loader
Picha

Nungwi Mnarani na harakati za maendeleo ya utunzaji kasa

KASA ni miongoni mwa viumbe wa baharini walio hatarini kutoweka kutokana na kupungua kwa idadi yao duniani kote. Vyanzo mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamii vinabainisha kuwa, kasa ni miongoni mwa viumbe walio katika kundi la reptilia.

Kwamba, kasa mkubwa anakuwa na kilo hadi 600, urefu wa hadi futi 5.25 na anaweza kuishi hadi miaka 150. Kasa huanza kutaga mayai anapofikisha umri wa miaka 25. Chakula cha kasa ni wadudu, samaki, uyoga, mwani na majani ya baharini.

Kihistoria inaelezwa kuwa, viumbe hawa wanaotembea umbali mrefu kutafuta makazi na chakula, kwa mara ya kwanza walionekana duniani miaka milioni 200 iliyopita. Kwa mujibu wa wanasayansi mbalimbali, kuna spishi saba za kasa wa baharini na wanaoishi hadi sasa ni Kasa Kasa, Kasa Mtumbi, Kasa Ng’amba, Kasa Duvi, Kasa Ngozi, Kasa Bapa na Kasa Kemp Ridley.

Sheria za Utunzaji wa Viumbe Wanaoishi Baharini Namba 9, Kifungu cha 12 inayohusu utunzaji wa mazingira ya baharini, inasema iwapo mwananchi atahusika na uharibifu wa viumbe walio hatarini kutoweka atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu hadi minne.

Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Zanzibar inayoshughulikia masuala ya uvuvi na mazingira yake katika kuhakikisha ustawi wa jamii na mazingira ya baharini, imekuwa ikijizatiti kuhakikisha rasilimali hizo na nyingine mbalimbali za baharini zinatunzwa na kulindwa ipasavyo kwa maslahi ya taifa. Inaelezwa kuwa, shughuli mbalimbali zikiwamo ujenzi wa hoteli za kitalii unatakiwa ufanyike umbali wa mita 30 kutoka ufukweni mwa bahari. Hatua hiyo kwa kiasi kikubwa huleta faraja kwa kasa ya kuja ufukweni kutaga na baadaye kurejea baharini.

Chanzo kimoja: “Kasa hawezi kuja kutaga nchi kavu kama kutakuwa na vishindo vingi vya watu kwa kuhofia usalama wake wa kuweza kukamatwa, kwa sababu anapokuwa ufukweni hana kasi ya mwendo wa kukimbia.”

Kichocheo kingine cha tishio la kutoweka kwa kasa, ni uvuvi haramu unaofanywa baharini na hivyo, kila mmoja kuwa na wajibu mkubwa kuuzia sambamba na kuepuka uharibifu wa mazingira yakiwamo ya fukwe za bahari. Mkurugenzi Idara ya Maendeleo na Uvuvi, Mussa Aboud Jumbe anasema kutokana na idadi sambamba na umuhimu wake, kasa ni wanyama wasiopaswa kuvuliwa kwani wana umuhimu mkubwa katika ikolojia ya bahari.

Mkurugenzi huyo anasema ili jamii itoe mchango wake katika utunzaji wa mazingira hasa ya baharini iko haja ya kuchukua jitihada na kufuata maelekezo wanayopewa na Idara ya Uvuvi ikiwemo kupewa elimu kuhusu wanyama sambamba na hasa kuzingatia usafi wa mazingira wa maeneo husika. Anasema faida ya wanyama hao inajulikana na kuthaminiwa siyo tu na Tanzania pekee, bali dunia nzima.

Kwa msingi huo anasema: “Ili kuhakikisha kuwa kasa wanalindwa, yeyote anayebainika kuchafua mazingira ya wanyama hao, anachukuliwa hatua kali za kisheria ili liwe fundisho kwa wengine…” Ushirika wa ufugaji wa kasa wa Nungwi Mnarani Aquarium uliopo Mkoa wa Kaskazini ‘A’ Unguja umekuwa ukijishughulisha na utunzaji wa mazingira ya viumbe wa baharini kama vile kasa, samaki na maisha yao kwa jumla kwa kutoa elimu kwa jamii mintarafu utunzaji ndani na nje ya nchi.

Ofisa Ushauri wa Aquarium Nungwi, Maulid Machano Adibu anasema juhudi za kuelimisha jamii zinazofanywa na ushirika huo, zinatoa mchango mkubwa kuwaenzi wanyama na hivyo, kuchangia kuzuia uharibifu unaofanywa na baadhi ya watu dhidi ya viumbe wengine.

Adibu anasema ushirika huo unaojumuisha watu 12 umeanza tangu mwaka 1993 na umeleta mafanikio makubwa kwa jamii ya Kijiji cha Nungwi na serikali kwa jumla hususan katika sekta ya utalii na taifa kwa hali iliyofanya wapige hatua katika harakati zao kimaisha. Anayataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kupata faida ya kuingiza fedha za kigeni kwa watalii wanaoingia katika eneo hilo kama wageni, kupata maji safi hali inayowapa faraja wanakijiji hao na kuyatumia kwa shughuli mbalimbali zikiwamo za mapishi, kufulia, kuogea na kumwagilia mashamba yao.

Ushirika huo pia umesaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa wanakijiji cha Nungwi kutokana na fursa mbalimbali zinazojitokeza hali inayowawezesha familia zao kujikimu kiuchumi. Kwa sasa Ushirika wa Uhifadhi kasa wa Nungwi unafanya kazi na jitihada mbalimbali kutunza mazingira ya kasa na kuweza kujiajiri wenyewe hasa vijana. Kwa sasa kasa wapatao 300 wanatunzwa hapo.

Kwa mujibu wa Adibu, kupitia Ushirika wa Aquariam wamejenga shule ya msingi hali iliyowaondolea usumbufu wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani na kurahisisha uapatikanaji wa elimu kwa vijana wao. Anasema hali hiyo imekuwa chachu ya kuendeleza kutoa elimu kupitia Idara ya Uvuvi kuhusu utunzaji wa mazingira na kuwarithisha vijana elimu na ari ya utunzaji kasa na mazingira ya baharini ili rasilimali na vivutio hivyo vya utalii viwe endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Katibu wa Jumuiya ya Uhifadhi Mazingira ya Nungwi Aquarium, Pondo Ali Hamadi anaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Tanzania kwa jumla kwa kuwakubali na kuwapa ushirikiano wa dhati, hali inayowafanya wapige hatua kimaendeleo na kutambulika ndani na nje ya nchi kwa kupokea idadi ya wageni wasiopungua 1,000 kila mwaka katika eneo la Aquariam Nungwi.

Anawataka wananchi kuwa na nia na utayari wa kuzipenda rasilimali na bidhaa za Tanzania na pia, kukubali na kuwa tayari kujifunza namna bora zaidi ya kuziendeleza kama urithi kwa vizazi vijavyo. Anawahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ambayo kasa wataachiwa kurudi katika maisha yao ya baharini kama ilivyo ada kila ifikapo Julai 20 wanapoachiwa na kurudishwa baharini.

Anasema jamii na serikali waunganishe nguvu kuona na kutambua ukweli kuwa, kukosekana kwa viumbe hao ni kama janga la taifa hivyo, washirikiane kwa dhati kutoa na kupokea elimu kuhusu uhifadhi bora wa kasa na viumbe wengine wa baharini sambamba utunzaji wa mazingira kwa jumla. “Kuna umuhimu mkubwa watu kushirikiana zaidi na Idara ya uvuvi kutunza mazingira ya baharini na viumbe wa baharini wakiwemo kasa na mazalio yao na pia, kuendelea kufuata sheria na taratibu zilizowekwa…. Ikumbukwe kuwa, ni marufuku kuvuliwa kasa kwani ni viumbe adimu na wa thamani kwa uwepo wao,” anasema.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu mstaafu wa Hesabu za Serikali (CAG), ...

foto
Mwandishi: Skina Ali

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi