loader
Picha

Mwafaka lugha ya kufundishia shuleni, vyuoni unahitajika

SERA ya Elimu ya Tanzania inasema Kiswahili kitatumika kama lugha ya kujifunzia mpaka chuo kikuu, hata hivyo hali halisi haiko hivyo! Je, jambo hili litatekelezwa lini? Tafiti zote zilizowahi kufanywa, zikiwemo za Mlama & Matteru (1978); Criper & Dodd (1984); Campbell na Qorro (1986); Msanjila (1990); Mulokozi (1991), Rubagumya (1995) Kiputiputi (1996); Mtembei (1997) n.k. zinaonesha kuwa Kiswahili ni bora kikitumika kama lugha ya kufundishia shule za sekondari na chuo kikuu.

Profesa Mshiriki kutoka Kitengo cha Stadi za Mawasiliano cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Martha Qorro aliyewahi kufanya utafiti kuhusu ‘Uwezo wa Kusoma na Kuelewa Vitabu vya Kiingereza kwa Wanafunzi’ mwaka 1986, anabainisha umuhimu wa Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia. Katika utafiti huo, Profesa Qorro akishirikiana na Dk Zaline Roy- Campbell waligundua kuwa, uwezo wa wanafunzi wa sekondari kusoma na kuelewa vitabu vya kiada ni mdogo kiasi kwamba, kati ya asilimia 94 ya wanafunzi hawawezi kusoma na kuelewa vitabu vinavyotumika shuleni.

Profesa Qorro katika wasilisho lake kwenye kongamano lililoandaliwa na taasisi ya HakiElimu mwaka jana, anaonesha masikitiko yake kuwa, licha ya kuwapo kwa kamati zaidi ya 20 zilizofanya utafiti na kuthibitisha kuwa lugha ya Kiingereza haifai kufundishia, suala hili halijafanyiwa kazi. Anasema nchi zinazoendelea zimerithi mfumo wa elimu kwa maslahi ya wakoloni, ndiyo maana kila nchi ya Afrika inatumia lugha ya nchi iliyoitawala.

Akataka jamii ijiulize; “Sisi ni nani na tunakwenda wapi”? Halikadhalika, Profesa Aldin Mutembei kutoka UDSM, anaunga mkono matumizi ya Kiswahili na kuwalaumu wamiliki wa shule za binafsi kuwa wanatetea Kiingereza kwa sababu za kibiashara. Mutembei pia alifanya utafiti kuhusu suala la lugha mwaka 1997. Anasema lugha za mataifa mengine tunazozisifia kuwa, zilikomaa kutokana na juhudi za makusudi za kuzikuza na kuzitumia katika shughuli zao za kila siku. Mutembei anakumbusha kuwa, iwapo lugha haiwatoshelezi watumiaji wake katika haja zao, basi ni kosa la hao watumiaji wake na siyo la lugha yenyewe.

Mchunguzi wa Lugha ya Kiswahili, Profesa Yohana Msanjila wa Chuo Kikuu cha St John cha Tanzania (SJUT), akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1986 alichunguza hali ya ufundishaji kwa Kiswahili katika vyuo vya ualimu na katika ripoti yake ya uchunguzi iliyochapishwa 1990. Katika utafiti wake, alibaini kwamba ingawa zipo istilahi za kutosheleza ufundishaji wa Kiswahili, bado walimu hawazitumii katika ufundishaji kwa kuwa walimu hao wamepata mafunzo yao kwa lugha ya Kiingereza.

Anabainisha kuwa, walimu hawana marejeo ya vitabu vya Kiswahili, na mojawapo ya mapendekezo ya mchunguzi huyu ni kwamba, Kiswahili kifanywe lugha ya kufundishia katika shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu ili kukiwezesha kuimarika na kueneza istilahi za Kiswahili. Kwa kweli kumekuwepo mijadala mingi na kwa muda mrefu kuhusu lugha ya kufundishia, tangu tulipopata uhuru mwaka 1961 lakini hadi leo hali imeendelea kuwa kama ilivyo, japo watetezi wa Kiswahili hawajakata tamaa, licha ya safari ndefu ya kukipigania.

Mjadala kuhusu suala hili umekuwa ukiwagawa wasomi katika kambi mbili, moja ikitetea lugha ya Kiingereza na wengine wakitaka Kiswahili kitumike kufundishia katika mfumo wote wa elimu kama ambavyo sera ya elimu Tanzania inasema. Mmoja wa wasomi wanaopinga matumizi ya Kiswahili katika kufundishia ni Mhadhiri na mtaalamu wa lugha ya Kiingereza, Dk Michael Kadeghe ambaye haamini kuwa Kiswahili kinaweza kuwa suluhisho la elimu bora. Halikadhalika Mhadhiri wa Elimu kutoka Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu (DUCE), Dk Luka Mkonongwa anabainisha: “Lugha ni kitu kidogo, ila mifumo tunayotumia kufundishia, maarifa aliyo nayo mwalimu na mazingira aliyo nayo mwanafunzi ndivyo vitu vinavyotakiwa. Lugha ni kitu kidogo tu.”

“Tunasema Kiingereza ni lugha ya kigeni, siyo kweli. Tumekuwa nayo miaka 50 sasa, wataalamu wote wamefundishwa kwa Kiingereza halafu tunageuka tunasema ndiyo shida.” Kimsingi, mgawanyiko wa mawazo kuhusu lugha ya kufundishia si tu umeathiri mfumo wa elimu nchini, bali pia umezalisha aina mbili tofauti za wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu katika mfumo mmoja.

Hali hii ilimfanya Casmir Rubagumya ambaye sasa ni Profesa wa lugha katika Chuo Kikuu cha St. John cha Tanzania (SJUT) kuchunguza utumiaji wa lugha mbili katika shule za sekondari. Katika makala yake iliyochapishwa 1994 akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, walimu wanatumia lugha zote mbili Kiswahili na Kiingereza katika ufundishaji ili kuwa na maelewano yenye manufaa kati ya mwalimu na mwanafunzi. Hali hii inatokana na sera kumlazimisha mwalimu kufundisha kwa Kiingereza ili kuwatayarisha wanafunzi kwa ajili ya mitihani inayotungwa kwa Kiingereza.

Wakati huohuo, ujuzi wa Kiingereza wa wanafunzi ni mdogo na ili wanafunzi waweze kuelewa wanachofundishwa, walimu wanaamua kupuuzia kanuni na kufundisha kwa Kiswahili au kufafanua baadhi ya istilahi kwa Kiswahili. Utafiti wa Rubagumya unaonesha kuwa tatizo la Kiingereza si la wanafunzi, bali hata baadhi ya walimu wanapata shida kufundisha kwa Kiingereza.

Kwa hali hii ndiyo maana sisiti kukubaliana na wote wanaotaka lugha ya Kiswahili itumike kufundishia, kwa kuwa kutoa elimu kwa lugha ya kwanza au lugha inayoeleweka kunampa mtoto fursa nzuri ya kuunganisha elimu na maisha ya kawaida. Pia, kunampa mzazi fursa ya kuchangia katika uelimishaji. Kiingereza kwa Tanzania ni ukuta unaozuia muunganisho huo, kwani wazazi wengi wanazungumza Kiswahili wakati elimu inatolewa Kiingereza, hivyo kumnyima mzazi haki na jukumu la kufuatilia elimu ya mwanawe.

Matokeo yake ni kwamba, jukumu la elimu limeachwa kwa walimu peke yake, ambao pia Kiingereza hawakimudu. Imebainika kuwa, baadhi ya wazazi pia wanafikiri wajibu wao ni kuwa na pesa nyingi ya kumpeleka mtoto katika shule binafsi ili apate elimu bora inayoaminika kuwa ni ile inayotolewa kwa Kiingereza. Hapa kuna umuhimu wa watu kuelimishwa nini maana ya elimu na tofauti iliyopo baina ya elimu bora na lugha ya Kiingereza. Elimu bora inaweza kuwa kwa lugha yoyote. Kuna uwezekano wa kujifunza Kiingereza bila kufanya lugha ya kutolea elimu. Kadhalika, kuna uwezekano wa kuongea Kiswahili bila kuchanganya na Kiingereza. Kuchanganya si ujanja, ni upungufu wa ustadi katika lugha.

Mtu aliye stadi katika lugha ni yule anayeweza kuzungumza lugha moja kwa ufasaha wake. Pia thamani ya elimu ni maudhui, si kujua kusema ‘Yes’ au ‘No’. Kama una maudhui mazuri kwa lugha yako dunia yote itakutafuta na kutafsiri. Si kubabaisha kwa kutumia lugha ya watu. Kumbuka kuwa Kiingereza ni lugha, si elimu. Elimu itolewe kama elimu na lugha ifundishwe kama lugha. Hivyo ndivyo nchi za wenye kujitambua zinavyofanya. Hivi Watanzania tunafikiria nini kwa watoto kujifunza maudhui ya Kiswahili kwa kutumia Kiingereza? Ni kama Mchina kuamua kujifunza maudhui ya Kichina kwa kutumia Kiswahili, au Mwingereza kujifunza maudhui yake kwa kutumia Kichina! Huu si uwendawazimu? Si vyema kuchukua lugha ya mgeni kujielimisha kuhusu mambo yanayokuhusu.

Elimu bora haimaanishi Kiingereza. Elimu bora ni maudhui. Na ili maudhui hayo yawafikie walengwa, ni lazima itolewe kwa lugha inayoeleweka. Inashangaza hata pale unaposhuhudia mwanafunzi wa Kitanzania kutumia Kiingereza kujifunza somo la Uraia, ambalo msingi wake ni kumsaidia kujitambua! Ninavyoamini, lengo la kujifunza lugha ya kigeni ni kusaidia kuwasiliana na mgeni, siyo kwa ajili ya kuwasiliana sisi kwa sisi, kwani sisi tayari tuna lugha na hatuna haja ya kutumia lugha za watu kujielimisha kwa mambo yanayotuhusu.

Binafsi naamini kuwa, mfumo wa mtoto kuanza elimu ya msingi akifundishwa miaka yote saba masomo yote kwa Kiswahili isipokuwa somo la Kiingereza, kisha anapoingia sekondari masomo yote kufundishwa kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili nadhani unaleta mkanganyiko mkubwa. Mkanganyiko huu unajitokeza kwa kuwa mwanafunzi anapoingia kidato cha kwanza, huanza kujifunza mambo mageni kwa lugha ya kigeni na hivyo kuufanya mfumo huu kuzalisha vijana wenye uwezo wa juu wa kukariri na si vijana wenye uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo.

Matokeo yake wanafunzi wa Kitanzania wanajikuta wakiwa hawajui Kiswahili wala Kiingereza. Mtindo huu wa ufundishaji umekuwa ukizima vipaji vingi na kuvilazimisha kukariri na mwisho kuviandaa vipaji hivyo kuwa mafisadi, kwani ufisadi unaanzia kwenye wizi wa mitihani na ‘madesa’. Kutumia Kiingereza tunawapa wanafunzi majukumu mawili; kujifunza lugha kwanza, halafu kuanza kutafsiri maudhui katika Kiswahili ili kupata ujumbe. Hiyo ni biashara kubwa unayouipa ubongo, na wachache ndio hufanikiwa kufanya biashara hiyo. Wengi wanaishia kukariri na kufaulu mtihani basi. Nadhani sasa tuamue kuhusu lugha ya kufundishia badala ya kuendelea na mkanganyiko huu unaoifanya elimu yetu kuwa kama kichekesho.

JUNI 20 ni Siku ya Wakimbizi Duniani, inayoadhimishwa tarehe kama ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi