loader
Picha

Simba yaapa kufa na Nkana

MABINGWA wa soka Tanzania Bara Simba, jioni ya leo watakuwa na kibarua kizito cha kuwakabili Nkana FC, ya Zambia ukiwa ni mchezo wa marudiano wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (Caf).

Simba inalazimika kushinda mchezo wa leo angalau bao 0-1, ili kufuzu hatua ya makundi hiyo inaokana na kipigo cha mabao 2-1 walichokipata ugenini Kitwe, Zambia wiki iliyopita. Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems, alisema wachezaji wake wote wapo vizuri kwa ajili ya mchezo huo na lengo lao ni kuhakikisha wanashinda ili kutinga hatua ya makundi.

“Tumejiandaa vyema kuhakikisha tunawakabili Nkana, natambua hautokuwa mchezo mwepesi kutokana na ubora wa wapinzani wetu lakini kwakua tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki wetu naamini na sisi tutakuwa na nafasi ya kulipa kisasi na kusonga mbele hatua ya makundi,” alisema Aussems.

Kocha huyo alisema katika mchezo huo amepanga kutumia jeshi lake la maangamizi kwa kupata mabao mengi ya mapema ili kupunguza presha za mashabiki na mabosi wao ambao wamejitoa katika kuiandaa timu hiyo.

Katika mchezo huo ambao mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Josesph Kakunda, Simba wameapa kufia uwanjani kwa kufanya kila linalowezekana ili kuvunja uteja mbele ya Nkana na kuhakikisha wanaweka hai ndoto zao za kutwaa ubingwa wa Afrika kama walivyoagizwa na Rais John Magufuli, mwishoni mwa msimu uliopita. Kwa upande wa kocha wa Nkana FC, Beston Chambeshi, alisema wamekuja wakijua fika ugumu wa mchezo huo wa leo lakini wamejipanga vyema kuhakikisha wanawazuia Simba wasipate bao huku nao wakitafuta bao la ugenini.

Alisema amewasoma vizuri Simba, kwenye mchezo wa awali hivyo anajua ni sehemu gani za kuwabana ili wasiwazuru kwenye mpambano huo ambao wameupa kipaumbele ili kuendeleza rekodi yao ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Caf.

“Ni mchezo wa presha kwa pande zote mbili na tunajua kama Simba ni timu nzuri na watacheza kwa nguvu ili kusawazisha lakini tumejipanga kuwakabili na kufanya kile kilichotuleta na naamini tutafanikiwa,” alisema Chambeshi. Kocha huyo ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo miaka ya nyuma alisema pamoja na Simba kuwa nyumbani lakini hawatokubali kuona wanapoteza mchezo huo na kutolewa kwenye michuano hiyo kirahisi.

Alisema anajivunia uwepo wa beki Hassan Ramadhani ‘Kessy’ kwenye kikosi chake ambaye anajua vyema mazingira ya wapinzani wao Simba na kusema uwepo wake utawasaidia kupata matokeo kwenye mchezo huo.

Mshindi wa jumla katika mchezo huo atafuzu moja kwa moja katika hatua ya makundi wakati timu itakayopoteza itashushwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

KAMPUNI ya MultiChoice imetangaza kuonesha michezo yote ya michuano ya ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi