Katika tukio hilo wanafunzi watatu walijeruhiwa.

Waliokufa ni Sabra Stambuli (10) wa darasa la pili A shule ya Bwawani, na Nasri Mjenge (8) wa darasa la kwanza shule ya Kijichi.

Ukuta ulioanguka ulikuwa unazitenganisha shule hizo na makazi ya watu, na pembeni kidogo kuna bonde dogo na mtaro wa kupitishia maji machafu.

Licha ya kuwa katika mazingira hayo imebainika kuwa ukuta huo mrefu ulijengwa kwa matofali tu bila kuimarishwa kwa nondo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Butiama, Haji Mgaya amesema, alipigiwa simu akaelezwa kuhusu tukio hilo na alipofika kwenye eneo la tukio alikuta wanafunzi wawili wamedondokewa na ukuta.

Amesema, alimkuta Sabra akiwa amelaliwa na ukuta kuanzia kiunoni hadi miguuni, na Nasri alikuwa amedondokewa kichwani.

Amesema, waliwatoa watoto hao ili kuwawahisha hospitali, Nasri alikuwa ameaga dunia na Sabra alipoteza maisha akiwa njiani kupelekwa hospitalini.

Mgaya amesema, ni kawaida kwa wanafunzi kucheza kwenye eneo la shule wakiwemo wanaokimbia kimbia kwenye eneo hilo la bonde jirani na ukuta huo.

Amesema, huenda kwenye kucheza huko waliugusa au kuushika hivyo kwa kuwa haukuwa imara ukaanguka.

Mgaya amesema, ukuta huo uliojengwa mwaka 200, na inaonekana walioujenga hawakuzingatia viwango stahiki kwa kuwa licha ya kuwa upo kwenye eneo la bonde karibu na mtaro wa kupitishia maji hakujengwa kwa viwango vinavyoendana na mazingira hayo.

Baba Mkubwa wa Sabra, Selemani Stambuli amesema, kwenye tukio hilo familia yao imempoteza mtoto huyo na mwingine, Mukrim Stambuli anayesoma darasa la pili amejeruhiwa.

“Familia ina huzuni kubwa ya kupotelewa na mtoto mmoja ambae hakika ni pigo kwetu. Tumepata habari hizo asubuhi na mchana huu nimekwenda kuhakikisha kwenye hospitali ya Temeke na kukuta kweli aliyetangulia mbele ya haki ni ndugu yangu ”amesema Stambuli.

Mwenyekiti wa Kamati ya Taaluma ya Mtaa wa Butiama, Salum Mohamed Ally amesema, tukio hilo limewaamsha na watahakikisha kuwa wanaendesha operesheni kukagua ubora wa kuta za shule zote kwenye eneo hilo.

”Hii shule imejengwa mwaka 1972 na ni miaka mingi huku ikiwa imewasomesha watoto wengi na wengine kwa sasa ni watu wazima wanaishi hapa, kwa pamoja tukio hili limetugusa na kutufundisha kikubwa ninawataka wazazi na walezi pamoja na ndugu kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu” amesema Ally.

Kamanda Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Emmanuel Kikula amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuthibitisha idadi ya waliopoteza maisha na majeruhi.

Kamanda amesema, ofisi yake inaendelea kuchunguza kubaini chanzo cha tukio hilo.

Mwanafunzi wa darasa la sita Ally Juma amesema, leo walienda kuchukua matokeo ya mitihani ya kufunga mwaka, wakaambiwa wasubiri yanaandaliwa hivyo wengine walienda kucheza jirani na ukuta huo.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Kijichi, Twaha Kifundi amewataja wanafunzi waliojeruhiwa kuwa ni Mukrim Stambuli wa darasa la pili Bwawani, Sharifa Ibrahim wa darasa la tatu wa shule ya Kijichi na Rehema Nongwa wa darasa la pili shule ya Bwawani.

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kutowachagua wagombea uongozi katika Uchaguzi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi