loader
Picha

Makumbusho yatakiwa kujiendesha kibiashara

TAASISI ya Makumbusho ya Taifa nchini imetakiwa kubadilika na kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa kufanya biashara ya huduma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inatekeleza maagizo ambayo imeelekezwa kuyafanya.

Taasisi hiyo imeagizwa kujenga makumbusho ya marais katika mkoa wa Dodoma, ujenzi wa makumbusho ya tembo, ujenzi wa nyumba za jamii za Watanzania katika Kijiji cha Makumbusho, uendelezwaji wa vituo vya malikale, ujenzi wa jengo la kuhifadhia magari yaliyopo Makumbusho na hata kurejesha mikusanyo ya mijusi aina ya Dinosaur iliyoko nje ya nchi.

Maagizo hayo kwa taasisi hiyo yametolewa na viongozi kwa nyakati tofauti yakitakiwa kutekelezwa katika mipango mikakati ya Makumbusho.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika Makumbusho ya Nyumba ya Utamaduni, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema ni muhimu Taasisi ya Makumbusho kubadilika na kufikiri zaidi kibiashara.

"Mjitangaze, mna mambo makubwa mnayoyafanya yaliyomo ndani ya taasisi hii lakini yanaweza yakawa hayafahamiki ipasavyo," amesema Kanyasu na kuwataka kuweka suala la utalii kwa ukaribu zaidi.

Amesema kwa kubadilika makumbusho wanaweza kuwa taasisi au shirika linalotoa gawio kwa serikali kama zilivyo taasisi nyingine.

Kanyasu amesema Makumbusho wanapaswa kuanza utekelezwaji wa maagizo hayo ili kujulikana walikofikia na walikokwama.

"Hivi aliyetoa agizo la kujenga Makumbusho ya marais, akifika atauliza maandalizi yamefikia wapi? Mmekwama wapi...fanyeni kwa awamu, kama hamjaanza basi inawezekana kuonekana haipo kabisa," amesema Kanyasu.

Amesema wanahitaji kuona wanakuwa wabunifu, kuwa imara zaidi, kufikiria kibiashara zaidi huku wakitoa elimu lakini ikiwa kibiashara zaidi.

Awali Kaimu Mkurugenzi katika Makumbusho, Mawazo Jamvi amesema mikakati mikubwa ya taasisi ni kuongeza idadi ya watalii jambo ambalo ni la msingi kwao.

Kuhusu maagizo ya ujenzi wa Makumbusho mbalimbali alisema yapo yaliyotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii na hata Naibu Waziri lakini pia yakiwepo yaliyotolewa na Waziri Mkuu kuhusu kushirikiana na wakuu wa mikoa kujenga nyumba za jamii za Watanzania.

Amesema, utekelezwaji wa maagizo hayo umekuwa ukisuasua kutokana na ufinyu wa bajeti na kwamba, hadi sasa inadaiwa zaidi ya sh milioni 700 za masuala ya uendeshaji.

Jamvi amesema ufinyu wa bajeti umesababisha kushindwa kukarabati majengo na miundombinu ya Makumbusho zilizopo nchini, kukosa vitendea kazi ikiwemo kompyuta na samani nyingine na hata kushindwa kujenga Makumbusho nyingine na kuboresha zilizopo.

Ameitaja changamoto nyingine inayoikabili taasisi hiyo kuwa ni mgongano wa sheria ya Makumbusho ya mwaka 1980 kwa kutotambua Maliasili na kutokutoa muongozo wa utekelezwaji wa mambo ya msingi kama usimamizi wa malikale na urithi kwa ujumla.

Amesema, ipo haja kwa sheria kupitiwa ili Idara ya Malikale iwe chini ya Makumbusho ili kusaidia taasisi hiyo kuongeza mapato yatakayosaidia kutimiza majukumu mbalimbali. Kwa sasa Idara hiyo iko chini ya Maliasili na Utalii.

Alisema changamoto nyingine in tozo za utafiti na kwamba, mtafiti anapokuja nchini huweza kulipa Idara ya Malikale, kulipa katika Taasisi ya Utafiti ya Costech na pia kutakiwa kulipa katika Taasisi ya Makumbusho na kwamba, mgawanyo ni mkubwa hivyo kupunguza idadi ya watafiti wanaokuja nchini.

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Nyantore iliyopo Kijiji cha ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi