loader
Picha

Karibu Airbus A220-300, tunajivunia kuwemo rubani Mtanzania

WAKATI tuna furaha ya kuilaki ndege mpya za Airbus A220- 300 inayotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam leo, pia tuna kila sababu kukiombea Chuo cha Taifa cha Usafi rishaji (NIT) kifanikiwe kutimiza azma yake ya kuanzisha kozi mpya ya mafunzo ya urubani na uhandisi wa ndege, ili kutoa fursa kwa vijana kujifunza fani hiyo ndani ya nchi.

Azma hiyo imelenga kwa mara ya kwanza kuiwezesha nchi iweze kuondokana na tatizo la muda mrefu ambapo vijana wenye uhitaji wa kuwa marubani wanalazimika kwenda nje ya nchi. Mbali na kuwa na uhaba wa marubani hapa nchini huku serikali ikiongeza kasi ya kuongeza ndege, imekuwa ni gharama kubwa kusomea taaluma hiyo adimu.

Tukiwa na mategemeo makubwa kwamba azma ya NIT itatimia ili kuziba pengo kubwa ambalo limekuwapo kwa muda mrefu, tuna kila sababu kuwapongeza marubani wazalendo wachache ambao tayari tunao hapa nchini.

Tunajivunia hao wachache akiwamo rubani Simon Myagila, kijana wa miaka 26, Mtanzania ambaye ni miongoni mwa marubani waliomo kwenye ndege hiyo.

Katika makala iliyomo kwenye gazeti hili leo ambayo inamwelezea kijana huyu, njia yake ya mafanikio ya kufikia hatua hii, inaonesha wazi kuwa, vijana wengi ambao wanatamani kuwa marubani kama yeye, hakika wanaweza kuona ugumu wake.

Hii inatokana na ukweli ulio wazi kwamba ili wafikie hatua hii, lazima ama wazazi au walezi wafunge mkanda kweli kweli waweze kupata vyuo nje ya nchi ili ndoto za watoto wao zitimie. Tujiulize, ni watanzania wangapi wataweza kutimiza ndoto hizo? Lakini, iwapo NIT itafanikisha azma yake ya kufundisha marubani hapa nchini, ni hakika kwamba, mbali na kutimiza ndoto za vijana wenye ari ya kuwa marubani, lakini pia itaziba uhaba wa marubani uliopo hivi sasa.

Tuzidi kuiombea serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ambayo kasi yake ya kuleta maendeleo kwa watanzania ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege ifanikishe hata hili la kuiwezesha NIT itimize matarajio yake. Ikumbukwe kwamba mwaka 2014 Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ilibaini kuwa Chuo cha Aviation University College (TAUC) kilichopo Tabata, Dar es Salaam, ambacho kimeidhinishwa na TCAA kutoa kozi ya maofisa wa kutoa huduma katika kampuni za ndege yaani Flight Operations Officers/Flight Dispatcher (FOO), kilikuwa kikiweka matangazo kuwa kinatoa kozi za urubani kwa ngazi ya PPL kwenye tovuti yake, taarifa ambazo hazikuwa sahihi.

 TCAA ilipobaini suala hilo wakati ilipofanya ukaguzi katika chuo hicho cha TAUC ilichukua hatua hapo hapo na chuo hicho kuondoa tangazo hilo kwa kuwa ulikuwa ni upotoshaji na vijana wengi wenye kiu na urubani walikuwa tayari wameanza harakati za kujisajili.

Huo ni mfano mmoja wa kuonesha ni kwa kiasi gani vijana wengi wa kitanzania wana hamu ya kuwa marubani, hivyo NIT isirudi nyuma, kwa kuwa walengwa wa kozi hiyo ni wengi na mahitaji ya taaluma hiyo kwa jinsi nchi inavyokwenda yatakuwa makubwa.

 Hadi kufikia Agosti mwaka huu 2013 Tanzania ina jumla ya marubani 539, takribani asilimia 40 ya marubani hao ni watanzania yaani marubani 208. Kuwepo kwa idadi ndogo ya marubani kunachangiwa na gharama kubwa za ada katika vyuo vya urubani pia uchache wa vyuo vinavyoweza kutosheleza mahitaji ya wanafunzi kwa gharama ndogo hapa nchini.

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, umekuwa ...

foto
Mwandishi: TAHARIRI

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi