loader
Picha

Niionavyo ziara ya wizara sita Kigoma

TUNAPOUANZA mwaka mpya wa 2019, serikali chini ya uongozi wa Rais John Magufuli imeandika historia mpya kwa kufanya kazi kwa mtindo wa kutatua changamoto mtambuka za sekta mbalimbali kwa kuzishirikisha wizara zote husika na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto hizo.

Katika wiki ya kwanza ya mwezi huu wa Januari, mawaziri watano kwa pamoja wamekutana mkoani Kigoma ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa masuala mbalimbali ya sekta zao.

Awali kabla hawajaenda wao, walitanguliwa na timu ya makatibu wakuu walioratibu zoezi zima kisha na baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, waliandaa tamko la Serikali kuhusu kukabiliana na changamoto hizo na kulisaini Januari 6, 2019.

Wizara zilizoshiriki katika zoezi hili zinajumuisha Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi); Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Maliasili na Utalii; Mifugo na Uvuvi; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Kilimo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma iliratibu na kushiriki kikamilifu katika kazi hii. Timu hiyo ya mawaziri ilikubaliana mambo kadhaa katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira mkoani Kigoma unaotokana na uvamizi wa mapori ya wanyamapori na hifadhi pamoja na kuhakikisha eneo lililotolewa na Rais lenye hekta 10,012.61 kutoka kwenye Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini kwa ajili ya kilimo na mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Ilikubalika kuwa, hekta 2,174 (ekari 5,435) zitolewe kwa Kijiji cha Mvinza, hekta 2,496 (ekari 6,240) zimetolewa kwa Kijiji cha Kagerankanda na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu hekta 5,342.61 (ekari 13,356.)

Serikali inaandaa mpango mahsusi wa matumizi bora ya ardhi ili kuwezesha zoezi la ugawaji kufanyika vizuri.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga jumla ya hekta 20,000 kutoka maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya ufugaji wenye tija na itaendelea kutafuta maeneo mengine kwa ufugaji wa namna hiyo.

Lingine lililokubaliwa ni Uongozi wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha kuwa usafirishaji wa mifugo unazingatia Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo Namba 12 ya Mwaka 2010.

Ilikubalika pia kuwa, wananchi wote waliovamia eneo lililoko kwenye mpango wa uanzishwaji wa vitalu vya ufugaji na mashamba ya kilimo katika Halmashauri ya Uvinza (Mwanduhubanhu) wapangiwe na mamlaka husika kwa ufugaji na kilimo chenye tija.

Hii ni baada ya tathmini iliyoelekezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kukamilika.

Aidha, ilikubalika kuwa Serikali itasaidia vijiji katika maeneo yao kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na katika mipango hiyo, watenge maeneo kwa ajili ya ufugaji na kilimo kulingana na mahitaji yao.

Tamko hilo lilisisitiza kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazohusu wakimbizi ili kuhakikisha kuwa, nao hawachangii uharibifu wa mazingira, maliasili na usalama wan chi.

Kwa msingi huo, ilikubalika kuwa wahamiaji haramu wote wataondolewa nchini haraka na serikali iendeshe operesheni ya kuondoa uvamizi wa wakulima, wafugaji na watu wengine wanaofanya shughuli zisizo halali katika misitu na mapori yaliyohifadhiwa kisheria zikiwemo hifadhi za misitu ya serikali kuu, hifadhi za misitu za halmashauri za wilaya na vijiji.

Kwa mtazamo wangu, mambo haya yakitekelezwa kwa umakini, yataleta ufumbuzi mkubwa wa migogoro ya kila uchao ambao siyo tu imekuwa ikirudisha nyuma uchumi wa nchi kwa kukosa mapato yatokanayo na utalii na mifugo, bali pia imekuwa ikiondoa uhai wa watu kupitia mapigano ya watumiaji wa ardhi.

Kimsingi tamko hili litasaidia kuondoa dhana mbaya iliyoanza kujengeka katika siku za hivi karibuni ya kubaguana kwa wananchi kwa kuona kuwa baadhi ya Watanzania hawana haki ya kuishi katika maeneo fulani.

Itakumbukwa kuwa, katika ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa mwaka jana katika Kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu, Rais Magufuli alikemea tabia ya kuwabagua wafugaji kwa kuwataka warudi walikotoka.

Mkuu wa Nchi akasisitiza kuwa, kila mwananchi ana haki ya kuishi popota nchini Tanzania kwa kufuata sheria za nchi.

Ni ukweli usiopingika kuwa, kila kitu kina umuhimu wake katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa binadamu na taifa kwa jumla, hivyo dhana ya kuona ama mifugo ni bora kuliko maliasili nyingine au maliasili nyingine ni bora kuliko mifugo, ni potofu na imepitwa na wakati.

Ukweli huu ndio unanifanya niseme kuwa, mtindo na mfumo waliotumia mawaziri hawa katika kutatua changamoto mkoani Kigoma hauna budi kupongezwa na kupigiwa mfano.

Kwa mantiki hiyo, kinachotakiwa sasa ni usimamizi makini na kamilifu ili mazingira, maliasili na mifugo ilindwe kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye.

Nimekuwa nikijiuliza hivi siku moja ikitokea kwamba mifugo yote nchini haipo, Tanzania itageuka kuwa nchi masikini kwa kiasi gani na madhara ya hali hii kwa watanzania yatakuwa makubwa kiasi gani.

Hii ni kwa kuwa faida za mifugo siyo tu ni nyingi, bali pia ni muhimu kwa uchumi, ajira, lishe kwa taifa.

Kadhalika, nimekuwa nikiwaza kama mazingira ambayo ni vivutio mbalimbali vya utalii ambavyoTanzania imebarikiwa kuwa navyo yakiharibiwa, ni majanga makubwa kiasi gani yatatokea na kuangamiza jamii.

Hakika tathmini iliyofanywa mkoani Kigoma kuhusu uvamizi wa hifadhi za misitu na tamko la serikali lililotolewa na wazara hizo sita na kusainiwa na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jaffo aliyekuwa Mwenyekiti wa timu hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamsi Kigwangala, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angelina Mabula na Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mussa Sima litakuwa na maana kama utekelezaji wake utasimamiwa kwa makini ili lilete matunda tarajiwa, badala ya kuzalisha changamoto nyingine.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe.

Kwa mfano, utoaji mifugo katika maeneo hayo unatakiwa kuzingatia sheria zote maana endapo sheria moja itaachwa, yataibuka matatizo makubwa kama ya awali tuliyoona maelfu ya ng’ombe yakikamatwa na kufungiwa bila kupewa malisho wala matibabu.

Hali hiyo, ilisababisha ng’ombe kadhaa kufa jambo ambalo lisingetokea kama sheria zote zingefuatwa kikamilifu na hata upotevu mkubwa wa mifugo usingetokea.

Ieleweke pia kuwa, mifugo ni hazina na mali ya taifa letu kwa kuwa faida ya mifugo siyo ya mmiliki wa mifugo pekee, bali inajizungusha na kuonekana kwa jamii nzima likiwamo suala la ubora wa kiuchumi.

Inashangaza kuona wakati fulani kwa baadhi ya watendaji wa serikali wamekuwa wakichukia mifugo na kuiadhibu bila kufuata sheria kwa kisingizo cha uvamizi.

Hii si jambo jema kama ambavyo binafsi sijawahi kusikia mashamba ya mazao yaliyopo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, eti yameng’olewa.

Bila shaka viongozi wakuu wa wizara hizi sasa wameonesha msimamo mzuri kuhakikisha mambo kama hayo hayajitokezi tena.

Hii ni kwa kuwa changamoto hizo zitatatuliwa kwa kuzingatia sheria zote ili kuliletea taifa maendeleo tarajiwa katika kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati.

Rasilimali hizi na mifugo zina mchango mkubwa katika mapinduzi ya viwanda. Usimaizi madhubuti wa tamko hilo, utasaidia kama siyo kuondoa kabisa, basi kupunguza baadhi ya athari zinazoweza kujitokeza.

Athari hizi ni pamoja na sehemu kubwa ya hifadhi za misitu na mapori ya wanyamapori kupoteza uoto wake wa asili, kuharibika kwa vyanzo vingi vya maji ikiwemo mito mikubwa na kupungua kwa bioanuai.

Nyingine ni kuongezeka kwa matumizi ya dawa za mifugo katika hifadhi kunakosababisha kuchafuka kwa vyanzo vya maji na kuua viumbe hai, tishio la kuzuka kwa magonjwa hatari kutokana na mwingiliano wa mifugo na wanyamapori katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Magonjwa haya ya mifugo ni pamoja na kimeta (anthrax) midomo na miguu (FMD), kichaa cha mbwa (rabies), malale (sleeping sickness) na nagana (trypanosomiass).

Aidha, athari nyingine kubwa ni pamoja na kuongezeka kwa migogoro kati ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hali inayosababisha mauaji na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Athari hizi zimesababisha kupungua kwa ubora wa malisho ya mifugo, wanyamapori pamoja na kuathiri upatikanaji wa mvua za uhakika na hivyo, kutishia uhakika wa chakula na kuongezeka kwa tishio la kiusalama.

Kimsingi, hali hii inachangiwa pia na wakimbizi na wahamiaji haramu kujihusisha na shughuli mbalimbali kinyume cha sheria katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Timu hiyo ya mawaziri pia ilishuhudia ndani ya Msitu wa Makere Kusini kuwapo kwa mashamba madogo madogo ya mazao mbalimbali yanayolimwa na wakimbizi.

Mawaziri hao walifanya ziara katika msitu huo kwa zaidi ya saa sita na kisha kufanya mkutano katika Kijiji cha Kabulanzwili baada ya kufika katika Mto Migezibiri ambao ni mpaka wa Hifadhi ya Makere wilayani Kasulu.

Mwandishi wa makala haya ni Kaimu Katibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi anapatikana kupitia 0784441180 na jmapepele1@gmail.com

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: John Mapepele

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi