loader
Picha

Naibu waziri ataka mimba za wanafunzi kudhibitiwa

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha ametaka uongozi wa Mkoa wa Morogoro kuchukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na wadau wengine ili kudhibiti mimba za wanafunzi.

Waziri huyo ametoa kauli hiyo baada ya kupatiwa taarifa kuwa katika mkoa huo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wapatao 567 wamepata mimba katika mwaka 2017/2018. Naibu Waziri alisema hayo juzi wakati akizungumza na watendaji wa mkoa wa Morogoro mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya elimu iliyosomwa na Ofisa elimu mkoa Joyce Baravuga .

Licha ya kuchukua hatua hizo, pia ameutaka mkoa huo uhakikishe wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanapata fursa kujiunga kidato cha kwanza ili wanufaike na mpango wa serikali wa elimu bure . Akizungumzia zaidi suala la mimba kwa wanafunzi aliutaka uongozi huo kuendelea kuweka mkazo zaidi katika kuzuia kwa kuanzisha masuala ya kutolewa ushauri nasaha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Suala hili la mimba kwa wanafunzi endeleni kuweka mkazo zaidi katika kuzuia kwa kuanzisha masuala ya ushauri nasaha ambapo nchi nyingi zinafanya jambo hili na limeleta mafanikio,” alisema. Kwa upande wake, Ofisa elimu mkoa Baravuga katika taarifa yake alisema mimba za utotoni mwaka 2017/2018 kati ya wanafunzi 567 waliopata ujauzito,111 ni wa shule za msingi na 456 ni wa shule za sekondari .

Alisema mimba kwa wanafunzi zinachangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo kucheza ngoma za “ Kigodoro” , kukosekana kwa hosteli shuleni na hivyo watoto wa kike kupata vishawishi kutoka kwa waendesha bodaboda kwa kuwahadaa. Hata hivyo alisema hatua mbalimbali zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi wa kike na wa kiume wa shule za msingi na sekondari kuhusiana na madhara ya mimba za utotoni na kwa wanafunzi.

Baravuga pia alitaja hatua nyingine ni kuwapima ujauzito wanafunzi wenye umri mkubwa pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote wanaowapa ujauzito wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Katika hatua nyingine alisema wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani wasichana ni 19,355 na wavulana 17,756 sawa na asilimia 77.38 ya watahiniwa 48,351 waliofanya mtihani. Alieleza kuwa ufaulu huo ni wa kuridhishwa kwa kupanda kwa asilimia 6.6 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2017 ambayo ufaulu wake ulikuwa asilimia 70. 78.

ZIKIWA zimesalia siku chache kwa Wizara ya Nishati kuwasilisha bungeni ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi