loader
Picha

Fuatilia wanachotazama wanao kwenye intaneti

MAMILIONI ya watu ulimwenguni wanatumia mitandao wakiwa katika maeneo mbalimbali kama vile nyumbani, kazini, shuleni, kwa marafiki, vyombo vya usafiri na kwingineko.

Huenda watoto, wanafunzi au familia yako wanaelewa zaidi ulimwengu wa intaneti kuliko wewe, na wanaweza kukuficha mambo wanayoyafanya kwenye mitandao.

Duniani pote watu wanawasiliana kwa njia ya mtandao, kwa mfano nchini Canada, takribani vijana wote wenye simu za mkononi wanatumia intaneti.

Mtandao huo umerahisisha mawasiliano lakini usipotumiwa vyema una hatari kwa mtoto au kijana. Katika nchi zilizoendelea wakati fulani ilionekana kwamba ingekuwa salama kutumia intaneti ikiwa kompyuta ingekuwa mahali palipo wazi.

Katika nchi zinazoendelea na hata zenye maendeleo makubwa, watoto na vijana wanaweza kutumia intaneti mahali popote kama vile katika maduka yenye kutoa huduma za intaneti (internet cafe ) na kwenye simu za mkononi.

Dunia ya sasa ni ya ushindani, watu wengi maarufu na wale wanaowaiga watu hao hutuma picha na habari za kila aina zinazoonesha maisha yao ya ukwasi na mambo mengine mengi ya usasa, yote haya huwavuta watu wengi kutumia mitandao.

Wazazi hawawezi siku zote kuwazuia watoto wao kuendesha gari au kutumia simu za mkononi, lakini wanaweza kuhakikisha kwamba watoto wao wamefundishwa kuendesha gari kwa njia salama

. Wazazi wengi wamechukua hatua kama hiyo kuhusu matumizi ya intaneti. Mkazi wa California nchini Marekani anayejitambulisha kwa jina la Michel anasema, ametenga muda kwa ajili ya wanawe kuangalia intaneti.

“Na ninaongea nao mara kwa mara kuhusu vituo visivyofaa na watu wanaoweza kukutana nao katika vituo mbalimbali vya mitandao wasio na nia nzuri kwao na pia madhara ya mtandao,” anasema.

“Ni jukumu la kila mzazi au mlezi kuhakikisha watoto wao hawafungui vituo visivyofaa na kuhakikisha wanawapa malezi mema na yenye maadili.”

Wazazi ambao watoto wao wanatumia intaneti wanahitaji kujua mambo ya msingi kuhusu mtandao huo na pia kufahamu watoto wao wanafanya nini wanapotuma na kupokea ujumbe mfupi, wanapofungua tovuti au kufanya mambo mengine katika mtandao.

"Usikate kauli kwamba wewe ni mzee sana au huna elimu ya kutosha kujifunza na pia usijione au kujihukumu kuwa umepitwa na wakati ," anasema Marshay, mama mwenye watoto wawili jijini Dar es Salaam.

"Usiachwe nyuma na teknolojia. Fuatilia kwa makini wanachokiangalia watoto wako au wanafunzi wako kupitia mtandaoni. Kwa kweli dubwana hili mengi mazuri ya kujifunza lakini pia lina kila aina ya uchafu, kwa kifupi ni kama kokolo, linalokusanya kila kitu kizuri na kibaya,” anasema.

Watu wanaotoa huduma za mtandao na programu za kompyuta wametengeneza programu zinazoweza kuchuja au kuzuia ujumbe unaokuambia ufungue tovuti zisizofaa .

Baadhi ya programu zinaweza hata kumzuia mtoto asitoe habari za kibinafsi kama vile jina au anuani yake. Nchini Uingereza, utafiti unaonesha kwamba zaidi ya asilimia 57 ya vijana walio na umri kati ya miaka 9 na 19 wanaotumia intaneti kila juma wametazama picha za ngono.

Asilimia 16 ya wazazi wanaoamini kwamba watoto wao wameona picha hizo chafu kwenye intaneti. Katika familia nyingi kazi za nyumbani zimekuwa zikifanyika kiuzembe na kuchelewesha muda wa chakula, hasa mwenye nyumba anapokuwa hayupo kwa sababu mitandao.

Uchunguzi uliofanywa nchini Uingereza unaonesha kwamba kijana mmoja kati ya watano aliye na umri wa kati ya miaka 9 na 19 anaweza kutumia intaneti katika chumba chake cha kulala.

Kuweka kompyuta mahali pa wazi kunawasaidia wazazi kuchunguza kile ambacho watoto wao wanafanya kwenye intaneti na kuweza kuwafundisha wajiepushe na mambo yasiyofaa.

Ni kwa mantiki hiyo mzazi unashauriwa kutenga wakati ambao watoto wanaweza kutumia intaneti, muda wanaopaswa kuitumia, na vituo ambavyo hawapaswi kuvifungua .

Zungumzia sheria zako hizo pamoja na watoto wako na uhakikishe kwamba wamezielewa na kuzifuata kwa manufaa yao na ya wengine. Ni muhimu kuwafundisha watoto kanuni zinazofaa ili wafanye uamuzi wenye tija wakati ambao wewe uko mbali nao.

Waeleze matokeo ya kuvunja sheria zako kuhusiana na intaneti na mambo mengine muhimu yatakayowasaidia maishani mwao.

Chunguza jinsi watoto wako wanavyotumia intaneti na uwaeleze kwamba utakuwa unawachunguza. Kufanya hivyo si kuingilia faragha yao.

Shirika la Upelelezi la Marekani linapendekeza kwamba wazazi wachunguze akaunti za watoto wao za mitandao kama Facebook, barua pepe zao na tovuti ambazo wanafungua. Huko wanaweza kujua kama wameshaanza kupotoka au la na kuwasahihsha.

Mwanasayansi na Profesa anayeishi California Marekani, Raymond Rugemalira Mwijage anasema ametenga muda maalumu wa familia yake kuangalia TV, na pia anafuatilia kwa ukaribu kila mwanafamilia anachofanya kwenye intaneti.

Anasema, huwezi kuchunguza jinsi mtoto wako anavyotumia intaneti kila wakati ila namna unavyowafundisha na mifano hai anayotoa anaona vinaweza kuwalinda, hivyo ni muhimu kuzungumza na watoto wako kuhusu hatari za intaneti.

“Njia bora zaidi ya kuwalinda watoto wako dhidi ya hatari za intaneti ni kuwasiliana nao wewe mwenyewe mzazi waziwazi.

"Tulizungumza na wavulana wetu kuhusu watu "wabaya" kwenye intaneti.

Pia tuliwaeleza ponografia ni nini, kwa nini wanapaswa kuiepuka, na kwa nini hawapaswi kamwe kuwasiliana na watu wasiowajua," anasema.

Intaneti imekuwa pia ikipotezea watu muda wa kufanya kazi watu wengi maofisini wamekuwa wakitumia muda mwingine kuchati na kusoma hata mambo yasiyo muhimu kwenye intaneti badala ya kuchapa kazi. Watoto wanapaswa pia kuelezwa madhara hayo.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi