loader
Picha

Rubani kijana Mtanzania anayeishusha Airbus Dar

“NAITWA Simon Myagila nina miaka 26, ni Mtanzania na kwa asili mimi natoka Mkoa wa Morogoro, mimi ni Mpogoro.” Ndivyo alivyoanza kujitambulisha kwangu, rubani kijana kabisa katika Kampuni ya Ndege la Tanzania (ATCL) ambaye anatarajia kuwa miongoni mwa marubani wa ndege mpya za Airbus A220-300 nchini.

Pamoja na kurusha ndege hizo, pia atakuwa miongoni mwa marubani watakaorusha mbawa hizo za Mlima Kilimanjaro kutoka nchini Canada hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ambako leo Jumapili ‘dege’ hilo linatua katika ardhi ya Tanzania.

Nilipata hamu ya kuzungumza naye kwa njia ya mtandao wa kompyuta baada ya kupata bahati tu ya kukutana naye ‘online’ akiwa katika mafunzo yake nchini Canada ya kuvurumusha ndege hizo mpya ambazo tutakuwa wa kwanza katika Bara la Afrika kuwa nazo na kuzitumia.

“Najua hatuzungumzii ukabila, tunajivunia utanzania wetu, lakini kwa asili kabila langu mimi ni Mpogoro,” anasema rubani huyo wa ATCL, wakati tukihojiana kuhusu wapi anatoka hapa nchini, huku akiongeza kuwa alianza kazi hapo kwa kurusha ndege aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba idadi ya watu mpaka 76.

Katika mazungumzo yetu, alisema alianza safari yake ya urubani mwishoni mwa mwaka 2014 baada ya kuhitimu Kidato cha Sita. Kwa wakati huo, alifanikiwa kupata chuo katika Jimbo la Florida nchini Marekani ambako alianzia leseni ya mwanzo ya urubani ya PPL baadaye IR pamoja na CPL, na kuhitimu.

Alirejea nyumbani Mei mwaka 2016, na mwaka mmoja baadaye, Mei mwaka 2017 alipata nafasi ATCL na kuwa miongoni mwa marubani wanne waliochaguliwa kwenda Toronto kwa masomo ya kurusha Bombardier Q400, ndege mpya za kwanza zilizonunuliwa na Serikali ya Rais John Magufuli.

Mafunzo hayo ya mwezi mmoja yalimpa uwezo wa kurusha ndege hizo hapa nchini na hivyo kuwa miongoni mwa marubani wanaoziwezesha kuwa angani ndege hizo nchini. Agosti mwaka huu, alifanikiwa tena kupata nafasi ya kwenda mafunzoni kwa ajiri ya ndege mpya kabisa na ya kisasa ambayo ni ya kwanza Afrika nzima ya Airbus A220-300.

Anasema anaona fahari kulitumikia taifa na hasa namna ambavyo nchi inajizatiti kuinua utalii kupitia kuwa na shirika la kisasa la ndege ili kuwapeleka watu maeneo mbalimbali yenye vivutio kwa kasi.

Pamoja na fahari hiyo, anaionea fahari Tanzania kwa kuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kumiliki ndege hizo za kisasa ambazo anaamini kwamba itakuwa zawadi nzuri ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa wananchi wa Tanzania kutoka kwa serikali inayowajali.

Akiwa amefanikiwa vyema katika mafunzo hayo na kupewa kibali, anasema Watanzania wana nafasi nzuri zaidi ya kupiga hatua za maendeleo hasa kutokana na mikakati ya serikali ya kuhuisha na kuboresha maeneo mbalimbali ya mapato kwa lengo la kuwa na uwezo thabiti wa kuisaidia jamii ya Watanzania.

Anasema katika mazungumzo kwamba kila mmoja ana wajibu wa kujituma kuitumikia nchi ili isonge mbele katika kuboresha hali ya ustawi wa ndani na nje. Kujituma huko ni pamoja na kuhakikisha kwamba mtu anapoenda kujifunza, anajifunza kwa bidii na kuurejesha utaalamu wake nyumbani.

“Nashukuru Mungu masomo yalikwenda vizuri na nikafaulu vizuri mno na kuweka historia ya kuwa mmoja wa Waafrika wa kwanza kufuzu mafunzo na kuwa endorsed (kupewa kibali) cha kurusha ndege hizo mpya za kisasa, aina ya Airbus A220,” anasema Myagila.

Akizungumzia historia yake, anasema alizaliwa jijini Arusha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mount Meru, Aprili 12, 1992 kutoka kwa baba Josephat Myagila na mama Verediana Sokole. Wakati mama yake ni mfanyabiashara, baba yeye ni mwajiriwa ingawa anajishughulisha na biashara.

Akiwa mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto wanne, alianza shule ya msingi mwaka 2001 katika Shule ya serikali ya Levolosi iliyopo jijini Arusha. Mwaka 2008, aliingia Shule ya Sekondari ya serikali ya Kaloleni jijini humo na kumaliza kwa kishindo mwaka 2011 kwa ufalu wa Agosti mwaka huu, alifanikiwa tena kupata nafasi ya kwenda mafunzoni kwa ajiri ya ndege mpya kabisa na ya kisasa ambayo ni ya kwanza Afrika nzima ya Airbus A220-300. daraja la kwanza.

Alijiunga na Kidato cha Tano shule binafsi ya Edmund Rice ya Arusha na kuhitimu Mei 2014. Hakukaa sana kwani wazazi wake walijinyima na kumtafutia chuo cha mafunzo ya urubani jijini Florida nchini Marekani ambako alianza Novemba 2014 na kumaliza Aprili, 2016.

Rubani kijana huyo ambaye hajaoa japo ana mchumba, anapenda sana maisha ya angani ingawa pia ardhini ana shughuli nyignine za kibiashara.

Pamoja na kufurahishwa kuwa angani, rubani huyo anasema kama zilivyo kazi nyingine, urubani pia una changamoto na kubwa zaidi ni hali ya hewa.

“Hali ya hewa inaaffect (inaathiri) kazi yetu kwa kiwango kikubwa, mfano mvua zinapokua kubwa mbali na kuharibu miundombinu yetu ya uwanjani, bali pia hutuwia vigumu kurusha na kutua ndege katika eneo husika,” alisema Myagila na kuongeza pia tatizo la upepo hasa unapokuwa mkali.

“Upepo unapokuwa mkali husababisha zoezi na kuruka na kutua kuwa mtihani hasa kutua, ukungu nao husababisha kushindwa kuona mbele wakati wa kuruka na kutua na hivyo mtu kuhitajika kutumia akili za ziada kuhakikisha kwamba hakuna madhara kwa watu wala kwa chombo husika,” alifafanua.

Akizungumzia furaha yake anapokuwa angani alisema, “Ninapokuwa angani kitu kinachonifurahisha sana ni mandhari kwa ujumla. Unakutana na mawingu yaliyokaa katika shepu mbalimbali na wakati wa kutua unaona jinsi miji ilivyo katika mpangilio.” Anapokuwa nyumbani, anaporuka anasema anafurahishwa sana na mandhari ya Dar es Salaam, Mwanza hasa ziwa Victoria, mkoani Kilimanjaro anapata fursa ya kuona jinsi milima ilivyojipanga hasa milima Kilimanjaro na Meru.

Akizungumzia matarajio yake ya baadaye, Myagila anasema: “Matarajio yangu ni kuendelea kufanya kazi na Air Tanzania kwa muda mrefu zaidi kwa sababu kampuni sasa inakua kwa kasi na mimi ningependa kukua nayo na kuwa miongoni kwa watu wanaokuza shirika letu la Taifa.” Ndege aina ya Airbus A220 ambayo moja inatua leo na nyingine itakuja baadaye, zina uwezo mkubwa hasa teknolojia yake ya kisasa inayofanya kuwa salama zaidi katika mazingira ya Afrika na kwingineko.

Ndege hii aina ya A220 inatengenezwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Airbus na Bombardier. Watu wa Airbus katika ushirikiano huu wamewezesha ndege za awali za Bombardier za mfumo wa jeti ambazo awali zilikusudiwa kuwa C Series kufanywa kuwa ndege za kibiashara.

Ndege hizi ambazo huchukua abiria kati ya 100 na 150, zimekuwa na mahitaji makubwa katika soko la dunia hasa kutokana na uwezo wake mkubwa katika teknolojia na madhara madogo zaidi kulinganisha na ndege zingine.

Ndege hizi za A220 zimetengenezwa katika hali ya kisasa zaidi na zinaendeshwa na injini mbili za Pratt & Whitney Pure- Power PW1500G zikiwa na matumizi asilimia 20 chini kuliko ndege nyingine Airbus A220 ambayo awali ilikuwa inajulikana kama Bombardier CSeries au C Series ni ndege yenye muundo mwembamba na injini mbili ikiwa na uwezo wa kutoa huduma kwa umbali wa wastani kwa kilometa 5020, ikifanyiwa mauzo na Airbus, lakini ikiwa imebuniwa na kutengenezwa Canada na Kampuni ya Bombardier Aerospace. Kutokana na ushirikiano uliopo na Airbus, ndege hizi zinatengenezwa na CSeries Aircraft Limited Partnership (CSALP).

Imeelezwa katika taarifa mbalimbali kwamba CSeries zimetengenezwa kwa asilimia 70 na malighafi za kisasa asilimia 46 zikiwa ni composite materials huku asilimia 24 ikiwa ni aluminium- lithium. Bombardier wanasema kuna manufaa makubwa katika kuwa na ndege hizo kwa kuwa zinapunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia 25 huku zikipunguza kelele za sauti mara nne zaidi ya ndege zilizopo sasa.

Aidha, zinatumia chini ya asilimia 20 ya mafuta yanayotumika na utoaji wa hewa ukaa. Bombardier injini zake na mabawa yalivyotengenezwa yanasaidia kuokoa asilimia 20 ya mafuta ukilinganisha na Airbus A320 na Boeing 737NG.

Wakati wa makabidhiano ya ndege Airbus A220 Ijumaa huko Mirabel, Canada, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Tito Kasambala alisema ndege hizo zenye uwezo mkubwa wa kiutendaji na zilizotengenezwa kumfanya msafiri wa anga kujisikia burudani, zitasaidia sana kuimarisha usafiri wa anga nchini na nchi jirani na kufungua njia kwenda masafa ya mbali zaidi kama India na Mashariki ya Kati.

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Nyantore iliyopo Kijiji cha ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi