loader
Picha

‘Namshukuru JPM kuijenga Mkuranga’

DESEMBA 31, siku ya mwisho kwa mwaka 2018, iliwakuta watu wengi duniani wakiwa katika shauku ya kuuaga mwaka na kuukaribisha mwaka mpya wa 2019 kwa kutembelea maeneo mbalimbali yakiwemo ya ibada, nyumba za starehe pamoja na kutembeleana ndugu, jamaa na marafi ki.

Kwa wananchi wa Wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani, siku hiyo waliitumia kwa kukaa pamoja na mwakilishi wao katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, wakitathmini kwa pamoja mambo ambayo wameyafanya ya maendeleo kwa mwaka 2018 pamoja na mengine ambayo wanatarajia kuyafanya mwaka 2019.

Ulega anasema Mkuranga ilikuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ikiwemo barabara ya kuelekea Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga sambamba na barabara zingine zinazounganisha maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo pamoja na madaraja. Ulega ambaye pia ni Naibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi anaweka wazi kwamba Rais John Magufuli, katika kipindi kifupi alichokaa ofisini ametekeleza ahadi kupitia yeye (mbunge) kwa kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja makubwa katika Jimbo la Mkuranga ambalo halikuwa na bajeti ya kutegenezewa madaraja hayo.

“Nilimwomba Rais Magufuli kunisaidia kutengeneza miundombinu ya Wilaya ya Mkuranga. Mheshimiwa Rais alitoa fedha na mdaraja hayo takribani matano na bado yapo katika hatua za ujenzi. “Tumefanya mambo mengi… lazima nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Nimempelekea mambo kadhaa amenisaidia,” anasema Ulega mbele ya watu zaidi ya 1,000 waliohudhuria mkutano huo wa hadhara.

Anasema mbali na ujenzi wa madaraja hayo kupitia mfuko wa jimbo, ataendelea kuhakikisha barabara za Wilaya ya Mkuranga inayolima korosho kwa wingi inapaa kiuchumi kupitia fedha kutoka serikali kuu na zake binafsi. “Wilaya yetu ya Mkuranga ina viwanda vingi ambavyo vingi vipo barabarani kwa hiyo ni muhimu tuwe na barabara nzuri za lami.

Halikadhalika katika eneo la Mbezi kunapita bomba la gesi na hivyo kuwa eneo zuri pia kwa watu wanaotaka kuwekeza kwenye viwanda na tayari tumetenga eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 10,000, kwa ajili ya viwanda,” anasema na kuwataka wakazi wa Mkuranga kuchangamkia fursa hizo. Ili kuhakikisha barabara zinapitika na kutumika mwaka wote wa 2019, mbunge huyo ameukabidhi uongozi wa Wilaya ya Mkuranga mapipa matano ya mafuta ya dizeli yenye jumla ya lita 1,000 na kuwatia hamasa wananchi wengine kuchangia mafuta hayo kwa ajili ya kulima na kusawazisha barabara za vumbi pale zinapoharibika.

Hata hivyo, anatoa onyo wananchi wasichangishwe fedha yeyote zaidi ya wao kuchangia mafuta. Ulega anasema matayarisho kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ya mikoani yanaendelea vizuri, hali inayotoa hamasa kwa siku zijazo mabasi ya mwendo wa haraka yaweze kufika hadi Mkuranga yakitokea katika ya Jiji la Dar es Salaam.

Kuhusu sekta ya elimu, Ulega anasema: “Tumepata watoto wengi sana wanaoingia kidato cha kwanza tofauti na uwezo wa shule, lakini hili ni jambo jema sana na tutazisidi kujenga shule mpya na kuboresha zilizopo. Kwa mfano mwaka 2018 tulijenga shule mpya tatu za sekondari katika wilaya yetu na kuboresha zilizopo. Tumejenga pia Shule ya Msingi Kipala,” anasema.

Anasema mafanikio katika elimu yanatokana na serikali kuamua kutoa elimu ambapo inatumia shilingi bilioni 25 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia elimu ya msingi na sekondari. Anasema ingawa serikali ya awamu ya tano inatekeleza miradi mingi ya kitaifa ambayo ndio inayotangazwa zaidi lakini haijaziacha wilaya mbali mbali nyuma ikiwemo Mkuranga katika kuzipelekea maendeleo.

Ametaja miradi mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa na Serikali kuwa ni pamoja na kuliimarisha shirika la ndege nchini (ATCL) ambapo Desemba 23 mwaka 2018 serikali ilileta ndege nyingine kubwa ya Airbus A220-300. Anataja miradi mingine mikubwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa uhakika la Stiegler’s Gorge.

Anasema serikali imefanya pia mapinduzi makubwa katika sekta ya afya kuiongezea bajeti maradufu na kusambaza vifaa tiba katika hospitali zote nchini ikiwemo ya Mkuruganga ingawa anasema hospitali hiyo bado ina changamoto kadhaa ikiwemo ya uhaba wa shuka iliyosababisha watu wengi kumpigia simu. Anasema katika kupambana na uhaba huo wa shuka alilazimika kununua shuka 100 kwa ajili ya hospitali hiyo kwa gharama ya Sh 1,100,000. Maelezo hayo yalimnyanyua mkazi mmoja wa Wilaya hiyo, Hamduni Mohamed aliyehudhuria mkutano huo na kuchangia fedha taslimu Sh 500,000 kwa ajili ya ununuzi wa shuka zaidi katika hospitali hiyo ya wilaya.

Ulega pia anamtaka Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Dk Stephen Mwandambo, kuhakikisha wazee waliopatiwa vitambulisho kwa ajili ya kupata huduma bure wanapatiwa huduma hizo kwani amekuwa pia akipata malalamiko ya wazee hao kusumbuliwa. Kuhusu maji ambayo bado ni changamoto katika maeneo mengi ya wilaya yake, Ulega anasema: “Tuna zaidi ya Sh bilioni tatu ambazo zimetengwa kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji katika Wilaya ya Mkuranga.” Anasema serikali ina dhamira ya kuhakikisha maji yanafika katika maeno mengi ya wilaya hiyo kadri inavyowezekana ili kuwaondolea adha wananchi.

Katika kusaidia makundi, Ulega anasema akinamama katika makundi yao walipatiwa kuku kwa ajili ya uzalishaji kibiashara na kwamba kwa sasa makundi mengine yanaangaliwa ili pia yawezeshwe. Kutokana na uchumi wa wilaya kutegemea kilimo cha korosho, Ulega anawataka wakulima wa zao hilo kuwa na subira na kwamba watapata haki yao kwa kuwa Rais Magufuli anaongoza kwa haki na ndio maana anafanikiwa na hana nia ya kumuumiza mnyonge.

Naibu Waziri huyo anawataka pia wananchi kuchangamkia fursa zilizpo katika sekta ya mifugo hususan ng’ombe wa maziwa kwa kuwa serikali imeweka katazo la viwanda vya ndani kuagiza maziwa kutoka nje ya nchi ili wananchi waweze kupatiwa fursa hiyo ya kuuza maziwa kwenye viwanda vya maziwa. Anasema Mkuranga ni kati ya wilaya ambayo patawekwa kituo cha kupokelea maziwa kutoka kwa wafugaji. Ulega pia anawahakikishia wapiga kura wake kwamba umeme utazidi kusambazwa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mkuranga kwa ajili ya kufungua fursa katika maeneo kadhaa katika kipindi cha mwaka huu wa 2019.

Katika kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuchapisha vitambulisho kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, Mbunge huyo alitumia mdhadhara huo kulipia vitambulisho 250 kwa ajili ya wanawake wanaofanya biashara ndogo ndogo huku akiahidi kulipia vitambulisho vingine 250 kwa ajili ya makundi mengine. Anasema vitambulisho hivyo ni mkombozi kwa wafanyabiashara ndogo ndogo na hivyo kuwataka wafanyabishara kuvichangamkia ili kutambuliwa rasmi na kuondokana na usumbufu wanapopita katika maeneo mbalimbali wakifanya biashara zao.

Katika hatua nyingine Ulega analalamikia uwepo wa mashamba pori kutokana na baadhi ya watu kununua maeneo na kuyaacha bila kuyaendeleza huku baadhi ya vijana katika wilaya yake wakiwa hawana maeneo ya kutosha kwa ajili ya kilimo. “Ninawataka walionunua mashamba katika Wilaya ya Mkuranga wayafanyie kazi ili yawe na tija badala ya kuyaacha mapori,” nasema.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Edward Kondela

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi