loader
Picha

Ziwa Nyasa na vivutio lukuki vya kitalii

UKITEMBELEA mwambao mwa Ziwa Nyasa, utashuhudia maeneo mengi yenye fukwe za mchanga unaovutia. Hili ni ziwa linaloshika nafasi ya tatu kwa ukubwa kati ya maziwa yaliyopo barani Afrika.

Ziwa hili linazihudumia nchi za Tanzania, Malawi na Msumbiji huku wananchi wa nchi hizi na wageni wengine wakinufaika na ziwa hilo kwa uvuvi wa samaki na viumbe wengine waishio majini kwa chakula na biashara. Ukifika katika Kijiji cha Mtupale kilichopo Kata ya Chiwanda utaona fukwe za mawe ambazo ni kivutio adimu cha utalii. Nakumbuka mwaka jana (2017) aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alifanya ziara ya siku nne ya kutembelea Mkoa wa Ruvuma.

Katika ziara hiyo Profesa Maghembe alivutiwa na vivutio vya Ziwa Nyasa wakiwemo aina zaidi ya 500 za samaki wa mapambo ambao imethibitishwa kuwa hawapatikani katika maziwa, mito na bahari sehemu nyingine yoyote duniani.

Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, tafiti zinaonesha kuwa katika Sayari ya Dunia, hakuna ziwa lenye samaki wa mapambo wa aina zaidi ya 400, bali ni Ziwa Nyasa pekee, ambalo pia linaongoza duniani kwa kuwa na viumbe wengi kati ya maziwa yenye maji baridi. Katika ziwa hili pia zipo fukwe nyingine zenye vivutio kwa watu. Vivutio hivi ni pamoja na ndengere, ngindo, lundo, lipingo, mkali, hongi, liuli, kihagara, mkili, lundu, mbaha, ndumbi na nyinginezo.

Kijiji cha Ndumbi ndicho chenye bandari ambayo makaa ya mawe yanayochimbwa na Kampuni ya TanCoal. Ni mahali unapoweza kutumia darubini kuitazama nchi jirani ya Malawi. Hata hivyo, fukwe za miji yenye kupokea wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani ni Mbamba Bay, Kilosa, Liuli, Lundu na ufukwe wa Mhalo ambao ni miongoni mwa maajabu yaliyopo katika Wilaya ya Nyasa.

Kwa upande wa pili wa Ziwa Nyasa, hasa katika Wilaya ya Kyela, utalii wa fukwe umeshika kasi kwa muda mrefu kutokana na kuwepo kwa Ufukwe maarufu wa Matema. Matema ni eneo tulivu lenye mandhali ya mimea ya rangi ya kijani kibichi likiwa limepambwa na Safu za Milima ya Livingstone yenye urefu wa mita 3,000 na kusheheni misitu ambamo hupatikana ndege wazuri wa angani.

Kwa Wilaya ya Nyasa, miongoni mwa mambo yanayoipatia sifa wilaya hii ni hifadhi za asili, ambapo hifadhi ya wanyamapori ya pili ya asili katika Mkoa wa Ruvuma inaitwa ‘Mbamba Bay Hill’ iliyopo katika Mji wa Mbamba Bay, makao makuu ya Wilaya ya Nyasa. Hifadhi ya Mbamba Bay Hill ina eneo la hifadhi lenye ukubwa wa ekari 420. Ndani ya hifadhi hiyo kuna wanyama kama nyani, nyoka, pimbi, chui na ndege wa aina mbalimbali.

Kulikuwa na mpango wa kuongeza wanyama kama swala, fisimaji, mbuzi mawe, digidigi na mbawala, hasa baada ya ujenzi wa uzio kukamilika. Hii ni kwa mujibu wa Ofisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Challe. Ndani ya Ziwa Nyasa kuna visiwa kadhaa vyenye mazingira mazuri ya utalii, mojawapo kikiwa Kisiwa cha Lundo kilichopo katika Kata ya Lipingo na Tarafa ya Ruhekei wilayani Nyasa.

Kisiwa hiki kina jumla ya ekari 20 na kimepewa jina la Lundo kwa sababu watu wa kwanza waliovuka kisiwa hicho kwenda ng’ambo ya pili walifikia kijiji cha Lundo. Taarifa za Ofisi ya Maliasili ya Mkoa wa Ruvuma zinaonesha kuwa, kisiwa hiki tangu zamani kilikuwa na manufaa makubwa kwa wanavijiji vya Lundo, Ngindo na Chinula kwa sababu wakati wa Vita vya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907, watu walikuwa wanakimbilia katika kisiwa hicho ambacho kina maeneo ya maficho.

Baada ya Vita ya Majimaji kuanzia mwaka 1908, kisiwa hiki kilitumiwa na wakoloni wa Kijerumani kuwahifadhi watu waliopata ulemavu kutokana na ugonjwa wa ukoma, ambao baada ya uhuru walihamishiwa katika makazi ya Ngehe wilayani Nyasa. Baadaye, serikali ilipendekeza kuwa Visiwa vya Lundo na Mbamba Bay kuwa hifadhi za wanyamapori, vikiwa ni hifadhi ya pekee ya wanyamapori pamoja na samaki wa mapambo wanaozaliana katika visiwa hivyo ndani ya Ziwa Nyasa.

Ndani ya Ziwa Nyasa, kuna Kisiwa cha Pomonda, katika eneo la Liuli. Liuli ni miongoni mwa miji muhimu katika Wilaya ya Nyasa. Mji huu unayo bandari muhimu inayotumiwa na meli zinazofanya safari katika Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania. Katika rekodi za kihistoria, kuna mengi ya kukumbukwa katika mji wa Liuli, lakini jambo muhimu ni kuwepo kwa Kisiwa cha Pomonda ambacho kimejaa historia kutokana na jiwe kubwa la Pomonda lenye pango liliweza kuhifadhi watu zaidi ya 200 waliokimbia kujificha wakati wa Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia.

Ni historia nzuri na tamu kwa wakazi wa Nyasa na vitongoji vyake, kwani jiwe hilo lipo karibu kabisa na Bandari ya Liuli ambapo kila abiria au msafiri yeyote anapotumia bandari hiyo ataweza kuliona. Jiwe hili ni moja ya vivutio vya utalii katika mji wa Liuli. Kutoka eneo la ufukwe mpaka kulifikia jiwe la Pomonda, kuna umbali wa kilometa moja na robo.

Pango lililomo ndani ya jiwe hili la Pomonda limezungukwa na miti ya asili ambayo unene wake hauzidi robo mita na umri wa miti hiyo ni takriban miaka 100. Pango hili la Pomonda limezungukwa na mawe yenye umbo la mafiga matatu, kuzunguka eneo hilo mpaka kulimaliza unachukua muda wa saa moja. Taarifa kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa zinaeleza kwamba, kwa miaka ya karibuni watalii wengi wamekuwa wakifika katika fukwe mbalimbali kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa, hali inayoongeza pato la taifa.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu mstaafu wa Hesabu za Serikali (CAG), ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi