loader
Picha

Matendo yanayoweza kusababisha upigwe radi

HIKI ni kipindi cha mvua katika maeneo mbalimbali nchini. Wakati mvua ikiwa neema kutokana na kustawisha mazao na kuleta maji, lakini upo wakati hugeuka majanga kutokana na kuambatana na mambo hatarishi kwa maisha ya watu, wanyama na mime.

Wiki iliyopita, jarida hili liliandika kuhusu mvua ya mawe hususani visababishi na ishara zake. Ikaelezwa kuwa mvua ya mawe ni mvua ambayo matone ya maji yanapofika kwenye ardhi huwa na umbo la vipande vya barafu.

Kitaalamu, mvua hii hutokea wakati matone ya maji ya mvua yanapita kwenye hewa baridi na kuganda hadi kuwa barafu. Mvua ya mawe ambayo mara nyingi huambatana na upepo mkali, imekuwa ikisababisha majanga katika maeneo mbalimbali na hivyo kuacha historia ya machozi.

Miongoni mwa majanga ni pamoja na kusababisha vifo kwa watu, wanyama na uharibifu wa majengo na vitu mbalimbali. Ikaelezwa kuwa watabiri wa hali ya hewa wana uwezo wa kutabiri ni lini mvua ya mawe inaweza kutokea.

Inawezekana kubaini aina ya mvua itakayonyesha. Mawingu meusi, mvua, mngurumo na mwanga mkali ni miongoni mwa ishara kwamba mvua inaweza kuwa ya mawe. Jarida hili lilionesha maeneo mbalimbali duniani ambako mvua ya mawe imekuwa ikinyesha au iliwahi kunyesha na kusababisha maafa makubwa. Miongoni mwa maeneo ni pamoja na kijiji cha Mwakata wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga. Mvua hiyo iliyonyesha Machi, 2015, ilisababisha vifo vya watu wapatao 40 na wengine 90 kujeruhiwa. Ilisababisha nyumba 160 kuanguka na nyingine kuezuliwa na upepo mkali. Watu wapatao 900 walikosa makazi.

Taarifa zilionesha kuwa watu wengi walifariki kutokana na kuangukiwa na kuta za nyumba na wengine kuangukiwa na mawe makubwa ya barafu baada ya mapaa kutobolewa. Inadaiwa mawe hayo yalikuwa na ukubwa wa ndoo ya lita 10 na yalizagaa katika kijiji hicho kabla ya kuyeyuka. Aidha, hivi karibuni, imeripotiwa mvua ya mawe mkoani Rukwa ambayo imesababisha vifo na uharibifu wa nyumba 336 katika vijiji vya Kipeta na Kilyamatundu katika kata ya Kipeta wilayani Sumbawanga. Mvua hiyo iliyoambatana na upepo ilisababisha vifo vya watu wawili. Mvua ya mawe hutokea sehemu za chini za mawingu ya mvua ya radi.

Sehemu hizo hupatikana katika hali baridi chini ya sentigredi sifuri. Yakigusana na matone mengine, huganda mara moja. Inaelezwa kwamba, mara nyingi vipande vidogo vya barafu vinavyotokea huanza kuanguka. Hata hivyo, wataalamu wanaonesha kwamba mara nyingi ipo hewa ya kuzunguka ndani ya mawingu ya mvua ya radi na hivyo vipande vidogo vya barafu vinaweza kurushwa juu.

Katika mwenendo huu, hugusana na matone mengine ya maji baridi sana yanayoganda mara moja wakati wa kuguswa na hivyo kukuza kipande cha barafu. Kipande cha barafu huinuliwa na upepo wa kupaa hadi kufikia uzito wa kutosha au nguvu ya upepo wa kwenda juu inafifia na ndipo huanza kuanguka. Inaelezwa kwamba, endapo masi ya barafu inatosha haiwezi kuyeyuka wakati wa kupita kwenye hewa yenye joto juu ya sifuri, hivyo hufika ardhini kama mvua ya mawe. Vipande vya barafu vinaweza kusababisha uharibifu hata kuua watu na mifugo.

Uharibifu hutegemea na uzito wake. Radi ni tukio lingine la asili liambatanalo na mvua ambalo pia ni hatari kwa maisha ya viumbe hai kwa maana ya kusababisha vifo kwa watu, wanyama na mimea. Pia huharibu miundombinu. Radi hutokana na kuachiliwa kwa umeme tuli, tukio ambalo hutokea kutokana na tofauti ya nguvu za umeme kati ya mawingu na ardhi.

Hizi ni cheche kubwa za umeme kutoka angani, ambazo huwa na nguvu . Radi inaweza kuunguza viungo muhimu mwilini na kusababisha kifo. Inaelezwa kuwa zaidi ya robo tatu ya wanaonusurika baada ya kupigwa na radi hupata ulemavu wa kudumu. Kitaalamu, radi hutokea kwenye sehemu ya chini ya anga na huenea kutoka wingu moja hadi jingine au kutoka kwenye wingu hadi ardhini. Radi inaweza kupiga mtu katika namna tofauti ikiwamo inayopiga moja kwa moja. Radi hii hupiga na nguvu za umeme kupitia ndani ya mwili hadi ardhini.

Nyingine ni kupigwa pembeni ambako kitu kilicho karibu kinaweza kupigwa radi na nguvu zikaruka na kumfikia mwingine. Radi nyingine ni ile inayopiga ardhini na kisha kumfikia mtu yeyote. Wataalamu wanashauri njia za kujikinga na radi ni pamoja na kutafuta hifadhi kwenye nyumba kubwa hususani yenye kifaa cha kujikinga dhidi ya radi au ndani ya gari, utakuwa salama.

Inashauriwa pia kuepuka maeneo ya wazi au kwenye mlima ulio wazi. Ikitokea ukakosa mahali pa kujihifadhi, ni vyema kujikunyata, kuchutama, kuweka mikono kwenye magoti na kuficha kichwa. Wataalamu wanahadharisha kuwa kujikinga mvua chini ya miti ni hatari kwa ni rahisi kupigwa radi. Vile vile inapaswa kukwepa maeneo yenye maji ikiwa ni pamoja na ufukweni. Kuwa karibu na maji huongeza hatari ya mtu kupigwa na radi . Kwa kuwa radi ni nguvu ya umeme, ushauri mwingine ni kuhusu kujiepusha na vitu vya chuma na vyenye ncha kali wakati wa mvua; miongoni mwake ni miavuli.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi