loader
Picha

Yajue yaliyosaidia kudhibiti ujangili

WANYAMAPORI ni maliasili, rasilimali na urithi ambao Tanzania imebarikiwa kuwa nao unaoiingizia fedha zikiwamo za kigeni kutokana na watalii wanaofi ka kuwaona.

Kati ya mwaka 2007 na 2013 kulikuwa na kiasi kikubwa cha tishio la ujangili dhidi ya wanyama pori hali iliyoonekana kuathiri na kupunguza zaidi idadi ya tembo. Hata hivyo, zipo jitihada kadhaa zilizofanyika kudhibiti hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti masoko ya bidhaa zitokanazo na tembo; hususani meno ya tembo. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Dk James Wakibara, anasema jitihada za serikali pamoja na ushirikishaji wananchi umesaidia kupunguza vitendo vya ujangili.

Kadhalika, jumuiya za kimataifa pia zimekuwa mstari wa mbele kushiriki katika juhudi za kudhibiti vitendo hivyo. “Maana halisi ya jangili siyo yule anayekamatwa na meno pekee, bali anayeua wanyama, lakini pia wapo wasafirishaji, wauzaji na hata masoko yenyewe,” anasema Wakibara. Anasema kwa sasa vifo vya tembo vimeshuka na mwaka jana, ni mafuvu matatu pekee ya tembo yaliyobainika tofauti mna miaka iliyopita hali ilipokuwa mbaya zaidi. Kwa mujibu za takwimu za Tawa, katika Pori la Akiba la Selous, idadi ya tembo kwa mwaka 2007 ilikuwa 70,000 na ilipofika mwaka 2013 baada ya ujangili kukithiri, idadi ilishuka hadi tembo 13,000.

Kuwapo kwa vitendo vya aina hiyo ni miongoni mwa vigezo vinavyoweza kusababisha wanyamapori kupungua kwa kiwango kikubwa achilia mbali, wanyama wanaokufa wenyewe ama kutokana na uzee, au magonjwa. Anasema jambo linaloashiria kuongezeka kwa tembo ni pamoja na wanyama hao kuondoka hifadhini kwenda kushambulia mashamba ya wananchi yenye mazao ya aina mbalimbali.

Kwa sasa Shirika la Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) liko katika mchakato wa kufanya sensa ya wanyama kutokana na utaratibu wake wa kila baada ya miaka mitatu jambo litakalobainisha idadi ya wanyama hao kwa sasa. Anazitaja zenye masoko zaidi ya bidhaa zitokanazo na ujangili wa tembo kuwa ni pamoja na China, Indonesia, Vietnam na Malaysia. Anasema kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa, ujangili umedhibitiwa. Nchini Tanzania, anasema ujangili umepungua kutokana na doria za mara kwa mara zinazofanywa na askari wa wanyamapori nchi nzima kutoka Tawa, Hifadhi za Taifa(Tanapa), Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Anasema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano baina yao na polisi, Mahakama, Idara ya Usalama wa Taifa, vyombpo mbalimbali vya ulinzi na usalama, pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi wanyamapori wa ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa ya uhifadhi. Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge WMA, Olais Olekoin anasema ujangili wa kitoweo unaofanywa na wananchi umekuwa changamoto kubwa. Anasisitiza kuwa ule wa meno ya tembo umetokomezwa kwa kiwango kikubwa huku elimu ikiendelea kutolewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi.

Katika hifadhi hiyo wapo tembo wengi wakiwa na ulinzi imara na watu hawaruhusiwi kwenda kuwatazama kwa kuwa wako katika eneo la kitalu. “Kufa kwa tembo katika hifadhi hii kunatokana na ugonjwa au uzee, pia uwapo wa silaha umeongeza kasi ya kupambana na majangili,” anasema Olekoin. Anasema hata hivyo mbinu za majangili hubadilika mara kwa mara, hivyo ni muhimu wahusika kupatiwa mafunzo zaidi ya mara kwa mara. Kwa msingi huo, ipo haja ya kuwa na watu wenye mbinu mbalimbali na ujuzi, na askari wa ulinzi kupatiwa mafunzo na silaha kali zaidi ili kuendelea kukabili ipasavyo vitendo hivyo ili kuvimaliza kabisa.

Olekoin anasema ipo haja kuwa na mbinu zaidi na ujuzi mpya wa kutosha kutokomeza vitendo vya ujangili hasa ikizingatiwa kuwa, maadui hujifunza mbinu mpya kila kunapokucha. Anasema: “Ni kweli kwa sasa ujangili wa meno ya tembo umepungua kwa kiwango kikubwa, na hata wanyama hao wameanza kuonekana katika mashamba ya wananchi wakishambulia mazao, jambo linaloonesha kuwa wameongezeka na ujangili kudhibitiwa.”

Kutokana na manufaa mbalimbali yatokanayo na uhifadhi wa wanyamapori, wananchi wakiwamo wanaozunguka hifadhi wameshirikishwa kwa kina ili washiriki moja kwa moja katika hatua zote za ulinzi na uhifadhi; na pia kutunza mazingira. Mkazi wa Kijiji cha Mwada, Nyakale Fomi anasema hifadhi ya Burunge iliyoundwa kwa kutumia maeneo ya wanakijiji wanajitahidi kutoa elimu kwa wananchi wanaoizunguka jumuiya hiyo jambo linalomfanya kila mmoja kuwa mlinzi wa eneo hilo. Hata hivyo anasema, mgawanyo sawa na wa wazi wa mapato yapatikanayo katika jumuiya hiyo kwenda kwa wananchi umekuwa ukiongeza ari kwa wananchi kushiriki kulinda hifadhi kwa nguvu moja.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi