loader
Picha

‘Nilijikinga mimba nikasahau ukimwi’

JANETH Matiko na Salmini Mayunga (siyo majina yao halisi), wanaishi kama mume na mke, mjini Iringa japo hawajafunga ndoa. Wote wana maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), lakini wanaonekana wana afya njema na wanashukuru dawa za kufubaza VVU za ARVs) zinavyowalinda.

Wanasema watoto wao wawili, mmoja wa miaka mitatu na mwingine wa miezi 10, wamezaliwa wakiwa hawana maambukizi. Wanasema kati yao, hakuna anayejua nani alikuwa na maambukizi ya VVUwakati wakianza uhusiano wa kingono ambao haukuwa salama. “Mahusiano yetu yalianzia shuleni, Janeth akiwa kidato cha kwanza na mimi nikiwa kidato cha nne, miaka minne iliyopita,” anasema Salmini (23).

Kadhalika Janeth (20) naye anasema: “Wakati nikianzisha mahusiano ya kimapenzi na Kalinga, nilikuwa na mahusiano na wanaume wengine wawili. Niliamini Salmin alipitia pia mahusiano kama hayo kwa wasichana wengine wakati tukiwa shule.”

Anasema katika uhusiano wake na wanaume watatu tofauti (akiwemo Salmini) alikuwa na taarifa nyingi muhimu kuhusu VVU/Ukimwi alizopata kwa njia mbalimbali na alihofia maambukizi yake. “Lakini hata hivyo, sikuwahi kuchukua tahadhari, na sikuwa na ujasiri wa kuomba na kuhimiza matumizi ya kondomu wakati nikifanya tendo la ndoa kwa ajili ya kinga ya maambukizi na badala yake, nikajikuta naogopa zaidi kupata mimba kuliko kupata maambukizi ya VVU,” anasema.

Katika uhusiano wake na wanaume hao, Janeth anasema: “Sikumbuki kama niliwahi kutumia kondomu, lakini nakumbuka kutumia dawa za kuzuia mimba kutunga baada ya kufanya tendo la ndoa siku za hatari.”

“Nilikuwa nikitumia mara kwa mara dawa aina ya Postinor 2 (P2) kuzuia mimba kutunga baada ya kufanya tendo la ndoa katika siku zangu za hatari,” anasema. Dk Arestus Mshana wa Maya Medics ya mjini Iringa anazungumzia dawa hizo akisema: “Baadhi ya vijana tunaomini wana elimu ya kutosha kuhusu mimba za utotoni na magonjwa mbalimbali ya zinaa,- huulizia na kununua sana dawa hizi.”

Anasema kwa kawaida yai (Ovum) la mwanamke likishapevuka hutoka kwenye ovari na kusafirishwa mpaka kwenye mfuko wa fallopian (fallopian tube). Hapo husubiria mbegu ya kiume ili lirutibike na likirutibika husafirishwa mpaka kwenye mfuko wa uzazi na hatimaye kutengeneza ujauzito. Anasema dawa hizo zinazoshauriwa kutumiwa ndani ya saa 72 baada ya kufanya ngono katika siku za hatari na huzuia au kuchelewesha kupevuka kwa yai, au kuzuia kusafirishwa kwa yai lililokwishaungana na mbegu ya kiume kutoka kwenye mfuko wa fallopian kwenda kwenye nyumba ya yuterasi.

“Kama vijana wetu, hasa wa kike, wanaogopa zaidi mimba kuliko maambukizi ya VVU ambavyo vyote vinazuilika, basi hii si dalili njema katika mapambano dhidi ya mimba za utotoni na maambukizi ya VVU mkoani Iringa na nchini kwa jumla,” anasema.

Ofisa Elimu- Taaluma katika Mkoa wa Iringa, Martha Lwambano, anatoa takwimu za mimba kwa shule za msingi na sekondari mkoani Iringa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2015 hadi 2017) akisemachangamoto ni kubwa.

Katika kipindi hicho anasema Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya wanafunzi waliopata mimba, ikifuatiwa na Wilaya ya Iringa (Iringa Vijijini). Wakati Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ikiwa na wanafunzi 169, Iringa Vijijini ilikuwa na wanafunzi 132, Mufindi 51, Mafinga Mji 36 na Iringa Manispaa 29.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Butusyo Mwembelo anasema kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Elimu yaliyopitishwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Juni mwaka 2016; kumpa mimba au kumuoa mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 au mwanafunzi wa shule ya msingi, au sekondari ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela. Hata hivyo Mwembelo anasema kesi nyingi za matukio hayo huishia njiani kwa sababu wamekuwa wakikosa ushirikiano kutoka upande ulioathiriwa. Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Mkwawa, Dk Nicodemus Matojo anashauri ufanyike utafiti kujua mimba za utotoni zinatokea wakati gani, katika mazingira gani na kwa sababu gani.

Alipokuwa na ujauzito wa kwanza uliomlazimu kukatiza masomo akiwa ameanza kidato cha pili, Janeth anasema: “Ilikuwa siri ya familia na hakuna mtu aliyejua ujauzito huo ulikuwa wa Salimi mpaka nilipojifungua na kuanza kuishi naye kama mume na mke.” Anasema mama yake anayemtaja kwa jina la Graceana alimsisitizia kuwahi kuhudhuria kliniki na wakati akipata huduma (za kliniki) ndipo alipojua pia ana maambukizi ya VVU. “Lilikuwa suala gumu kwa familia, binti yetu alikatiza masomo kwa sababu ya mimba, lakini pia aligundulika na maambukizi ya VVU.

Nashukuru alipokea vizuri ushauri na kuanzishiwa tiba ya kuzuia maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto; hatua iliyonusuru ujauzito wake,” anasema mama huyo. Janeth mwenyewe anasema: “Baada ya kupata ujauzito huo, sikuamini kwa sababu nilikuwa nikitumia P2 kila nilipotaka kufanya mapenzi siku za hatari, na kwa kweli sikujiandaa kuwa mama.” Anasema ndoto yake ya kumaliza elimu ya sekondari na chuo ilipotoea baada ya kupata ujauzito huo na kuingia mapema kwenye maisha mapya ya mke na mume.

Kauli ya Janeth kwa mujibu wa Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na haki za wanawake na watoto la Life Concern Tanzania (LICOTA), Pamela Makene, inazungumza hatari waliyo nayo wasichana wengi ambao ndoto zao hazijatimia mkoani Iringa na Tanzania kwa jumla. “Chukua wasichana 10 wenye miaka 15 hadi 19 wanaojihusisha na mapenzi katika mtaa wowote mjini Iringa au popote pale nchini, kati yao wapo watakaokiri kufanya mara kwa mara ngono zisizo salama na hivyo kuwa katika hatari ya kupata mimba na VVU,” anasema Makene.

Utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria wa mwaka 2015 na 2016 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaonesha tatizo la mimba za utotoni nchini limeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2016. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu anasema watoto wa kati ya miaka 15 na 19 wameendelea kupata ujauzito na kuharibiwa malengo yao.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2017 ya Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 11 ya wanawake waliojifungua duniani kote walikuwa na umri wa kati ya miaka 15 na 19 na kati yao asilimia 95 wapo katika nchi zinazoendelea.

“Tunataka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini hatutaweza kamawatoto 36 katika kila watoto 100 nchini wanaolewa kabla ya miaka 18 na watoto 27 wa Kitanzania wanapata mimba kabla ya umri huo, hili ni tatizo kubwa ambalo athari zake zitaonekana baadae.” anasema.

Pamoja na kutoa elimu, anasema kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kuokoa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mbalimbali ikiwemo ya mitandao, inayozuia watu kutumiana picha za ngono ili kurejesha maadili ya watoto.

Lakini pia mwaka 2016 serikali kwa kushirikiana na wadau wake ilizindua Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto; mpango ambao moja ya lengo lake ni kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 27 ya sasa hadi kukia asilimia tano ifikapo 2021/2022.

Mkurugenzi wa LICOTA, Pamela Makene anasema: “Mimba za utotoni ni ukatili wa kijinsia kwa watoto na ili tufanikiwe kuukomesha, tunahitaji kuielimisha jamii wakiwemo wavulana na wanaume kwa kuwa ni wahusika kwenye suala la mimba.” Dk Pendo Saro wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) anasema baadhi ya wanawake kwa mara ya kwanza wanajua kuhusu hali yao ya maambukizi ya magonjwa ya ngono na VVU wakati wa ujauzito.

“Mjamzito anatakiwa kupima VVU, homa ya ini, kaswende, gono na magonjwa mengine ya zinaa ambayo ni hatari kwa ujauzito wake,” anasema. Anaongeza kuwa, mjamzito akigundulika kuwa na moja ya maambukizi hayo, huanzishiwa matibabu ili kuzuia mtoto asipate maambukizi yake.

Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi uliofanywa katika ngazi ya kaya kati ya mwaka 2016 na 2017 unaonesha kuwa, Mkoa wa Iringa ni wa pili kitaifa kwa maambukizi ya VVU ukiwa na asilimia 11.3 ukifuatia Mkoa wa Njombe ukiongoza kwa asilimia 11.4. Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Iringa, Menrad Dimoso anazungumzia taarifa za upimaji wa VVU mkoani Iringa kwa mwaka 2017 akisema watu 144,451 kati yao wanawake wakiwa 75,271 na wanaume 69,180 walipimwa. Anasema watu 10,444 wanawake wakiwa 6,093 na wanaume 4,351 walikutwa na maambukizi ya VVU, idadi ambayo ni sawa na asilimia 7.2 ya watu waliopima.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile anasema tabia na mazingira hatarishi kama biashara ya ngono, mapenzi na ndoa za umri mdogo, mfume dume unaowapa wanaume fursa ya kufanya ngono na wanawake wengi, kutotumia kondomu na ukatili wa kijinsia ni baadhi ya sababu zinazosababisha wanawake waambukizwe zaidi VVU. Mtaalamu wa Mambo ya Familia na mwalimu wa shule ya sekondari ya Highlands ya mjini Iringa, Denis Mapunda, anasema “Vita hii ni kubwa” na wazazi wanahitaji taarifa sahihi ya afya ya uzazi kwa vijana ili washiriki kuelimisha watoto wao.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Frank Leonard

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi