loader
Picha

Mwaka 2018 na mafanikio utekelezaji miradi ya miundombinu

KATIKA mwaka 2018, serikali imeacha alama kubwa na muhimu za kimaendeleo katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, bwawa la kuzalisha umeme wa Mto wa Rufi ji pamoja na ujenzi unaoendelea wa reli ya kisasa (SGR).

Jambo la kipekee ni kwamba, kwa kiasi kikubwa miradi hii inatekelezwa na serikali kwa kutumia fedha zake yenyewe pasipo kutegemea misaada au mikopo kutoka kwa nchi au mashirika wafadhili kutokana na kuwapo mapato ya ndani kutoka vyanzo mbalimbali. Hiyo ni alama muhimu na yenye kulijengea heshima kubwa taifa hili kwa kuthubutu kujivua kutoka katika fikra za muda mrefu ambazo nchi nyingi za Afrika zilikuwa zikiamini kuwa, pasipo misaada na mikopo ya kifedha kutoka kwa wafadhili, haziwezi kutekeleza mipango yake ya kimaendeleo.

Mapinduzi hayo ya kifikra ambayo serikali chini ya Rais John Magufuli inayatekeleza fedha zake yenyewe, yanapaswa kuendelezwa na kuwa chachu ya mabadiliko ya kifikra kwa baadhi ya nchi za Afrika ambazo bado zinaamini kuwa haziwezi kuendelea bila misaada na mikopo ya wafadhili. Msomi na Mchumi kutoka Zambia, Dambisa Moyo, anasema katika kitabu ‘Dead Aid’ yaani Msaada Mfu (tafsiri isiyo rasmi), anasema zaidi ya miaka 30 iliyopita, nchi nyingi zilizokuwa zikitegemea misaada, zilikua kwa wastani wa asilimia hasi 0.2.

Moyo anasema kati ya mwaka 1970 na 1998, kiwango cha misaada kilichotolewa kwa Afrika kilikuwa juu, lakini kiwango cha umaskini pia kiliongezeka kutoka asilimia 11 hadi kufikia asilimia 66. Anasema kwa miaka zaidi ya 50, Dola za Marekani zaidi ya trilioni 1 zilitumwa Afrika kutoka nchi tajiri kama msaada wa kimaendeleo, lakini fedha hizo hazikufanya maisha ya Waafrika kuwa bora katika miongo hiyo, bali wameendelea kuwa masikini.

Serikali ya Tanzania imewajengea na inaendelea kuwajengea Watanzania ujasiri wa kujiletea maendeleo kwa nguvu zao kupitia kodi wanazolipa na kujituma kufanya kazi kwa ufanisi. Katika kuhakikisha sekta ya usafirishaji wa reli na barabara inaimarika ili kufikia uchumi wa kati na viwanda, serikali inatekeleza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro katika awamu ya kwanza na awamu ya pili inayoanzia Morogoro hadi Dodoma kwa takriban Sh trilioni 7.

Zote zinatolewa na serikali. Reli ya kisasa inaelezwa kuwa bora kuliko reli zote barani Afrika. Ubora huo unatokana na mambo mbalimbali ukiwemo uwezo wa reli kupitisha treni zenye mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa, kupitisha mzigo wa tani kati ya milioni 17 hadi 25 kwa mwaka pamoja na madaraja yenye uwezo wa kudumu kwa miaka 100 huku chuma cha reli hiyo kikidumu kwa miaka 40 kabla ya kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Desemba 19 mwaka huu, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la upanuzi wa Barabara ya Morogoro katika njia nane ambazo katika sehemu nyingine zitakuwa 12 kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha yenye urefu wa kilomita 19.2 kwa gharama ya Sh bilioni 141.5, ambazo pia zimetolewa na serikali. Upanuzi huu unaofanywa na kampuni ya mkandarasi Mzawa ya Estim Construction Company Ltd, utaifanya barabara hiyo iliyopewa jina la Tanzania One kuwa barabara bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, itakamilika katika kipindi cha miezi 30.

Kukamilika kwa upanuzi wa barabara hii, kutachochea ukuaji wa uchumi kwa kurahisisha shughuli za usafirishaji bidhaa ndani ya nchi lakini pia kati ya Tanzania na nchi jirani za Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutumia fedha zake yenyewe, pia inatekeleza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Mto Rufiji kwa gharama ya Sh trilioni 6.558 utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 na utakamilika katika kipindi cha miezi 36.

Mradi huu unaojengwa na Kampuni ya Kikandarasi ya J.V Arab Contractors/El Sewedy Electric kutoka nchini Misri, unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 70 zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme duniani. Katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradu huu Ikulu jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, alisema ujenzi wa bwawa hilo, unaifanya Tanzania kushika nafasi ya 60 kati ya 70 ya nchi zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme duniani.

Utekelezaji wa miradi hiyo bila kutegemea misaada na mikopo kutoka kwa wafadhili au taasisi za kifedha za kimataifa, ni mageuzi makubwa ya kiuchumi na kifikra ambayo serikali ya awamu ya tano imewaletea Watanzania. Hatua ya serikali ya kujenga miundombinu hii mikubwa kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi ni muhimu kwa kuwa siyo tu inajenga hali ya kujiamini kama taifa, bali pia ni heshima kwa taifa na watu wake.

Misaada siyo kitu kibaya, lakini kama anavyosema Moyo, imechangia kuchelewesha maendeleo ya Waafrika kwa zaidi ya miaka 50, hivyo hatua ya serikali kutumia fedha zake kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ni mageuzi ambayo nchi za Afrika zilipaswa kuyafanya zilipopata uhuru wake. Profesa wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi, anasema uwekezaji huo wa Serikali unaufanyika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa na uzalishaji wa umeme, ni muhimu kwa kuwa itasaidia katika shughuli za uzalishaji na uchumi itakapokamilika.

Anasema uamuzi wa serikali kujenga miundombinu hii kwa fedha zake zenyewe ni ‘best practices’ (mfano bora wa kuigwa), lakini akataka serikali iwawezeshe zaidi wataalamu wazawa ili wajenge miradi kama hiyo badala ya kuwatumia wataalamu wa kigeni. “Ni muhimu sana uwekezaji kama huu ukawa unatekelezwa na wataalamu wazawa, hivyo ni muhimu kwa serikali ikaijengea uwezo wa kiteknolojia na kifedha nguvu kazi ya ndani ili kuepuka kuwatumia wataalamu wa kigeni, ukiyatumia makampuni ya ndani uchumi unakua vizuri kwa sababu fedha zinabaki hapa nchini,” anaeleza Profesa Ngowi.

Mtaalamu mwingine wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Razack Lokina, anasema uamuzi huo wa serikali wa kujenga miundombinu ya barabara, reli na mradi wa kuzalisha umeme wa Mto Rufiji kwa fedha zake ni sahihi kwa sababu hakuna haja ya kulimbikiza madeni kama uwezo wa kufanya wenyewe upo. Lokina anasema miradi hiyo ina manufaa makubwa kiuchumi ya muda mfupi hususani inapotekelezwa kwa kuwa kuna watu walioajiriwa na waliojiajiri kupitia shughuli binafsi zinazoambatana na ujenzi huo, lakini pia manufaa ya kiuchumi ya muda mrefu kwa kuwa husaidia katika usafirishaji wa bidhaa na watu.

Maendeleo katika utekelezaji wa miradi hii mwaka 2018 ni mafanikio ya ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere zilizolenga kuwafanya Watanzania kuondokana na umasikini kupitia uongozi wake uliotukuka na uzalendo wake kwa nchi. Mwalimu daima aliwataka Watanzania kufanya kazi kama njia pekee ya kuondokana na umasikini na kupambana na maadui wengine ambao ujinga na maradhi.

Kwa kutambua thamani ya uhuru, Chama cha TANU chini ya Mwalimu Nyerere kilitangaza Azimio la Arusha mwaka 1967 ikiwa ni miaka sita tu baada ya uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961. Katika Kitabu, ‘Miongozo Miwili’ ambacho ni kazi ya Bashiru Ally, Saida Yahya- Othman na Issa Shivji, Azimio la Arusha linatambua kwamba uhuru wa nchi na watu wake haukamiliki kutokana na kupata wimbo na bendera ya taifa au mawaziri na viongozi wazawa, bali uhuru huo ni hatua ya awali katika mchakato wa ukombozi.

Katika kitabu hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru anasema ukombozi katika jamii una pembe tatu, yaani uhuru wa nchi iliyotawaliwa na wakoloni, uhuru wa watu au jamii katika nchi na tatu, ni ukombozi wa wavuja jasho kutoka makucha ya unyonyaji na ukandamizaji. Kwa mantiki hiyo, Azimio la Arusha linaamini katika dhana ya pembe tatu za ukombozi, yaani uhuru wa nchi hautakuwa na maana wala hautakuwa salama kama nchi itaendelea kutegemea misaada, mikopo na uwekezaji kutoka nje maana ‘kujitawala ni kujitegemea.’ Mwalimu mara zote amekuwa akiwataka viongozi kuendelea kushughulika kwa dhati dhidi ya umasikini wa wananchi na pia, kuwatia moyo na shauku ya kujitemea.

Mbunge wa Mbinga Mjini kwa tiketi ya CCM, Sixtus Mapunda, anasema kuwa taifa lolote duniani linalotaka kujitegemea, huanza na kile ilicho nacho mkononi badala ya kuanza kwa kutegemea misaada na mikopo ya wafadhili. Anasema uamuzi wa serikali wa kujenga miradi hiyo kwa kutumia mapato ya ndani unatokana na taifa kumpata Rais mzalendo Magufuli anayetambua kuwa, misaada huwa na masharti magumu na mikopo huwa na riba kubwa. “Haya ni maendeleo chanya yanayotupeleka katika kujitegemea kwa kuwa hata nchi kama za Japan, China, Korea Kusini, zimeendelea kwa kutegemea fedha zao wenyewe siyo misaada na mikopo; kuombaomba ni kujidhalilisha,” anaeleza Mapunda.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, anasema bado serikali inakopa fedha. Rais Magufuli mara nyingi amekuwa akiwasisitiza Watanzania kupenda kulipa kodi kwani ndiyo inayotumika kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa pamoja na mradi wa kuzalisha umeme wa Mto Rufiji. Kwa kulipa kodi, taifa litaepuka mtego wa kuwa na madeni makubwa na madogo kama anavyoeleza Profesa Lokina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi