loader
Picha

Mashine kunasa mafataki

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imezindua mashine ya kuchunguza vinasaba (DNA) ambayo itakuwa muarobaini kwa watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo kuwapa mimba wanafunzi wa shule na kuwakimbia.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Asha Ali Abdallah wakati akisoma taarifa ya matumizi ya mashine hiyo ambayo ilizinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein sambamba na maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Abdallah alisema kununuliwa kwa mashine hiyo kumekuja baada ya kilio cha muda mrefu cha wananchi pamoja na wanaharakati kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo wanafunzi kupewa uja uzito huku ushahidi ukikosekana.

Alisema kukosekana kwa mashine hiyo na kulazimika baadhi ya vipimo kupelekwa Tanzania Bara na kuchukuwa muda mrefu kupatikana kwa majibu yake, kulitoa mwanya mkubwa kwa watu waliokuwa wakifanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kuwapa uja uzito wanafunzi wa shule.

Aliwataka wafanyakazi wa kitengo cha kuchunguza vinasaba katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kujenga tabia ya uadilifu zaidi katika kutoa matokeo ya uchunguzi wa maabara.

“Matarajio yetu makubwa ni kwamba mashine hii itatumika vizuri kwa kutoa matokeo yanayokubalika na kuondosha utata ambao unaweza kusababisha malumbano na migogoro ya kisheria,” alisema.

Baadhi ya wanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) wamefurahishwa na kuwepo kwa mashine hiyo ambayo ilikuwa moja ya kilio kikubwa kwa ajili ya kudhibiti watu wanaowapa uja uzito wanafunzi na baadaye kukimbiya.

Alisema zipo kesi nyingi za wanafunzi kupewa ujauzito na kulazimika kuacha shule huku wakisubiri majibu ya vipimo vya DNA ambavyo huchukua muda mrefu kupatikana.

“Sisi chama cha waandishi wa habari wanawake Tamwa tumefurahishwa kwa kiasi kikubwa kuzinduliwa kwa mashine ya kuchunguza vinasaba ambayo tunaamini sasa muarobaini wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia umepatikana,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Suleiman Hassan alisema kupatikana kwa mashine ya kuchunguza vinasaba ni hatua moja kubwa ambayo itasaidia kupatikana kwa matokeo ya haraka kwa taarifa za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Alikiri kuwepo kwa sampuli nyingi za vinasaba vinavyotaka kufanyiwa kazi na kupatikana majibu yake yanayohusu mimba kwa wanafunzi lakini kwa bahati mbaya hazijapata majibu zikisubiri wakati wake wa uchunguzi.

“Malalamiko ya Jeshi la Polisi kuzikalia kesi za mimba kwa wanafunzi wakitafuta ushahidi wa kutosha sasa jibu lake limepatikana...mashine ya vinasaba ni muhimu kwa ajili ya kupata matokeo ya kesi zinazohusu mimba kwa wanafunzi wa shule,” alisema.

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Nyantore iliyopo Kijiji cha ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi