loader
Picha

Uhuru ni Kazi

LEO Watanzania tunaadhimisha miaka 57 tangu Tanganyika ilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni, Desemba 9, 1961.

Uhuru tunaosherehekea leo ni baada ya kazi kubwa aliyoifanya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere.

Tuna kila haki kufarahia uhuru wetu, umoja wetu lakini zaidi amani ambayo tangu wakati huo, nchi hii ilivyojengewa misingi imara ya upendo, amani na uzalendo, vitu ambavyo ni tunu na bora tukaendelea kuvienzi kwani vimetujengea sifa kubwa si tu bara la Afrika bali pia hata duniani kwa ujumla.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli tangu iingie madarakani katika kipindi cha miaka mitatu imefanya sherehe za uhuru mara moja, tena kwa mara ya kwanza zilifanyika Makao Makuu Dodoma mwaka jana.

Mwaka juzi, Rais Magufuli aliamua siku hiyo itumike kufanya usafi na fedha zilizokuwa zimetengwa zilipanua Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kipande cha kutoka Morocco hadi Mwenge.

Mwaka huu, fedha za uhuru zitajenga hospitali kubwa mkoani Dodoma itakayojulikana kama Hospitali ya Uhuru ili isaidiane na ile ya Benjamin Mkapa na hospitali ya mkoa.

Rais anafanya yote haya kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wa leo na haya yataendelea kuwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Ikumbukwe kwamba wakati ule wa kupata uhuru, Mwalimu Nyerere aliwasisitiza Watanzania kuzingatia kuwa, kupata uhuru siyo suala la kumiliki kitu na kukiweka mezani kama pambo, bali uhuru una masharti yake likiwamo moja la kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Hayo ndiyo maarifa anayoyatumia Rais wa sasa, Dk John Magufuli kwani kufanya usafi nchi nzima na fedha zile kufanya jambo ambalo litasimama miaka na miaka, si tu vinaiwekea historia serikali ya awamu hii, bali pia vinaonesha dhamira thabiti na nia njema ya serikali ya kuwakomboa wanyonge.

Ndio maana Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba bila kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kutumia nyenzo za watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora; uhuru mnaokuwa nao ni bure.

Watanzania tusherehekee siku hii kwa kutokwenda majukwaani, lakini pia tuweke akilini kwamba serikali hii inahubiri Uhuru ni Kazi. Tukatae uvivu na uzembe. Tukatae rushwa na ufisadi. Tuepuke ukabila na upendeleo.

Tujiepushe na ngono zembe ili kulinda afya zetu zisiathirike na ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Tuwajali wazee na kuwalea watoto wetu wawe na nidhamu kwa ajili ya kuilinda nchi yetu isijetekwa na wadhalimu kupitia vizazi ambavyo hatukiviandaa vyema.

Tutumie rasilimali zetu kwa uangalifu na kuepuka siasa za uchochezi.

Tunasema siasa nzuri kwa kuwa hata Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba ili tuwe na maendeleo ya kweli ni lazima tuwe na watu, siasa safi na viongozi bora.

Watu wapo ndio sisi Watanzania, viongozi bora wapo na sisi tu mashahidi wa hili, sasa tunahitaji siasa safi isiyoyumbisha watu wakiwemo wanasiasa ambao badala ya kujadili hoja za nguvu, wanajadili nguvu za hoja zenye mitizamo hasi.

Hivyo, Watanzania tumuunge mkono Rais Magufuli tuweze kuijenga nchi yetu kwa pamoja. Uhuru ni kazi!

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, umekuwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi