loader
Picha

MV Mbeya II Mkombozi usafiri Ziwa Nyasa

UJENZI wa meli mpya na ya kisasa ya abiria iliyopewa jina la MV Mbeya II kwa ajili ya matumizi ya mwambao wa Ziwa Nyasa ulioanza Julai mwaka 2017, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Hizo ni habari njema kwa wakazi wa mwambao wa ziwa hilo maarufu na la tatu kwa ukubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.

Kukamilika kwa ujenzi huo unaofanywa na raia wa Tanzania aliyebobea katika ujenzi wa vyombo vya usafiri majini, Saleh Songoro wa kampuni ya Songoro Marines ya jijini Mwanza, kunakamilisha ndoto za Rais, Dk John Magufuli aliyeahidi kutatua kero ya usafiri katika ziwa hilo lenye urefu wa kilometa 560 na upana wa kilometa 50-80 ambalo linapatikana katika nchi za Tanzania, Malawi na Msumbiji.

Alitoa ahadi hiyo wakati akiomba ridhaa ya kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwishoni mwa mwaka 2015.

Baada ya kuchaguliwa kuingia madarakani kumrithi mtangulizi wake, Jakaya Kikwete, serikali ya Rais Magufuli ilimwaga fedha kiasi cha Sh bilioni 20.1 kwa ajili ya ujenzi wa meli tatu; mbili zikiwa za mizigo na moja ya abiria na mizigo.

Tayari mbili, MV Njombe na MV Ruvuma ambazo ni za mizigo zimeshakamilika na hivyo kuanza kufanya kazi, huku MV Mbeya II, meli ya kwanza ya kisasa katika mwambao wa Ziwa Nyasa ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika. Ujenzi wake unaendelea katika bandari ya Itungi.

Meli hiyo ina urefu wa meta 57.4 (zaidi kidogo nusu ya uwanja wa mpira) na upana wa meta 11. Itakapomilika, itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 kwa wakati mmoja. Ujenzi wake unaosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), unatajwa kugharimu Sh bilioni 9.1.

Nyingine mbili za mizigo zimegharimu Sh bilioni 11 na kila mmoja ina uwezo wa kubeba tani 1,000 kwa wakati mmoja.

Kasi ya maendeleo Kwa mujibu wa Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abed Gallus, kukamilika kwa ujenzi wa meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II kunatarajiwa kutatua changamoto za usafiri wa abiria na mizigo katika mwambao wa Ziwa Nyasa, lakini pia kuchochea kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi katika ukanda huo.

“Serikali kupitia TPA inafanya kila linalowezekana kuboresha hali ya usafiri na usafirishaji wa majini katika kila kona ya Tanzania, na hapa kwetu katika Ziwa Nyasa tayari meli mbili za mizigo zilizoahidiwa na Rais Magufuli zinafanya kazi tangu kukamilika kwake mwaka jana, na sasa hii ya abiria nayo inakamilika. Matarajio ni ndani ya mwezi huu.

“Hatua iliyobakia ni ya kukamilisha mradi huo wa meli kwani inahusisha ufungaji wa mitambo ikiwa ni pamoja na injini, kuweka vyumba, kufunga viti na umaliziaji wa shughuli nyingine. Kwa ujumla chombo kimekamilika kwa kiasi cha kuridhisha,” anasema Gallus.

Anaongeza kuwa, meli hiyo ya abiria inatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa watumiaji wa usafiri wa majini kutokana na ukweli kwamba itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo na abiria kwa wakati mmoja.

MV Mbeya II inatarajia kufanya safari zake katika bandari mbalimbali kongwe na nyingine mpya zitakazoanzishwa na TPA katika mwambao wa Ziwa Nyasa ili kuleta ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo ziwani.

Bandari 15 kufikika Kwa upande wa Tanzania, Ziwa Nyasa lina bandari 15 zilizopo katika mikoa mitatu ya Mbeya, Njombe na Ruvuma, huku bandari kuu zaidi ikiwa Itungi, wilayani Kyela, Mbeya.

Nyingine kuu ni Kiwira na Matema za wilayani Kyela, Mbamba Bay, Liuli na Ndumbi za wilayani Nyasa mkoani Ruvuma na bandari ya Manda iliyopo Ludewa, Njombe.

Aidha, Mamlaka inasimamia bandari ndogo nane katika ukanda wa Ziwa Nyasa ambazo ni Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde na Lupingu wilayani Ludewa, wakati kwa upande wa wilaya ya Nyasa zipo bandari za Lundu, Nkili na Njambe.

Maboresho ya bandari Sambamba na kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo, TPA pia imeelekeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya bandari zake katika bahari na maziwa makuu, za Ziwa Nyasa zikiwemo.

Gallus anataja maboresho mengine yanayofanyika kuwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi, karakana na gati lenye urefu wa meta 70 katika bandari ya Itungi ambavyo vimekamilika.

Katika bandari ya Kiwira, anasema kumejengwa gati lenye urefu wa meta 15 na ghala lenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 1,000 za shehena mbalimbali.

Katika Bandari ya Ndumbi inayotumika kupakia makaa ya mawe kutoka mradi wa Ngaka, wilayani Mbinga, Ruvuma kunatarajiwa kujengwa gati la kudumu sambamba na ujenzi wa ofisi, nyumba za wafanyakazi na sakafu ngumu.

Ujenzi huo utahusisha pia ununuzi wa vifaa kama mashine za kuinua vitu vizito, malori ya kusombea makaa ya mawe na kadhalika.

“Uboreshaji huu unatarajiwa kuongeza ufanisi katika upakiajia makaa ya mawe katika bandari ya Ndumbi kwa kupunguza idadi ya siku zinazotumika kupakia kutoka siku mbili na nusu hadi saa 12 tu,” anasema meneja huyo.

Kwa upande wa bandari za Liuli, Manda na Mbamba Bay, kuna ofisi na nyumba za wafanyakazi. Pia Mbamba Bay kumejengwa gati lenye urefu wa meta 15.

Ufanisi maradufu Maboresho hayo, kwa mujibu wa Gallus, yamesaidia kuongeza ufanisi ambao umeanza kuonekana katika bandari za Ziwa Nyasa

. Anatolea mfano kuwa, mapato katika bandari 15 ndani ya ziwa hilo hayakuwahi kuvuka Sh milioni 298, lakini sasa wanakadiria kuwa na uwezo wa kukusanya Sh bilioni 2.4 katika mwaka huu wa fedha, hivyo kuzifanya bandari hizo kuanza kujiendesha kwa mara ya kwanza bila ya kutegemea ruzuku kutoka makao makuu ya TPA.

Aidha, kabla ya ujio wa meli mpya za mizigo, uwezo wa bandari ulikuwa ni kusafirisha tani 3,600 tu hadi mwaka uliopita wa fedha, lakini katika mwaka huu wa 2018/19 bandari hiyo inatarajia kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena hadi kufikia zaidi ya tani 30,000.

Malengo ya mwaka ujao wa fedha, yaani 2019/2010 ni kuhudumia tani 136,000 kwani mizigo zaidi ya makaa ya mawe, saruji, clinker na mingine, inatarajiwa kuongezeka kwa kasi.

Faida kwa ujumla Mbali ya kuishukuru Serikali chini ya utawala wa Rais Magufuli, Gallus anaipongeza TPA chini ya uongozi wa Deusdedith Kakoko kwa kasi ya maendeleo na uboreshaji wa bandari zake.

Anasema kwa upande wa Ziwa Nyasa wanatarajia faida nyingi mno, ikiwa ni pamoja na kuboresha shughuli za usafirishaji na mzunguko wa kibiashara katika ukanda huo kuongezeka, hasa kuanzia Januari mwaka huu.

Anasema awali, hali ya usalama wa abiria na mali zao haikuwa na uhakika kutokana na kutegemea zaidi mashua, boti, ngarawa na kadhalika, vyombo ambavyo havikuwa salama sana hasa katika ziwa hilo linalotajwa kuwa miongoni mwa maziwa yenye mawimbi makubwa na hatarishi yanayofikia ukubwa wa hadi meta 2.5.

Kiuchumi, mbali ya kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi wakati wa ujenzi hadi kuanza kutumika kwa meli hizo, Gallus anasema uwepo wa meli utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa katika maeneo yanayopitiwa na bandari.

Anatoa mfano kuwa, kusafirisha tani moja ya makaa ya mawe kutoka Ngaka hadi Kiwira, ni wastani wa Sh 110,000 kwa njia ya barabara, lakini kwa usafirishaji kwa njia ya Ziwa Nyasa gharama haizidi Sh 97,500.

Pamoja na kuokoa gharama, anasema meli hizo zinatarajia kupunguza idadi kubwa ya malori barabarani na hivyo kuipunguzia serikali mzigo wa ukarabati wa mara kwa mara wa barabara zinazoharibiwa kila kukicha na malori ya mizigo. Gallus anatoa mfano kuwa, meli moja ya kubeba tani 1,000 za mizigo ni sawa na malori 33 yenye uwezo wa kubeba tani 30 kila moja.

Akizungumzia pia faida katika kupunguza athari za mazingira, menaja huyo anasema meli inazalisha kiasi kidogo cha hewa ukaa kutokana na matumizi madogo ya mafuta ikilinganishwa na kiasi kinachoweza kuzalishwa na malori 33 kwa kila tani 1,000.

"Kwa meli, ili kusafirisha makaa ya mawe kutoka bandari ya Ndumbi hadi Kiwira, kiasi cha mafuta kinachoweza kutumika ni lita kati ya 2,000 na 2,200. Kwa lori ni wastani wa lita zisizopunguza 300 kusafirisha mzigo kati ya maeneo hayo, sasa angalia kama una tani 1,000 maana yake malori 33 kila moja litumie mafuta lita 300. Ni takribani lita 10,000. hapo kiuchumi fedha inateketea sana, lakini pia kimazingira athari ni kubwa kwa kutumia malori," anasema.

Mwanga wa mafanikio Anasisitiza kuwa, tangu kuanza kwa maboresho chini ya usimamizi wa TPA, mwanga wa mafanikio kuelekea ukuaji kiuchumi unaonekana katika bandari zilizoko Ziwa Nyasa, huku akiwataka wadau kuiunga mkono serikali iweze kuboresha huduma kwa upande wa bandari.

Ujio wa meli na uboreshaji wa miundombinu umepongezwa na wakazi wa mwambao huo, miongoni mwao akiwa mfanyabiashara, Albert Mwaohojo anayesafirisha bidhaa kutoka kisiwa kimoja hadi kingine.

Mwaohojo anasema uwepo wa usafiri wa uhakika utawasaidia kuokoa muda walioupoteza njiani kwa kutumia magari au boti na mashua katika mazingira hatarishi.

“Hali ya usafirishaji bidhaa haikuwa rafiki, iwe majini au huko barabarani kwa sababu nyakati kama za masika hali haikuwa nzuri. Lakini ujio wa meli hizi hakika ni ukombozi na siku si nyingi mtashuhudia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo kwa ujumla katika ukanda huu,” anasema Mwaihojo aliyekuwa katika bandari ya Itungi.

Akizungumzia Ziwa Nyasa linalotajwa kuwa na aina nyingi za samaki, takribani 1,500, lakini wachache wakivuliwa kwa chakula na wengine wakiuzwa nje ya Afrika, mvuvi Atubone Mwakinyamana, alisema sasa wanaona nuru, kwani watakuwa na uwezo wa kufanya uvuvi wenye tija kwa kuwa kuna usafiri wa uhakika.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia sekta za Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo mapema mwaka jana, alisema ni matarajio ya Serikali ni kuwa meli mpya kaika ziwa hilo zitainua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Aliongeza kuwa, anaamini zitaondoa pia changamoto ya usafiri, kupunguza gharama ya usafiri kwa kuwa usafiri wa meli ni wa gharama nafuu zaidi, hivyo kushauri wafanyabiashara kutumia meli hizo kusafirisha mizigo yao.

Pia alitoa maelezo kwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kufunga mitambo ya kisasa ya mawasiliano kwenye meli hiyo ili abiria wapate mawasiliano muda wote wakiwa safarini ndani ya Tanzania, Malawi au Msumbiji ambako meli ya abiria itatoa huduma zake.

Hakika kwa uamuzi wa Rais Magufuli na Serikali yake, kuna nafasi kubwa ya kuifungua kiuchumi na maendeleo mikoa ya mwambao ya Ziwa Nyasa.

Bila shaka ni suala la wakati tu kuweza kujionea ‘ndoto’ za Rais na wananchi wake zikitimia.

RIPOTI inayotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa (IPCC) mara ...

foto
Mwandishi: Eric Anthony

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi