loader
Picha

TRA kusikiliza kero kila alhamisi

KUANZIA sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeamua kila siku ya Alhamisi, itakuwa ni siku maalumu kwa ajili ya mameneja wa mikoa na wilaya nchini, kuwasikiliza na kutatua changamoto za walipakodi.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema hayo alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu makusanyo ya kodi kwa kipindi cha miezi sita kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Kayombo alisema siku hiyo ya Alhamisi, itawahusu mameneja wote wa TRA wa mikoa nchini ili kuweza kutatua kero hizo zinazowakabili wananchi kuhusu masuala ya kodi.

“Tumekuwa na maelekezo mbalimbali tuliyopewa na Rais ikiwa ni pamoja na malalamiko ya walipa kodi. Ili kuwa na kitu chenye mwendelezo kila Alhamisi itakuwa ni siku ya kuwasikiliza wananchi kwa mameneja wote wa mkoa nchini.

“Kuna malalamiko baadhi ya walipa kodi wamekadiriwa mapato makubwa huenda baadhi ya malalamiko hayo yametokana na kazi zilizofanywa na maofisa wa TRA,” alisema.

Sambamba na hilo, ili kuongeza ufanisi na kuwa karibu na walipa kodi, TRA imefungua kituo maalum cha ushauri kwa walipa kodi kwa Mkoa wa Dar es Salaam kilichopo jengo la Shirika la Nyumba (NHC) mtaa wa Samora na Bridge. “Vituo vingine vitaendelea kufunguliwa katika mikoa mingine,” alisema.

Alisisitiza kuwa wananchi wenye shida yoyote wana uhuru wa kufika katika kituo hicho kwa ajili ya kujieleza na kupata ushauri ama kuomba maelekezo ya aina yoyote.

Pia Kayombo alisema katika kuongeza wigo wa walipakodi, mamlaka hiyo imeanza kampeni rasmi ya usajili wa walipakodi wapya kote nchini kwa kuwapatia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) bure katika maeneo wanayofanyia biashara.

“Katika kuongeza wigo wa walipakodi TRA wameanza kampeni nchi nzima kila mfanyabiashara anapaswa kusajiliwa na kupata tin bure bila malipo.

“Tunajaribu kuboresha mazingira bado kuna maeneo tunaendelea kufanyia kazi kuwezesha mazingira ya mlipakodi kuwa rahisi,” alisema.

Pia mamlaka hiyo inawakumbusha wamiliki wa majengo nchini, kulipia kodi ya majengo, ambayo viwango vyake ni Sh. 10,000 kwa nyumba za kawaida, Sh. 50,000 kwa kila sakafu ya ghorofa na Sh. 20,000 kwa ghorofa za wilayani na vijiji.

Katika hatua nyingine TRA imewasisitiza wafanyabiashara wadogo kuchangamkia vitambulisho vya wamachinga, ambavyo vinapatikana nchi nzima katika ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya kwa Sh. 20,000.

Vitambulisho hivyo ni maalumu kwa wale tu, ambao mauzo yao ghafi hayazidi Sh. milioni nne kwa mwaka.

Alitoa wito kwa walipakodi na wananchi wote, kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Awali akielezea makusanyo ya kodi kwa kipindi cha miezi sita kwa mwaka wa fedha 2018/19, Kayombo alisema TRA imefanikiwa kukusanya Sh. trilioni 7.99 kwa kipindi cha miezi sita ya mwaka wa fedha 2018/19 ikiwa ni kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, ikilinganishwa na Sh. trilioni 7.83 ambazo zilikusanywa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha wa 2017/18. Alisema kiasi hicho ni sawa na ukuaji wa asilimia 2.01.

Alisema makusanyo ya Desemba mwaka jana, yaliongezeka kuzidi makusanyo ya miezi yote iliyopita kwa mwaka huu, ambapo TRA ilikusanya Sh. trilioni 1.63 ambapo kwa Novemba mwaka jana ilikusanya Sh. trilioni 1.21 na Oktoba mwaka jana zilikusanywa Sh. trilioni 1.29.

WABUNGE wameitaka serikali ije na mkakati wa kurejesha biashara ya ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi