loader
Picha

Vijana 125 wajifunza kilimo Israel

USHIRIKA wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUGECO) kwa kushirikiana na uongozi wa chuo hicho (SUA), umewezesha vijana 125 kwenda nchini Israel kwa ajili ya kujifunza teknolojia za kilimo, mifumo ya uzalishaji, masoko, ujasiriamali na kubadilisha fi kra na mtazamo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sugeco, Revocatus Kimario alisema hayo hivi karibuni katika taarifa yake mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kufundisha vijana kujenga vitalu nyumba na ulimaji wa mbogamboga kibiashara kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba.

Alisema jumla ya wataalamu 50 ambao ni wahandisi wa kilimo, maji na umwagiliaji wa vipando na udongo wa mbogamboga na matunda na wengine wa uchumi na biashara kilimo, walijengewa uwezo wa kufundishwa teknolojia ya kitalu nyumba. Hata hivyo Kimario alisema vijana hao walipelekwa nchini humo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kwa mwaka huu vijana 45, wapo nchini humo kujifunza kwa muda wa mwaka mmoja. Alisema wanaporudi huwafundisha vijana wenzao na wengine wamefanikiwa kujiunganisha na kuanzisha kampuni.

Tayari vijana watatu wameweza kupata mkopo wa zaidi ya Sh milioni 200 kutoka Benki Maendeleo ya Kilimo na hivi sasa wanaendesha kilimo cha mbogamboga wilayani Rufiji, mkoani Pwani. Alisema kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Sugeco imewafikia vijana 5,000 kuwahamasisha kuingia kwenye kilimo hususani kilimo biashara baada ya kufanyia kazi mambo ya msingi ikiwemo kubadili fikra na mitazamo yao.

Aidha vijana hao baada ya kupewa stadi na ujuzi stahiki wa elimu ya ujasiriamali na jinsi ya kutunza fedha wameweza kufanya mambo mengi ya maendeleo na sasa baadhi yao wanaendesha miradi ya kuwaingizia kipato. Katika hatua nyingine, Kimario alisema kwa sasa vipo vikundi 15 vinavyowezeshwa na vinavyojihughulisha na shughuli mbalimbali zikiwemo wa kilimo cha vitalu nyumba.

Naye Mtaalamu wa Lishe wa Sugeco, Jolenta Joseph ameeleza kuwa moja ya kazi zinazofanywa na wajasiriamali ni utengenezaji wa biskuti za viazi lishe, mikate na juisi yake. Alisema viazi lishe ni vizuri kwa afya kwa kuwa vina vitamini na madini na virutubishi vingine kwa wingi ambayo husaidia kuondoa utapiamlo na upungufu wa vitamizi A endapo vikitumiwa ipasavyo. Naye mjasiriamali aliyewezeshwa na Sugeco, Veronica Kavishe alisema alifundishwa jinsi ya kutengeneza juisi za aina mbalimbali za matunda na ya viazilishe na sasa biashara yake imekuwa na uhakika wa kumwingizia kipato, ambapo kwa siku anatengeneza juisi lita 200.

MAWAZIRI wa Sekta wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi wa nchi zilizo ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi