loader
Picha

Kila mwanafunzi anaweza kufundishwa hisabati akafaulu

KUNA tafsiri nyingi za neno ‘elimu’, lakini mojawapo ni inayosema kwamba elimu ni maarifa au ujuzi wa ziada aupatao mtu kwa kufundishwa au kujifunza katika mfumo maalumu au mfumo usio rasmi.

Kila binadamu huzaliwa na utashi asilia wa kutambua na kupambana na mambo yaliyo katika mazingira anamoishi ili kuweza kuyamudu. Binadamu anapaswa kuongeza na kupanua uwezo zaidi wa kufikiria na kuwa na maamuzi sahihi juu ya jambo fulani. Uwezo huu unatafsiriwa kuwa ni kiwango cha elimu alichonacho mtu. Katika mfumo rasmi, elimu hutolewa kwa kuzingatia vipengele muhimu kama vile umri, mtaala, aina ya vitabu vya ziada na kiada, aina ya masomo pamoja na mahitaji mengine kutegemea mazingira, wakati na ngazi ya elimu inayotolewa.

Hapo nyuma nchi yetu haikuwa na mfumo rasmi kwa ajili ya masomo ya awali, yaani chekechea, ambayo ni miaka miwili. Hivyo mwanafunzi alikuwa anaanza moja kwa moja darasa la kwanza. Siku hizi kumekuwa na shule za awali, ambako watoto huandaliwa kwa miaka miwili kabla ya kuanza darasa la kwanza. Umri wa kuanza darasa la kwanza ni miaka saba.

Kadiri mwanafunzi anavyopanda madarasa masomo ya kujifunza aidha huongezeka au kubadilika kulingana na mtaala wa kufundishia, ambao ndio dira na mwongozo katika shughuli nzima ya ufundishaji na kujifunza. Katika darasa la kwanza, mwanafunzi anaanza kujifunza masomo ya Hesabu, Kiswahili, Sayansi na Elimu ya Mazingira. Katika somo la Hesabu ambalo makala haya italiangazia kwa kina zaidi, mwanafunzi anajifunza dhana kuu za kuhesabu. Pia anajifunza kuandika, wakati katika somo la Kiswahili hujifunza kusoma na kuimba.

Masomo ya darasa la kwanza na la pili, kwa kiasi fulani yanafanana na kutofautiana kidogo sana. Katika darasa la tatu, somo la Hesabu huanza kuitwa Hisabati. Hapa mwanafunzi anaanza kujifunza matendo makuu manne; yaani kujumlisha, kutoa, kuzidisha na kugawanya katika tarakimu ndogo. Katika ngazi ya darasa la tano na kuendelea hadi darasa la saba, somo hili linakuwa na mada nyingi na nzito kiasi ambazo mwanafunzi anapaswa kujifunza. Aidha kunakuwa na namba zenye tarakimu nyingi, sehemu, desimali, asilimia, vipimio, aljebra, mafumbo na elimu ya maumbo.

Hii ni ngazi ambayo baadhi ya wanafunzi huanza aidha kulichukia somo hili au kuliona kuwa ni ngumu kiasi cha kuanza kulikwepa ama kukata tamaa katika kujifunza kwa bidii, hali ambayo mara nyingi huendelea hadi ngazi za juu za elimu. Pamoja na hayo, somo hili ndilo ambalo limepewa vipindi vingi katika ratiba za masomo kwa hiyo mwanafunzi asipokata tamaa mazingira haya yanamwezesha kulifahamu vyema somo hili ambalo siri yake kubwa ni kulipenda na kulifanyia mazoezi ya mara kwa mara.

Aidha somo hili mara nyingi vipindi vyake hupangwa asubuhi wakati wanafunzi bado hawajachoka kiakili. Hii nayo ni faida kwa wanafunzi. Hisabati pia ni somo linalopendelewa kwa kupewa maswali mengi na muda mrefu kuliko masomo mengine katika ratiba za mitihani ya ndani au ya nje. Ni vyema wanafunzi wakajua pia kwamba serikali imekuwa ikifanya juhudi za makusudi katika kutoa kipaumbele cha ajira kwa walimu wa masomo ya sayansi ikiwamo somo la hisabati na hivyo mwanafunzi anayejitahidi katika somo hili ajue hilo. Kana kwamba hiyo haitoshi, wanafunzi wa elimu ya juu wanaosoma masomo ya sayansi, wamekuwa wakifikiriwa zaidi katika suala nzima la mikopo.

Hii yote ni kuhakikisha ufanisi mkubwa katika masomo ya sayansi na hesabu ambayo hutoa wataalamu mbalimbali na muhimu katika maendeleo ya taifa letu. Lingine la kuzingatia ni kwamba hisabati haikwepeki kwa mwanafunzi anayetarajia kuendelea na masomo ya elimu ya juu ambako anaweza kulazimika kufundishwa utafiti (research) na takwimu, masomo ambayo kuna mahesabu ya kukokotoa.

Nchi yetu inapojielekeza katika kujenga uchumi wa kati unaotegemea viwanda, hakuna ubishi pia kwamba umuhimu wa Hisabati na dada zake (masomo ya sayansi) unakuwa mkubwa zaidi. Lakini kwa bahati mbaya kuna dhana imejengeka miongoni mwa jamii kuwa somo la hisabati ni ugonjwa wa kitaifa. Hii ikimaanisha na kuhalalisha kwamba mwanafunzi kushindwa au kutofanya vizuri katika somo hili sio tatizo lake bali ni tatizo la kitaifa! Dhana hii imezaa matunda mabaya, ambayo huwafanya baadhi ya wanafunzi kukata tamaa na kuacha kujifunza somo la hisabati kwa bidii kubwa.

Katika uchunguzi wangu, walimu pia ni kikwazo kwani baadhi yao hawako tayari kufundisha somo hili hata kama wana uwezo wa kufundisha na hivyo utakuta ni walimu wachache sana wanaochukua somo hili wakiwa katika mafunzo yao ya ualimu vyuoni. Hii inasababisha uhaba wa walimu wa somo hili mashuleni na mimi sitaki kuamini kuwa kila mwalimu hana uwezo wa kufundisha hesabu, hasa kwa shule za msingi. Tatizo lingine ninaloliona kutokana na uchunguzi wangu au kusikia kutoka kwa wanafunzi ni baadhi ya walimu huwabagua wanafunzi darasani.

Walimu kadhaa hupenda kuwashirikisha na kuwauliza maswali wanafunzi wenye uelewa mkubwa wa somo hili na kuwaacha wengine, hali ambayo huwakatisha tamaa au kuwafanya wasijishughulishe na kujifunza kwa bidii. Kila mwanafunzi anapaswa kushirikishwa na kushiriki ipasavyo katika kujifunza bila kujali uwezo wake wa kulifahamu somo.

Kuna dhana nyingine potofu miongoni mwa waalimu kwamba wanafunzi wa kike hawawezi kufanya vizuri katika somo hili, hali inayoweza kumfanya mwalimu asiwatilie maanani katika kipindi chote anachokuwa anafundisha. Hili pia ni kosa kubwa. Kumekuwa hata na misemo inayoashiria kuwa somo la hisabati na dada zake (masomo ya sayansi) ni kwa ajili ya wavulana na kwamba eti wasichana masomo yao ni ya lugha na sanaa. Tabia hii imekuwa ni kikwazo kikubwa kuwafanya baadhi ya wanafunzi hasa wa kike kufanya vizuri katika somo la Hisabati. Baadhi ya wazazi na walezi ni tatizo pia.

Wazazi na walezi wengi huwakatisha tamaa watoto katika kujifunza na kufanya vizuri katika somo la hisabati, kwa kutumia historia zao wakati wakiwa shuleni. Baadhi yao huwaambia watoto kwamba hisabati ni somo gumu kwani hata wao lilikuwa linawapa tabu katika kujifunza enzi zao. Wakati wazazi hawahamasishi somo la Hisabati, wengi wao hupenda watoto wao kufahamu zaidi lugha ya Kiingereza. Ukweli huu unajidhihirisha pale ambapo watoto wengi hupelekwa katika shule zinazotumia Lugha ya Kiingereza kufundishia (English Medium Schools).

Hata watoto wanapohitimu masomo ya shule ya msingi, utaona wakati wa maandalizi ya kujiunga na kidato cha kwanza (pre form one) wanafunzi wakifundishwa Kiingereza na siyo Hisabati! Ni vyema jamii ikafahamu kwamba licha ya Hisabati kuhusika katika maisha yetu ya kila siku lakini, kama nilivyodokeza hapo juu zama hizi ni za sayansi na teknolojia ambazo zinatuhitaji pia kuwa weledi wa Hisabati. Hakuna kisichowezekana endepo walimu na wadau wengine watazidisha bidii ya dhati katika kuhakikisha wanafunzi wanapenda na kujifunza Hisabati.

Mwalimu makini, mbunifu na anayefundisha kwa kujituma ni chachu kubwa sana katika kuwafikisha wanafunzi wake kufanya vizuri katika masomo yao ikiwemo hisabati. Ni vyema jamii kuanzia sasa ikawajengea watoto msingi imara wa Hisabati na kulipenda somo hilo kuanzia ngazi ya chini.

Wanafunzi wapongezwe, washindanishwe, washauriwe na kupewa motisha mbalimbali katika harakati za kujifunza hisabati, wajengewe utamaduni wa kufanya mazoezi mengi ya hisabati na wajifunze somo hili kutoka kwa wataaamu mbalimbali kupitia vitabu vya Hisabati. Naishauri serikali iendelee kutoa kipaumbele cha kuajiri walimu na wataalamu wa hisabati pamoja na kuwapa motisha mbalimbali zitakazowapa nguvu na ari ya kufanya kazi kwa bidii.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Samson Sombi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi