loader
Picha

‘Fuateni ushauri wa daktari matumizi ya dawa’

JAMII imetakiwa kuzingatia matumizi ya dawa kwa kufuata ushauri wa madaktari kwani baadhi ya dawa zinaweza kumsababishia mtu ulemavu na nyingine kumfanya mjamzito kujifungua mtoto mwenye ulemavu.

Aidha, imeonywa pia kutotumia dawa kwa kufuata taarifa za kwenye mitandao bila kumuona daktari na kupata ushauri na dawa sahihi kulingana na tatizo alilonalo. Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Walemavu yaliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana.

Mkuu wa Idara ya Famasia katika Hospitali hiyo, Deus Buma alisema dawa kama Thalidomide akiitumia mwanamke mwenye ujauzito anajifungua mtoto ambaye hana mikono.

“Kuna wanaoingia kwenye mitandao hii ya kijamii wakidhani ni suluhisho la matatizo yao kumbe kuna taarifa nyingine hazijachujwa, kuna dawa ambazo zina madhara makubwa na zinaweza kusababisha ulemavu,” alisema.

Dk Buma alisema dawa kama hiyo ya Thalidomine ilikuwa kwa ajili ya kuzuia kichefuchefu lakini baadaye iliondolewa, hata hivyo ilirudishwa tena kwenye matumizi baada ya kubainika kuwa ni tiba ya saratani ya damu, hata hivyo haitakiwi kutumiwa na mjamzito.

“Yaani akiitumia tu mwanamke mwenye ujauzito atajifungua mtoto hana mikono kabisa na hii si utani, kwa hiyo dawa hizi ni vizuri zitumike kwa kufuata maelekezo ya wataalamu na si mtu kujikusanyia taarifa kwenye mitandao,” alisema Dk Buma na kuongeza kuwa dawa nyingine zinaweza kusababisha magonjwa ya ngozi au matatizo ya macho na hivyo kuingia katika ulemavu.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Ndani, Dk John Rwegasha aliitaka jamii kuwashirikisha wenye ulemavu katika mambo ya kijamii na si kuwatenga. Pia alisema hospitali hiyo inajitahidi kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu katika huduma za matibabu, kutoa ajira na kutoa tiba kwa vitendo kama vile kuwa na wataalamu wa sauti na mafiziotherapia.

Naye mgeni rasmi katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Compass inayoshughulika na mambo ya habari, Maria Sarungi alisema ili kuwasaidia watu wenye ulemavu ni kuwashirikisha na kuwapa msaada ili waweze kusimama wenyewe na kwamba ulemavu ni jambo ambalo linaweza kumpata mtu yeyote. Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Kuwajengea uwezo, kuwahusisha na kuwapatia haki sawa watu wenye ulemavu’.

WABEBA nyama kwenye machinjio na mabucha watachukuliwa hatua za kisheria ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi