loader
Picha

Wachimbaji wakwepa kodi kunyimwa leseni

SERIKALI imesisitiza kuwa haitatoa leseni kwa wachimbaji wa madini wanaofahamika kuwa si waaminifu na wamekuwa wakitumia sababu mbalimbali za kujitungia kukwepa kulipa kodi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema hayo kijijini Itumbi kata ya Matundasi wilayani Chunya alipokuwa akijibu hoja za wachimbaji wadogo juu ya kuchelewa kwa leseni kwa watu walioomba.

Alikuwa akifungua mafunzo ya siku mbili yaliyolenga kutoa matokeo ya utafiti wa kina wa kijiosayansi wa dhahabu.

Msanjila alisema pamoja na kuwa serikali ilisitisha kwa muda utoaji leseni, kwa sasa baadhi ya wachimbaji walioomba wameshaanza kupewa.

Hata hivyo aliwataka kutambua kuwa kwa wale wanaofahamika kuwa si waaminifu wasitarajie kupata leseni mpya.

Katibu mkuu huyo pia alionesha kusikitishwa na hatua ya idadi ya maduhuli ya kodi yanaokusanywa kutoka kwa wachimbaji wadogo kuwa ndogo kuliko ya wachimbaji wakubwa, licha ya kuwa takwimu zinaonesha kada hiyo ndiyo iliyo na leseni nyingi zaidi.

Aliwataka wachimbaji kutanguliza uzalendo wa kulipa kodi wakitambua kuwa serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya mikakati mbalimbali ya kukuza sekta ya wachimbaji wadogo, ikiwamo kuendesha tafiti kubwa kama hiyo ya kijiosayansi iliyogharimu Sh bilioni saba.

"Wizara ya madini tutaendelea kushirikiana nanyi kwa kufuatilia matokeo ya tafiti hizi, namna zinavyotumika na pia itaendeleza nyingine. Lengo hapa ni kuongeza uzalishaji kwenu ili siku moja muwe wachimbaji wakubwa,"alisema.

Alisema serikali inafanya jitihada kubwa na sasa kuna vituo saba vya mafunzo vinavyojengwa. Kati ya hivyo kimoja kiko wilayani Chunya.

“Pia kipo kituo cha mfano cha uchenjuaji dhahabu kinajengwa hapa hapa Itumbi,” alisema na kuhimiza ulipaji kodi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Madini (Stamico), Sylvester Ghuliku alisema utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti madini (GST) na Stamico uliofanyika kati ya Septemba 2016 na Machi mwaka huu, utawezesha wachimbaji wadogo kutoka walipokuwa wachimbaji wa kati hadi wakubwa.

Mjiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti madini Tanzania, Joseph Matalu alisema matokeo ya uchunguzi uliofanyika yaliwezesha ukadiriaji wa mashapo.

Wakizungumzia mafunzo na matokeo ya utafiti huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wadogo mkoani Mbeya (Mbelema), Leonard Manyesha alisema yamekuja kwa muda muafaka kwa kuwa yatawaondolea adha ya kuchimba kwa mazoea pasipokujua ulalo wa mwamba wenye madini chini ya ardhi.

WABUNGE wameitaka serikali ije na mkakati wa kurejesha biashara ya ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Chunya

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi